Kana kwamba vita haitoshi, maji safi na salama ni mtihani mwingine Gaza: UNICEF
Kana kwamba vita haitoshi, maji safi na salama ni mtihani mwingine Gaza: UNICEF
Kumekuwa na upungufu mkubwa wa uzalishaji wa maji safi katika Ukanda wa Gaza na hivyo kuathiri upatikanaji wa huduma ya usambazaji wa maji kwa karibu watu 500,000 kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF ambalo lipo bega kwa bega na waathirika kuhakikisha wanasaidiwa .
Hali ni tete katika kambi ya Al Korban huko Deir al- Balah, watu wamekusanyika karibu na lori la maji la UNICEF ili kupata maji safi ya kunywa. Wakimbizi wa ndani katika kambi hii hutumia majerekeni na vyombo vingine kujaza maji na kuyarudisha kwenye mahema yao. Hizi ni juhudi ambazo zinafanywa na UNICEF kutokana na uhaba wa maji safi uliosababisha hali mbaya zaidi kwa wakazi wa Gaza. Nehal Al-Fayoumy ni miongoni mwa waathirika anasema “Unaweza kuona vipele kwenye ngozi ya mtoto wangu? Wanatoka kuishi kambini. Tuna minyoo na mende wakubwa ndani ya hema kwa sababu ya ukosefu wa maji safi, na taka zilizokusanywa karibu nasi. Tunaishi katika hali mbaya sana hapa.”
Mamlaka ya maji ya manispaa ya Pwani na Mamlaka ya maji ya Palestina zimeripoti uzalishaji wa maji salama wa takribani lita 89,000 kwa siku kwa ajili ya kunywa na matumizi ya nyumbani kote katika Ukanda wa Gaza.
Msemaji wa UNICEF katikaeneo hili ni Salim Oweis “Sasa niko mbele ya mtambo wa UNICEF wa kuondoa chumvi kwenye maji. Mtambo huuhutoa maji safi, kwa watu hawa wote na zaidi. Mtanbo huu kabla ya vita umekuwa ukizalisha zaidi ya lita 20,000 za maji safi. Izlipunguzwa hadi 2000 na hadi 500 tu baada ya vita. Ni jambo zuri kwamba bado unafanya kazi, lakini inafanya kazi kwa sehemu ya uwezo wake. Kama unavyoona, watu wanapanga foleni kutafuta maji yao.”
UNICEF inatoa wito kwa pande zote kwenye mzozo kuzingatia wajibu wao chini ya sheria za kimataifa ya kibinadamu. Hiyo ni pamoja na kuchukua tahadhari kubwa kuwaokoa raia na miundombinu ya kiraia, kukidhi mahitaji muhimu ya raia na kuwezesha ufikiaji wa haraka, salama na usiozuiliwa wa msaada wa kibinadamu.