WEIF2024 imenikutanisha na wawekezaji – Muasisi FYWEDO
WEIF2024 imenikutanisha na wawekezaji – Muasisi FYWEDO
Kutana na Ngwi Favor Njikta.Anajitambulisha akisema ni Muasisi na Rais wa FYWEDO ambalo ni shirika la kiraia la kusaidia mashirika ya kibiashara yanayoendeleza wajawasiriamali wanawake nchini Cameroon na barani Afrika kwa ujumla.
Nilikutana naye ndani ya ukumbi wa maonesho yaliyopatiwa jina Familia Fanisi, yakileta wajasiriamali wabunifu wanaotumia vipaji vyao kujikwamua sio tu kiuchumi bali kuinua familia zao.
Nikamuuliza kulikoni yuko Manama, Bahrain kwenye jukwaa la kimataifa la uwekezaji kwa wajasiriamali, na hakusita kujibu akisema, “Niko hapa kwenye jukwaa la kimataifa la uwekezaji kwa wajasiriamali lililoandaliwa na UNIDO kuonesha kile tunachofanya na wanawake wajasiriamali nyumbani.”
Shirika lao linatoa mafunzo ya ujasiriamali kuanzia kwenye biashara za mtandaoni, nishati salama, usindikaji wa vyakula hadi ubunifu wa mavazi, na utengenezaji wa vitambaa bila kusahau vipodozi.
Tumeanzisha zaidi ya mashirika 50 madogo na ya kati yanayoendeshwa na wanawake na pia tuna wajasiriamali zaidi 1500 wa mtandaoni.
Changamoto ni ukosefu wa stadi za kidijitali
Akanieleza anachokiona kama kikwazo akisema ni matumizi ya vifaa vya kidijitali ili kuendeleza stadi zao na pia kufikia masoko. Changamoto hii imewakwamisha kwenye kuunda wavuti mtandaoni ili kufikisha bidhaa na huduma zao kwenye masoko barani Afrika. Kwa kuja hapa nimekutana na watu wengi wabobezi wa dijitali ili wapate mbinu na wajiongeze zaidi.”
Kuhusu manufaa ya WEIF2024, Favor anasema amekutana na baadhi ya wawekezaji ambao wanavutiwa na miradi mbali mbali wanaayoendesha na wanawake kwenye eneo lao.
Kwa hiyo kutoka hapa tunaelekea kwenye hatua nyingine ya maandalizi ya mipango ya biashara na mengineyo. Na kwa mikutano tuliyohudhuria, watoa mada wameweza kutuelimisha juu ya será mbali mbali zinazosimamia nchi za Ghuba na fursa nyingine zilizo wazi kwa wajasiriamali kwenye ukanda wetu.”
FYWEDO ilianzishwa mwaka 2017 na inashirikiana pia na shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake, UN Women nchini Cameroon. Na tayari Muasisi wake anaona imekuwa na mabadiliko chanya kwa wanawake na wasichana.
Wanawake wengi wafanyabiashara wanapoungana na shirika letu wanakuwa kwanza hawana uelewa kabisa wa jinsi ya kulinda na kuendeleza mazingira na kupata faida kutokana na kile wanachofanya. Tumewafundisha jinsi ya kuwa makini na shughuli zao na pia jinsi ya kuboresha na kutangaza bidhaa zao ili zifikie kiwango cha kimataifa. Tumewapatia pia mafunzo ya kuboresha mipango ya ya biashara.
Mfano wa matunda chanya ya FYWEDO
Ametolea mfano msichana Grace anayemtaja kuwa mmoja wa simulizi za mafanikio FYWEDO ambaye alihitimu TEHAMA Chuo Kikuu akiwa amebuni programu ya usalama wa mitandao.
Tulimsaidia kuendeleza hii programu ya kompyuta ya biashara. Tayari amepata wateja wa awali na sasa afanya kazi za masuala ya usalama wa kimtandao nchini Cameroon.”
Na kumalizika kwa jukwaa kunamaanisha anarejea nyumbani Cameroon kwa wanawake na wajasiriamali anaowaongoza na anachoondoka nacho ni umuhimu wa stadi za kidijitali.
Kuelimisha wajasiriamali Cameroon ili wawe na miradi bunifu, inayoongozwa na teknolojia. Kwa sababu unaona siku zijazo zitatawaliwa na Akili Mnemba. Sasa hili ni jambo muhimu naondoka nalo hapa.
Mfano mjasiriamali atatumia vipi teknolojia kwenye elimu na uendelezaji wa vipodozi. Tunataka kuwahamasisha juu ya umuhimu wa teknolojia kwenye lile wafanyalo. Teknolojia itapunguza muda wa uzalishaji, na kuwapatia ufanisi. Hii ni moja ya ujumbe ambao naenda nao nyumbani na ni muhimu sana kwani lilikuwa ni pengo kubwa sana.”
Kuhusu WEIF2024
Jukwaa la Nne la kimataifa la kuwekeza kwa wajasiriamali, WEIF2024 lilifanyika mwezi Mei mwaka huu wa 2024 kuanzia tarehe 14 hadi 16 huko Manama, Bahrain likiandaliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la MAendeleo ya Viwanda, UNIDO ofisi ya Uendelezaji wa Biashara, ITPO nchini humo.
Lilimulika ni kwa vipi ubunifu na teknolojia vinaweza kutumika kusongesha Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs.