Kuna hatari kubwa kwa virusi vya polio kusambaa Gaza: UN
Kuna hatari kubwa kwa virusi vya polio kusambaa Gaza: UN
Hatari ya kusambaa kwa polio huko Gaza bado ni kubwa endapo hakutokuwa na hatua Madhubuti na za kina dhidi ya tishio hilo kubwa la kiafya, wameonya leo wataalam wa kibinadamu wa Umoja wa Mataiifa.
Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO na lile la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF katika taarifa yao ya pamoja iliyotolewa mjini Geneva Uswis wamesema "Angalau awamu mbili za chanjo ya polio ya matone itakuwa muhimu ili kuzima kusambaa kwa maambukizi".
Taarifa yao inakuja baada ya virusi vya polio aina ya 2 vinavyotokana na kutopata chanjo kutambuliwa tarehe 16 Julai na Mtandao wa Maabara ya Kimataifa ya Polio GPLN katika sampuli za maji taka zilizokusanywa tarehe 23 Juni kutoka kwenye miji ya Khan Younis na Deir al Balah.
Utafiti kuhusu kupooza
Kesi tatu za kupooza ziliripotiwa mwishoni mwa Julai na mamlaka ya afya ya Gaza na sampuli zilitumwa Jordan kwa uchunguzi.
Kupooza kwa papo hapo kunaweza kusababishwa na sababu nyingi ikiwa ni pamoja na virusi vya polio, kulingana na WHO, ambayo imesisitiza kwamba matokeo bado hayajachapishwa kwa watu walioathiriwa kutoka kaskazini mwa Gaza, Deir al Balah na Khan Younis.
Shirika la afya la Umoja wa Mataifa limebainisha hapo awali kwamba ingawa Gaza ilikuwa na chanjo bora zaidi dhidi ya polio kabla ya vita, miezi ya mapigano imeunda "mazingira magumu ya kuwa na chanjo dhaifu ya virusi vya polio na kuweza kubadilika na hivyo kuwa hali yenye nguvu zaidi ya kusababisha kupooza miongoni mwa wale ambao hawajakamilisha chanjo.”
WHO na UNICEF pia wameelezea wasiwasi wao kuhusu ucheleweshaji wa utoaji wa chanjo ya hiyo ya polio na vifaa muhimu vya mnyororo baridi huku kukiwa na mapigano makali na ukosefu wa usalama katika eneo hilo na ambavyo mvutano wa kikanda unaohusishwa na vita huko Gaza unavyotishia ghasia zaidi.
Ombi kwa wahudumu wa misaada
Usitishaji wa mapigano kwa minajili ya kutoa misaada ya kibinadamu unahitajika ili kuwachanja watoto na kupunguza hatari ya maambukizi", yamesisitiza mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa, baada ya Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus kuidhinisha kutolewa kwa dozi milioni 1.23 za chanjo ya polio ya matone aina ya 2 (nOPV2) kwa ajili ya kutumika huko Gaza kwa nia ya kuchanja zaidi ya watoto 640,500 walio chini ya umri wa miaka 10.
Ili kampeni kubwa ya chanjo ifanye kazi, "upatikanaji salama na endelevu wa wahudumu wa afya unahitajika", yamesisitiza mashirika hayo, huku yakibainisha kuwa ni hospitali 16 tu kati ya 36 ndizo "zinazofanya kazi kwa kiasi huko Gaza.”
Ni vituo 48 tu kati ya 107 vya huduma ya afya ya msingi vilivyosalia vikifanya kazi.
Taarifa yao imesema "Athari katika mfumo wa afya, ukosefu wa usalama, kutoweza kufikiwa kwa watu wengi, watu kufurushwa na uhaba wa vifaa vya matibabu vimechangia kupunguza viwango vya chanjo, pamoja na ubora duni wa maji na uharibifu wa usafi wa mazingira, kuna hatari kubwa ya magonjwa yanayoweza kuzuilika, ikiwemo polio na milipuko mingine."
Huko Gaza, chanjo ya kawaida ya polio ilishuka kutoka asilimia 99 mwaka 2022 hadi chini ya asilimia 90 katika robo ya kwanza ya 2024, kulingana na WHO na UNICEF.