MUHTASARI WA HABARI: Bangladesh, Maandamano Uingereza na kumbukumbu ya Hiroshima
MUHTASARI WA HABARI: Bangladesh, Maandamano Uingereza na kumbukumbu ya Hiroshima
Katika muhtasari wa habari: hali bado ni tete nchini Bangladesh , huko Uingereza maandamano yanaendelea kusambaa na leo ni miaka 79 ya kumbukumbu ya shambulio la bomu la atomiki huko Hiroshima Japan lililofanywa na Marekani
Baada ya Waziri Mkuu wa Bangladesh Sheikh Hasina kukimbia nchi kufuatia maandamano makubwa kutoka kwa wanafunzi, na kisha jeshi kutangaza kuwa serikali ya mpito itaundwa na Bunge kuvunjwa Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini humo Ms. Gwyn Lewis amezungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa na kusema naweza kusema hali imekuwa tulivu asubuhi leo na tunajaribu kusoma hali ilivyo. Jeshi linahakikisha usalama nchi nzima ikiwemo rai ana wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa. Lakini hali si ya uhakika hadi serikali ya mpito itakapoundwa. Najua mazungumzo yanaendelea na vyama vya siasa na wanafunzi wenyewe.
Na sasa nchini Uingereza ambako maandamano yaliyochochewa na taarifa potofu na za uongo yanazidi kusambaa ambapo Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, Filippo Grandi amesema ghasia hizo ikiwemo dhidi ya wasaka hifadhi zinashtusha na vivyo hivyo kwa habari za uongo zinazozichochea. Amesema kila mtu bila utofauti wowote ana haki ya kujihisi salama kwenye jamii zao na kuishi huru bila ya chuki, hofu na ukosefu wa stahmala.
Na leo ikiwa ni miaka 79 tangu MArekani iangushe bomu la nyuklia huko Hiroshima nchini Japani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ni ajabu kuwa silaha hizo na tishio lake la kuzitumia bado havijaondolewa kwenye matumizi. Amesema ni tishio halisi na ni hatari hivyo dunia isisahau ilichojifunza baada ya Agosti 6, mwaka 1945.