Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Suluhisho la kisiasa linahitajika kuleta utulivu Mashariki ya Kati

Raia wa Palestina waliokimbia makazi yao wakitembea katika mitaa iliyojaa vifusi huko Gaza huku majengo yakiharibika.
© UNRWA Wakazi wa Gaza wakiitikia amri kutoka Israeli za kuwataka wahame, amri zinazotolewa mara kwa mara bila hata ya kuweko kwa mahala salama pa kukimbilia.

Suluhisho la kisiasa linahitajika kuleta utulivu Mashariki ya Kati

Amani na Usalama

Kuna hatari kubwa ya vita ya Gaza kusambaa kwenye ukanda mzima iwapo hakutakuweko na sitisho la dharura la mapigano na kuachiliwa huru kwa mateka, ameonya Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Mchakato wa Amani ya Mashariki ya Kati, Tor Wennesland.

Akizungumza kutokea Yerusalemu kwa njia ya video wakati wa mkutano wa kila mwezi na Baraza la Usalama kuhusu hali ya Mashariki ya Kati uliofanyika Alhamisi jijini New York, Marekani, Wennesland ameonya kwamba kufanya kosa lolote katika mchakato wa  hali katika Gaza kunaweza kusababisha kupanuka kwa vita na kuingiza mamilioni zaidi katika mgogoro.

Wennesland amesema kuwa, “kusitishwa kwa mapigano mara moja na kuachiliwa kwa mateka huko Gaza kunamaanisha hatua za kidiplomasia za kupunguza mapigano, kurejesha mfumo wa kisiasa wa kumaliza mzozo na kuanzisha suluhisho la mataifa mawili.”

Riyad Mansour, Mwangalizi wa Kudumu wa Nchi ya Palestina, akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama katika UMOJA WA MATAIFA.
UN /Eskinder Debebe Riyad Mansour, Mwakilishi wa Kudumu wa Palestina kwenye UN akihutubia Baraza la Usalama 22 Agosti 2024 kuhusu Mashariki ya Kati

Jaribio lolote la kuzuia utoaji chanjo kitakuwa ni nia ya mauaji ya kimbari - Balozi Mansour

Mwakilishi wa kudumu wa Palestina katika Umoja wa Mataifa, Riyad Mansour, aliunga mkono  pendekezo la kusitishwa kwa mapigano akisema kuwa hilo litaruhusu ugawaji wa chanjo dhidi ya polio na kuokoa maisha ya maelfu ya watoto wa Kipalestina.

Amesema, "jaribio lolote la kuzuia ugawaji wa chanjo hiyo litaonekana kama nia ya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina."

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kudumu wa Israeli katika Umoja wa Mataifa, Balozi Gilad Erdan amesema kwamba Israel imekuwa ikishirikiana na shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni (WHO) na lile la kuhudumia watoto (UNICEF)  kusambaza chanjo huko Gaza.

Ameongeza kuwa "asilimia 90 ya wakazi wa Gaza wamepata chanjo, na kwa sasa kuna kampeni ya kuwachanja watoto walio chini ya umri wa miaka 10 huko Gaza."

Mashirika ya UN yanaendelea kutoa misaada licha ya mapigano

Katika hotuba yake, Wennesland amethibitisha kwamba licha ya kukabiliwa na changamoto kubwa, Umoja wa Mataifa na mashirika ya kibinadamu yanaendelea kutoa msaada wa kuokoa maisha kwa kupitia maeneo yote ya kuvukia yanayopatikana.

“Ikiwa tunataka kuzuia kupanuka zaidi kwa mgogoro, lazima vurugu  na uchochezi vimalizwe. Ukiukaji wowote wa maeneo matakatifu pia lazima ukataliwe vikali,” amesema.

Akitoa pongezi kwa wapatanishi wa amani ikiwemo Misri, Qatar, na Marekani kwa juhudi zao huko Doha na Cairo, Wennesland ameomba pande husika kufikia makubaliano katika siku zijazo. “Hakuna muda wa kupoteza. Hata hivyo, “kusitishwa kwa mapigano kwa muda mrefu tu ndiko kutawezesha majibu kamili ya kibinadamu na urejeleaji wa haraka katika Gaza.” 

Tor Wennesland, Mratibu Maalum wa Mchakato wa Amani wa Mashariki ya Kati, anawasilisha taarifa kwa kikao cha Baraza la Usalama kuhusu hali katika Mashariki ya Kati, ikiwa ni pamoja na suala la Palestina.
UN Tor Wennesland, Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Mchakato wa Amani Mashariki ya Kati, na Mwakilishi Binafsi wa Katibu Mkuu akihutubia Baraza la Usalama kutoka Yerusalemu, wakati lilipokutana kujadili suala la Mashariki y aKati.

Mfumo wa kisiasa ukubalike Gaza

Ili kujenga upya Gaza, Wennesland amesema, “ni muhimu tuanzishe mfumo wa kisiasa unaokubalika na watu wa Palestina na unaoshughulikia matarajio malalamiko yao, huku pia ukishughulikia wasiwasi wa usalama wa Israeli.”

Wennesland amebaini kwamba Mamlaka ya Palestina lazima ipewe kipaumbele katika utawala wa Eneo la Palestina linalokaliwa, akionya kwamba “hakuna mbadala.”

Hata hivyo, ameonya kuwa ili kuhakikisha utulivu na usalama kwa wapalestina na waisraeli, hatua lazima zichukuliwe na pande zote na jumuiya ya kimataifa ili kuimarisha na kuunga mkono mamlaka ya Palestina. 

“Jumuiya ya kimataifa lazima ifanye kazi pamoja ili kushughulikia mgogoro wa kifedha wa muda mrefu wa mamlaka ya Palestina, kuimarisha uwezo wake na kuwezesha kurejea kwake Gaza.”

Hamas wakisambaratishwa, Gaza itajitawala yenyewe - Balozi Erdan

Gilad Erdan, Mwakilishi wa Kudumu wa Israel katika UMOJA WA MATAIFA, akizungumza kwenye jukwaa wakati wa mkutano wa Baraza la Usalama UN mjini New York.
UN Photo/Manuel Elías Gilad Erdan, Mwakilishi wa Kudumu wa Israel katika Umoja wa Mataifa akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu hali ya Gaza.

Akizungumzia suala hilo, Balozi Mansour amesema kwamba Palestina itaanzisha mchakato wa kumaliza kukaliwa  haramu na Israel kwa kutafuta kutungwa kwa sheria kuhusu ushauri wa awali wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki katika mkutano ujao wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Hoja ikajibiwa na Balozi Erdan ambaye amesema  "Israeli haina nia ya kukalia Gaza,  na kwamba mara tu HAMAS itakaposambaratishwa, Gaza itaweza kujisimamia yenyewe. 

Jinsi ya kumaliza mgogoro Gaza

Hatimaye, Wennesland amebaini kwamba njia pekee ya kutoka kwenye janga hili ni upeo wa kisiasa utakaomaliza uvamizi na kufanikisha suluhisho la mataifa mawili. Israeli upande mmoja na upande mwingine Taifa la Palestina lenye uhuru, demokrasia, likiishi kwa amani na usalama ndani ya mipaka salama na inayotambuliwa kwa msingi wa mipaka ya kabla ya mwaka 1967, na Yerusalemu ikiwa mji mkuu wa pande zote mbili.