UNICEF yapeleka Gaza dozi za chanjo dhidi ya polio
UNICEF yapeleka Gaza dozi za chanjo dhidi ya polio
Hatimaye shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF linapeleka Gaza huko Mashairki ya Kati dozi milioni 1.2 za chanjo dhidi ya ugonjwa wa polio aina ya 2, wakati huu ambapo ugonjwa huo hatari umethibitishwa kuweko eneo hilo, ikiwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 25.
Kupitia ukurasa wake wa X zamani Twitter, UNICEF inasema dozi hizo milioni 1.2 za chanjo dhidi ya polio zitatumiwa kwa watoto zaidi ya 640,000.
Chanjo hizo zinapelekwa wakati wiki iliyopita shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni, WHO lilithibitisha kuwa mtoto mmoja mwenye umri wa miezi 10 huko Deir al-Balah aliugua polio hiyo aina ya 2 na amepooza sehemu ya chini ya mguu wake. Ingawa hivyo hivi sasa hali yake inaendelea vizuri.
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA, nalo kupitia mtandao wa X linasema kwa kuzingatia hatari kubwa ya kusambaa kwa ugonjwa huo hatari huko Gaza kutokana na ukosefu wa huduma za kujisafi na maji safi, kwa kushirikiana na UNICEF na WHO siku zijazo watazindua kampeni ya chanjo dhidi ya polio kwa watoto zaidi ya laki sita wenye umri wa chini ya miaka 10.
Kwa mujibu wa UNRWA, operesheni za jeshi la Israeli huko Deir Al Balah zimeharibu miundombini ya maji na kwamba ni visima vya maji 3 tu kati ya 18 ndio vinafanya kazi na kwa mantiki hiyo uhaba wa maji ni asilimia 85.