Chonde chonde sitisheni uhasama kuruhusu chanjo ya polio Gaza: Guterres
Chonde chonde sitisheni uhasama kuruhusu chanjo ya polio Gaza: Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres leo ametoa wito kwa pande zinazozozana huko Gaza kuweka chini silaha zao ili wahudumu wa kibinadamu waweze kuwachanja kwa usalama dhidi ya ugonjwa wa polio watoto zaidi ya nusu milioni.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Guterres amesema "Ninatoa wito kwa pande zote kutoa hakikisho thabiti mara moja linalohakikisha usitishaji wa mapigano kwa minajili ya kibinadamu ili kampeni ya chanjo iweze kufanyika”.
Ameongeza kuwa "Hebu tuseme wazi mafanikio ya chanjo hiyo ya polio yanategemea amani na usitishaji mapigano wa kibinadamu. Lakini kwa vyovyote vile, usitishwaji mapigano kwa ajili ya chanjo ya Polio ni lazima.”
Polio haina cha kusubiri
Bwana Guterres almeeleza kuwa Gazaiko katika "maangamizi ya kibinadamu kwa sababu wakati unafikiri hali haiwezi kuwa mbayaza zaidi kwa Wapalestina huko Gaza, mateso zaidi yanaongezeka na ulimwengu unakodoa."
Virusi vya polio viligunduliwa hivi karibuni Gaza katika sampuli za maji taka katika maeneo mawili, Khan Younis na Deir Al-Balah, ikimaanisha kuwa ugonjwa huo ambao unaweza kusababisha kupooza unazunguka kichinichini na kuweka maelfu ya watoto hatarini.
"Polio haijali kugawanya mistari na polio haisubiri," amesisitiza Katibu Mkuu.
Chanjo ziko tayari
Kuanzia mwishoni mwa mwezi huu, Umoja wa Mataifa unatazamiwa kuzindua kampeni ya awamu mbili ya kuwachanja zaidi ya watoto 640,000 huko Gaza walio chini ya umri wa miaka 10.
Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO tayari limeidhinisha kutolewa kwa dozi milioni 1.6 za chanjo ya polio na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF linaratibu juhudi za ufikishaji wa chanjo hizo na vifaa vya baridi vinavyohitajika kuhifadhi chanjo hizo.
Wakati huo huo, timu za wahudumu wa afya kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Palestina, UNRWA ambalo ndio mtoa huduma mkubwa zaidi wa afya ya msingi huko Gaza wako tayari kusimamia chanjo na kusaidia kwa vifaa.
Changamoto kwenye kampeni
Bwana Guterres ameelezea changamoto kubwa zinazokabili juhudi hizi akisema mifumo ya afya, maji na usafi wa mazingira ya Gaza "imeharibiwa, hospitali nyingi na vituo vya huduma za msingi havifanyi kazi, na watu wanalazimika kukimbia kutafuta usalama.”
Zaidi ya hayo, amesema chanjo za kawaida zimetatizika sana kutokana na mzozo huo, hivyo kuongeza kusambaa kwa magonjwa ya surua, homa ya ini na magonjwa mengine yanayoweza kuzuilika.
Amesema "Tunajua jinsi kampeni ya ufanisi ya chanjo ya polio inavyopaswa kusimamiwa. Kwa kuzingatia uharibifu wa jumla huko Gaza, angalau asilimia 95 ya chanjo itahitajika wakati wa kila duru ya kampeni ya duru mbili ili kuzuia kusambaa kwa polio na kupunguza kuibuka kwake."