WHO na UNRWA yasisitiza umuhimu wa sitisho la mapigano Gaza
WHO na UNRWA yasisitiza umuhimu wa sitisho la mapigano Gaza
Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO, leo limeangazia mfululizo wa hali za dharura zinazoendelea kuongezeka katika kanda ya Mashariki ya Kati, likisisitiza hitaji la haraka la kurejea kwa amani na juhudi za kibinadamu zilizoratibiwa.
Mkurugenzi wa WHO kanda ya Mediteranea ya Mashariki Dkt. Hanan Balkhy akizungumza kwa njia ya video kutoka Cairo, Misri, amesema kuwa "katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, kanda hii imekumbwa na mfululizo wa migogoro mikubwa. Ameitaja mlipuko wa virusi vya polio uligunduliwa Gaza."
Kuhusu eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu, Balkhy amebainisha kuwa mwishoni mwa mwezi Julai, WHO ilisaidia uhamishaji wa wagonjwa zaidi ya 100 wenye hali mbaya za kiafya kutoka Gaza kwenda Ubelgiji, Uhispania, na Umoja wa Falme za Kiarabu UAE.
Ameitaja operesheni hiyo ilikuwa “ngumu sana kutokana na kufungwa kwa kivuko cha Rafah tangu Mei, ikihitaji safari ngumu zaidi kupitia kivuko cha Karem Shalom na uwanja wa ndege wa Israeli."
Balkhy ameonya kuwa licha ya juhudi hizi, zaidi ya watu 10,000 walio Gaza bado wanahitaji kuhamishwa kwa ajili ya matibabu na kwamba kugunduliwa kwa aina mpya ya virusi vya polio aina ya 2 katika sampuli za mazingira za Gaza kumeibua wasiwasi mkubwa.
Ameongeza kuwa “WHO inasisitiza hitaji la kusitisha mapigano kwa muda ili kuhakikisha mafanikio ya kampeni za sasa za chanjo dhidi ya polio.”
Kupitia taarifa hiyo, WHO pia imeeleza wasiwasi mkubwa kuhusu kuongezeka kwa vurugu na mashambulizi ya kijeshi katika kanda, ambayo yanaongeza hatari ya mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu.
Balkhy ameendelea kueleza kwamba “WHO inajiandaa kwa uwezekano wa kuongezeka kwa migogoro kwa kupeleka wataalamu wa dharura na vifaa, hasa nchini Lebanon, na kusaidia mifumo ya afya nchini Syria, Iran, Jordan, na nchi nyinginezo kwa mipango ya dharura.”
Njaa Sudan
Akizungumza kuhusu Sudan, Balkhy ameeleza kuwa nchi hiyo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, ambapo Kamati ya tathmini ya njaa IPC, imetangaza baa la njaa katika sehemu za Darfur Kaskazini, hasa kambi ya Zamzam.
Zaidi ya hayo, amesema vurugu zinazoendelea zimefurusha mamilioni ya watu, na kufanya juhudi za kibinadamu kuwa ngumu zaidi. Ametoa wito wa kufunguliwa haraka kwa njia za kuvuka mipaka, kama vile kivuko cha Adre kati ya Chad na Sudan, ili kupeleka msaada muhimu.
Balkhy pia ameitaja ripoti ya Haki za Binadamu inayoeleza ukatili mkubwa wa kijinsia nchini Sudan akisema kuwa imewashutumu maafisa wa WHO, ambao sasa wanazingatia kusaidia waathirika kwa huduma za matibabu na usaidizi wa kisaikolojia.
Kuhusu Athari za Mabadiliko ya Tabianchi, taarifa hiyo imeyataja matukio makubwa ya mabadiliko ya tabianchi, ikiwa ni pamoja na mafuriko na mawimbi ya joto, kama changamoto kwa maisha ambayo inachochea masuala ya athari za afya, kuanzia kuenea kwa magonjwa hadi mgogoro wa uzalishaji wa chakula.
WHO imetoa wito wa kujenga upya na kuimarisha mifumo ya afya katika kanda, ambayo tayari inaelemewa na rasilimali chache na uharibifu wa miundombinu.
Shirika hilo pia limezitaka pande zote kuheshimu msingi wa huduma za afya, kutoa fursa za ufikiaji wa kibinadamu bila vikwazo, na kuunga mkono ufadhili endelevu kwa juhudi za misaada ya kibinadamu.