Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ongezeni fedha kufadhili miradi ya hatua kwa tabianchi - Guterres

Jengo huko Samoa limezungukwa na maji ya bahari yanayoongezeka, kuonyesha athari za kupanda kwa usawa wa bahari kwa mataifa ya visiwa vya Pasifiki.
United /Kiara Worth Ongezeko la kina cha maji ya bahari lina madhara kwa nchi za visiwa vya Pasifiki, kama inavyooenekana kwenye eneo hili hapa Samoa.

Ongezeni fedha kufadhili miradi ya hatua kwa tabianchi - Guterres

Tabianchi na mazingira

Akiwa Tonga, taifa la kisiwa katika bahari ya Pasifiki Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito akiupatia jina Okoa Bahari Zetu au SOS kutokana na kitisho kinachokumba maeneo ya visiwani kwa sababu ya ongezeko la kina cha maji ya bahari.

Tweet URL

Guterres  akizungumza na waandishi wa habari kwenye mji mkuu wa Tonga, Nuku’alofa, ambako yuko ziarani, amesema ongezeko la kina cha maji ya bahari linatishia paradiso hii ya Pasifiki, wito aliotoa baada ya ripoti kutoka Umoja wa Mataifa kuangazia ongezeko lisilo la kawaida la kiwango cha maji ya bahari sambamba na joto, vikichochewa na utoaji wa hewa chafuzi utokanao na nishati kisukuku.

Tafiti na ripoti kutoka WMO zinasema nini?

Ripoti iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la Hali ya Hewa, WMO kuhusu Hali ya Tabianchi Kusini-Magharibi mwa Pasifiki sambamba na Ripoti ya Timu ya Hatua kwa Tabianchi kutoka Umoja wa Mataifa ikipatiwa jina Ongezeko la Kina cha Bahari katika dunia yenye ongezeko la joto inaonesha kuwa hal inazidi kuwa mbayá na mabadiliko katika baharini na yenye madhara makubwa.

Kwa pamoja ripoti hizo zinaonesha ni kwa vipi viwango vya joto kwenye bahari kila mwezi vinaendelea kuvunja rekodi.

Viwango vya kina cha maji ya bahari vinaongekeza kwa kasi ambayo haijawahi kushuhudiwa katika miaka 3000 iliyopita, huku ukanda wa Pasifiki ukikumbwa na madhara makubwa zaidi.

“Ripoti za hivi karibuni za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa viwango vya joto baharini na matukio ya mawimbi joto baharini ni vikubwa na vinaongezeka kwa kasi,” amesema Guterres.

Hali halisi visiwani Pasifiki

Mafuriko maeneo ya pwani, yakichochewa na ongezeko la kina cha maji ya bahari na vimbunga vinatishia visiwa vilivyoko bahari ya Pasifiki, ambako idadi kubwa ya wakazi wanaishi karibu na pwani.

Viwango vya joto kwenye bahari huko kusini-magharibi mwa Pasifiki vinaongezeka mara tatu zaidi ya wastani wa kiwango cha ongezeko duniani, na kina cha maji ya bahari katika baadhi ya maeneo kinaongezeka zaidi ya sentimeta 15 katika kipindi cha miaka 30 iliyopita, amesema Katibu Mkuu.

“Iwapo viwango vya joto duniani vitaendelea kuongezeka, madhara ya muda mrefu yanawza kujumuisha kupotea kabisa kwa mabamba makubwa ya barafu na uwezekano wa ongezeko la kina cha maji ya bahari kwa hadi mita 20,” amesema Katibu Mkuu.

Wanaume watatu wanafanya kazi kwa kutumia majembe kujenga kizuizi dhidi ya mmomonyoko wa pwani kwenye ufuo huko Tuvalu, huku bahari ikiwa nyuma yao.
© UNICEF/Lasse Bak Mejlvang Wafanyakazi hujenga vizuizi ili kukabiliana na mmomonyoko wa bahari kwenye ufukwe wa Tuvalu.

Sasa nini kifanyike?

Guterres anasema hali halisi hivi sasa inahitaji hatua za dharura kutoka kwa viongozi wa dunia kupunguza utoaji wa hewa chafuzi, kuongokana na nishati kisukuku na kukumbatia hatua thabiti za kuhimili tabianchi.

“Bila hatua za dhahiri na mabadiliko ya haraka, gharama za kiuchumi na kibinadamu zinaweza kufikia matrilioni ya dola , huku miji ya pwani na jamii zao duniani kote wakikabiliwa na hatari kubwa.”

Katibu Mkuu amesema dunia iamua haraka kupunguza madhara hayo na kuzingatia mustakabali endelevu hasa kwa maeneo yaliyo hatarini zaidi kama visiwa vilivyoko bahari ya Pasifiki.

Kwa upande wa jumuiya ya kimataifa, Guterres amesema, “lazima isikie Wito wa Okoa Bahari Zetu na zichukue hatua muhimu kutatua janga la sasa kabla hali haijawa mbaya zaidi.”

Akimulika mkutano wa baadaye mwaka huu wa Umoja wa Mataifa kuhusu tabiachi, Katibu Mkuu amesihi nchi ‘zichagize ufadhili bunifu.’ Nchi tajiri lazima zitimize ahadi zao ambazo ni kuongeze maradufu angalau dola bilioni 40 kila mwaka ifikapo mwaka 2025.