Manusura wa ugaidi asimulia madhila wanayopitia baada ya kuachiliwa na waasi wa LRA
Manusura wa ugaidi asimulia madhila wanayopitia baada ya kuachiliwa na waasi wa LRA
Hii leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa kumefanyika tukio la siku ya kimataifa ya kukumbuka na kuenzi manusura na waathiriwa wa vitendo vya ugaidi ambapo viongozi waandamizi wa Umoja wa Mataifa na manusura walizungumza na kuelezea misimamo yao. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa ujumbe kwa njia ya video kwa kuwa yuko safarini huko Samoa.
Katika ujumbe wake wa siku hii alioutoa kwa njia ya video Guterres amesema vitendo vya ugaidi vinaleta huzuni isiyoelezeka, na familia na jamii zinazokumbwa na vitendo hivyo husambaratishwa milele huku makovu yanayoonekana na yasiyo onekana hayawezi kupona kikamilifu.
Amesema "tunatoa heshima zetu kwa waathirika na manusura wote, ikiwemo wale waliochagua kutushirikisha simulizi zao kuhusu uvumilivu na msamaha huku tukitafakari juu ya kiwewe walichopitia ili kuelimisha wengine kuhusu vitendo vyao vya ujasiri mkubwa. "
Katibu Mkuu amesema siku hii inahimiza kila mtu kusikiliza na kujifunza na kukumbuka kuwa "lazima wote tutafute nuru ya matumaini. Kwa pamoja, tunaweza kupaza sauti za waathiriwa na manusura wote. Kwa pamoja, tunaweza kusaidia kuelimisha vizazi vya sasa na vijavyo na kwa pamoja, tunaweza kujenga jamii zenye amani na uthabiti zaidi kwa wote.”
Kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya kuwakumbuka waathirika wa ugaidi mwaka huu inasema “Sauti za amani: Wahanga wa ugaidi kama watetezi wa amani na waelimishaji.”
Tunabaguliwa, mahitaji ya kiafya hayajakidhiwa – manusura wa ugaidi
Natumai itifaki imezingatiwa! Jina langu ni Grace Acan, ni manusura wa tukio la kigaidi la kutekwa nyara kaskazini mwa Uganda tarehe 10 Oktoba 1996 na waasi wa kundi la Lord’s Resistance Army, LRA.
Ndivyo alivyoanza hotuba yake kwa washiriki wa tukio la siku ya kimataifa ya kukumbuka waathirika na manusura wa matukio ya ugaidi lililofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa New York, Marekani kwa njia ya mtandaoni na pia ukumbini.
Kati ya 100 tuliotekwa, 70 waliachiliwa huru na 30 tulibakishwa
Grace alihutubia kutoka Uganda akielezea madhila yaliyowakuta yeye na wenzake 100 waliotekwa nyara usiku huo wakiwa kwenye shule ya wasichana ya St. Marys, kaskazini mwa Uganda.
“Tulitekwa 100 lakini baadaye wengine waliachiliwa huku wasichana 30 nikiwemo mimi pia tulisalia na waasi wa LRA kwa miaka minane.” Anasema Grace na kwamba, “tukio hilo lilibadilisha sio tu maisha yangu bali pia ndoto zangu na za wasichana wengine ambao tuliotekwa nao na kushindwa kupata elimu.”
Changamoto: Fidia, Afya na watoto waliozaliwa vitani
“Kukosa elimu, hakuna fidia, hakuna kutambuliwa, licha ya matatizo yote tuliyopitia, ukosefu wa mahitaji muhimu, kila moja lina madhara kwa watoto wetu waliozaliwa vitani. Ubaguzi na matatizo ya kiafya ambayo hayajashughulikiwa, kukosa fedha, na kupoteza wapendwa wetu,” amesema Grace ambaye sasa hivi ni mchechemuzi wa kutetea haki za manusura wa ugaidi nchini Uganda kupitia shirika la kiraia la utetezi wa manusura wa ugaidi na ukatili ambalo yeye ni muasisi mwenza.
Kupitia shirika hilo anasema kwa umoja wao kwa rasilimali chache walizo nazo wameweza kupaza sauti za manusura kwa ajili ya fidia ndani ya nchi, kikanda na kitaifa.
Sasa Grace akawa na ujumbe wa washiriki wa tukio hilo akisema, “kwa niaba ya waathiriwa wote wa ugaidi natoa wito kwa wale wote walioko hapa leo hii, na wale wanaoshiriki tukio kama hili kupitia jukwaa lolote, kuchukua hatua yoyote inayoweza kuleta mabadiliko chanya kwa manusura wa ugaidi. Hii inaweza kuwa kifikra, kijamii, kisheria na kiuchumi. “
Na zaidi yote ametaka ushirikishwaji kuanzia mwanzo akisema “washirikisheni manusura kuanzia kwenye mikakati yoyote inayowahusu. Chukua hatua leo kwani safari ya maili 1000 inaanza na hatua moja.”
Tumejizatiti kusikiliza uzoefu wa manusura na kuzuia ugaidi - Voronkov
Ni kwa kutambua wito huo wa Grace, Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupambana na ugaidi, Vladmir Voronkov alihutubia washiriki akisisitiza kwamba azma ya Umoja wa Mataifa ya kuendelea kuzuia vitendo vya kigaidi iko imara zaidi.
Amesema kusikiliza uzoefu wa manusura ni jambo thabiti linalokumbusha kuwa ugaidi hauna nafasi duniani.
Tazama mahojiano na Ahmed Hadji manusura wa shambulio la kigaidi Uganda mwaka 2010. Alizungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa mwaka 2018.
Katibu Mkuu Guterres pia amesifu subira za waathirika wa ugaidi kwa kueleza licha ya kupitia mateso na maafa lakini dunia imeshuhudia mifano yao ya ustahimilivu na nguvu ya ubinadamu wetu wa pamoja.
Kusoma zaidi kuhusu siku hii tembelea wavuti rasmi wa siku hii hapa