Maonesho ya picha za ICC katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa
Maonesho ya picha za ICC katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa
Na Anold Kayanda
Sheria na Kuzuia Uhalifu Ijumaa Agosti 23 imekuwa siku ya mwisho ya maonesho ya picha yaliyoandaliwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani.
Maonesho haya yanachunguza uhusiano wa pamoja unaooneshwa katika simulizi za watu kutoka hali zote ambapo ICC imeanzisha uchunguzi. Maonesho haya pia yanaangazia baadhi ya wapokeaji wa kwanza wa maagizo ya malipo ya ICC.
Ingawa simulizi hizi zinatoka katika mabara manne, zina ufanano mwingi. Watu wanapoteza nyumba, ardhi na familia zao. Pia zinaonesha jinsi jamii ni muhimu katika kujenga upya maisha.
Simulizi hizi zinazoonekana hapa kwenye picha zimewekwa wazi ili watu waone na waongeze ufahamu kuhusu uhalifu ambao umewatesa wengine na pia kutoa wito wa msaada wa kimataifa kusaidia waathirika.
Maonesho haya yanaonesha mambo yanavyofanana kwa watu wote duniani pindi wanapofanyiwa uhalifu. Kama si kupoteza makazi na ardhi utapoteza ndugu. Pia maonesho haya yanaonesha umuhimu wa jamii katika ujenzi mpya wa maisha.
Utakuwa na roho ngumu sana ikiwa utapita kwenye maonesho haya na moyo wako usifurike majonzi. Sitapitia picha zote lakini angalau kwa uchache utaipata picha.
Picha kutoka Uganda. Paul, 23, anasimulia jinsi alivyotumia ujana wake wote kuyakimbia mashambulizi ya kundi la Lord’s Resistance Army (LRA). Alitekwa nyara akiwa na umri wa miaka 9 1/2, na akakaa miaka 2 akiwa kifungoni msituni. Maafisa wakuu wa LRA walimlazimisha kufanya vitendo vingi vya kutisha.
Aliporudi nyumbani, alipata usaidizi kutoka kwa familia yake. Ndoto yake tangu utoto alipenda kuwa mtaalamu wa afya na ijapokuwa kutekwa kwake kuliichelewesha ndoto yake lakini sasa ameshaitimiza na hapa kwenye picha anaonekana akiandika maelezo ya mgonjwa.
Picha inayofuata hapa ni kutoka Kenya. Maelfu ya vijumba vidogovidogo vya mahema. Kambi ya wakimbizi wa ndani (IDP) huko Eldoret ambapo zaidi ya watu 10,000 walitafuta hifadhi baada ya ghasia za baada ya uchaguzi nchini Kenya mwaka wa 2007/2008.
Pana picha nyingine hapa. Ina maandishi juu, Njaa na Kukata tamaa. Bwana mmoja amekalia sanduku moja, amejiinamia na sanduku jingine liko pembeni yake. Maandishi chini ya picha yanasema Mkimbizi aliyekata tamaa katika kambi ya mpito huko Choucha Ras Djir, kilomita nane kutoka mpaka wa Tunisia na Libya, 27 Februari 2011. Zaidi ya wakimbizi wapya 55,000 kutoka Libya walisajiliwa katika siku kumi kabla ya tarehe ya picha hii. Wakati huohuo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) lilikuwa likijenga kambi mpya ya kuchukua wakimbizi wapya 12,000-15,000.
Kuna picha nyingine, maandishi yake yanasema, ‘kile kinachoitwa vita’. Vita dhidi ya dawa za kulevya. Hii ni kutoka Ufilipino. Binti mdogo tu anaonekana amejikinga kwa mkono wake kuzuia jua kwenye macho yake. Ni nani huyu? “Karla” alikuwa na umri wa miaka 12 shangazi yake alipouawa. Karla alihudhuria maziko, nako huko mazikoni wakashambuliwa. Kukuru kakara, mtoto huyu akajificha chini ya jeneza la shangazi yake, na kutokea hapo alishuhudia baba yake akipigwa risasi. Mauaji yote mawili yanayodaiwa kuwa ni sehemu ya kampeni inayoitwa "vita dhidi ya dawa za kulevya". Karla, akiwa na umri wa miaka 14 kwenye picha hii ya mwaka 2019, anaishi mitaani na kaka zake wawili.
Picha zinaendelea, kama si muda kubana ningekueleza kuhusu DRC, Afrika ya Kati, Palestina, Bangladesh, Darfur Sudan na kwingineko. Matukio yote haya, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ilifuatilia, inafuatilia na hata kuna wanaolipwa fidia.