Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nimeshtushwa na kushangazwa na kauli ya waziri wa Israel kuhusu watu wanaokufa njaa Gaza: Türk

Volker Türk akizungumza katika Mkutano wa Vijana wa Watetezi wa Haki za Binadamu wa Vienna 2023 katika Kituo cha Kimataifa cha Vienna.
UNIS Vienna Volker Türk Kamishina Mkuuwa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa

Nimeshtushwa na kushangazwa na kauli ya waziri wa Israel kuhusu watu wanaokufa njaa Gaza: Türk

Haki za binadamu

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR, leo imetoa wito kwa mamlaka ya Israel kufuatilia maafisa wakuu ambao kauli zao hadharani kuhusu mzozo wa Gaza zinaweza kuendeleza uhalifu wa kivita.

Msemaji wa ofisi hiyo OHCHR Jeremy Laurence amesema “Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu Volker Türk ameshangazwa na kushtushwa na maoni yaliyotolewa na waziri wa fedha wa Israel Bezalel Smotrich, ambaye amependekeza kuwa kuacha Wapalestina milioni mbili huko Gaza kufa kwa njaa kunaweza kuhesabiwa kuwa ni maadili na haki ili kuwaachilia huru mateka”.
Kamishna Mkuu amelaani vikali kauli hiyo kuwa ni maneno makali, ambayo pia yanachochea chuki dhidi ya raia wasio na hatia.
Mwanamke Mpalestina akifua nguo huku watoto wawili wadogo wakicheza katikati ya vifusi vya jengo lililoharibiwa huko Gaza.
© UNRWA Maji na chakula bado ni changamoto kubwa kupatikana katika Ukanda wa Gaza.

Hatari ya uchochezi

Bwana Laurence ameeleza kuwa kutumia njaa kwa raia kama njia ya vita na adhabu ya pamoja ya wakazi wa Palestina ni uhalifu wa kivita.
"Kauli hiyo ya moja kwa moja na ya hadharani inaweza kuchochea uhalifu mwingine wa kikatili," amesema akiongeza kuwa “Kauli hizo, hasa za viongozi wa umma, lazima zikome mara moja. Ni lazima wachunguzwe na ikibainika kuwa ni uhalifu, lazima washtakiwe na kuadhibiwa.”
Bwana Laurence pia amesisitiza ombi la muda mrefu la OHCHR la kusitisha mapigano mara moja huko Gaza, kuachiliwa kwa mateka wote na kuongezeka kwa misaada ya kibinadamu kupitia ndani ya eneo hilo.
"Huu ni wito wa haraka kwa mamlaka ya Israel kwamba ni wajibu wao kufuatilia tabia hii. Zaidi ya hayo, tupige hatua moja baada ya nyingine. Hiyo ni hatua ya kwanza. Ni jukumu la Waisraeli."
Wanaume wa Kipalestina wakiwa wamepanda farasi katika mitaa iliyojaa vifusi huko Khan Younis, Gaza, huku familia zilizopoteza makazi zikitembea nyuma.
© UNRWA Amri mpya ya watu kuahama Khan Younis yazilazimisha familia wakiwemo watoto kukimbia

Wanaofurusha kutoka Khan Younis

Wakati huo huo, athari za amri ya hivi karibuni yawatu kkuhama huko Gaza tayari zinaonekana sana, afisa mkuu wa mawasiliano wa shirika la Umoja wa Mataifa linalosaidia wakimbizi wa Palestina, UNRWA, amesema.
Louise Waterridge amezungumza na UN News siku moja baada ya jeshi la Israel kutoa agizo hilo, na kuwalazimu maelfu ya watu kukimbia mashariki na kati mwa Khan Younis na eneo la Al Salqa la Deir Al-Balah.
Bi Waterridge alikuwa Khan Younis Alhamisi alasiri na alishuhudia mamia ya familia zikielekea magharibi katika hali mbaya iliyozidi nyuzi joto 30.
"Matukio yalikuwa ya kutisha," amesema. "Ni kama kufurushwa kwa watu hawa kwa mara nyingine tena. Wanabeba chochote wanachoweza. Hawaonekani kuwa na vitu vingi vilivyobaki. Tuliona magari machache yenye familia na watu wengi walikuwa wakitembea kwa miguu."
Watoto wachanga kabla ya wakati wakiwa kwenye kiangulio katika Hospitali ya Al-Helal Al-Emarati huko Rafah, Gaza, wakipokea huduma ya matibabu kutoka kwa wafanyakazi.
© UNICEF/Eyad El Baba watoto katika hospital ya al Shifa wakiandaliwa kuhamishwa

Kampeni ya chanjo ya polio

Bi Waterridge pia amezungumzia mipango ya kuwachanja zaidi ya watoto nusu milioni huko Gaza dhidi ya polio kufuatia kugunduliwa kwa ugonjwa huo katika sampuli za maji taka mwezi uliopita.
UNRWA, pamoja na shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia watoto UNICEF, na Wizara ya Afya ya Gaza wanatazamiwa kuzindua awamu mbili za hatua ya chanjo katika siku zijazo.
"Kampeni hii, bila shaka, ingekuwa rahisi zaidi na haraka zaidi kuwezeshwa endapo kungekuwepo na usitishaji mapigano," amesema.
Ameongeza kuwa “Tumekuwa tukitoa wito wa kusitishwa kwa mapigano kwa miezi kadhaa. Itanufaisha sana aina yoyote ya hatua za kibinadamu katika Ukanda wa Gaza, ikiwa ni pamoja na kampeni ya chanjo dhidi ya polio.
Amesisitiza dhamira ya kina ya UNRWA ya kuongoza kampeni za chanjo mashinani, akionyesha jukumu lao kama shirika kubwa zaidi katika Ukanda wa Gaza.