Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO yataka kuongezwa msaada wa kuokoa maisha Sudan na kuchagiza uzalishaji wa ndani wa chakula

Mkulima akiwa amesimama mbele ya nyumba yake Al-Fashaga, Sudan.
© FAO/Mahmoud Shamrouk
Mkulima akiwa amesimama mbele ya nyumba yake Al-Fashaga, Sudan.

FAO yataka kuongezwa msaada wa kuokoa maisha Sudan na kuchagiza uzalishaji wa ndani wa chakula

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO limetoa wito wa kusitishwa uhasama mara moja nchini Sudan, kuongezwa msaada wa dharura wa  chakula cha kuokoa maisha, lishe na fedha taslimu pamoja na msaada wa dharura wa kilimo.

Wito huo umechochewa na matokeo mapya yanayothibitisha hali ya njaa katika sehemu za Darfur Kaskazini nchini humo .

Kupitia taarifa ya shirika hilo kwa  vyombo vya habari iliyotolewa mjini  Roma, Italia,Mkurugenzi Mkuu wa FAO QU Dongyu amebainisha kuwa maeneo yaliyoathiriwa na migogoro yanahitaji msaada huu zaidi ili kushughulikia mahitaji ya dharura na kuzuia hatari ya baa la njaa kuongezeka na kuathiri maeneo mengine nchini Sudan.

Kamati ya tathimini ya hali ya njaa ya IPC imebaini kwa uhakika kuwa hali ya baa la njaa inaendeleakatika kambi ya Wakimbizi wa ndani (IDP) ya Zamzam ambayo inahifadhi watu 500,000 nje ya mji wa El Fasher huko Darfur.

Sudan imekumbwa na mgogoro wa kutokuwa na uhakika wa chakula na viwango vya juu zaidi vya njaa kuwahi kurekodiwa na IPC nchini  humo, pamoja na mgogoro mkubwa zaidi wa wakimbizi wa ndani.

Watoto wapumzika kwa kivulini katika kituo cha Tambasi huko El Fasher, Darfur Kaskazini.
© UNICEF/Mohamed Zakaria
Watoto wapumzika kwa kivulini katika kituo cha Tambasi huko El Fasher, Darfur Kaskazini.

Darfur hali ni mbaya

Akielezea athari za mgogoro unaoendelea Mkurugenzi Mkuu wa FAO QU Dongyu  amesema, “tunashuhudia hali mbaya ya njaa katika sehemu za Darfur Kaskazini na hatari inayoongezeka ya njaa katika makazi mengine na maeneo yaliyoathiriwa na migogoro, hasa Darfur, Kordofan Kusini, Khartoum na Al Jazirah. Tumekuwa tukionya kuhusu janga hili linalokaribia, lakini kutokana na mgogoro unaoendelea na upatikanaji mdogo wa misaada ya kibinadamu jamii hizi bado hazipati msaada wa haraka wanaohitaji. Tunahitaji hatua za haraka na za pamoja kuzuia janga kubwa zaidi la kibinadamu kutokea. Njaa inaweza kusitishwa, lakini kusitisha uhasama mara moja ni hatua muhimu ya kwanza. Amani ni sharti la uhkika wa chakula, na haki ya chakula ni haki ya msingi ya binadamu."

Taarifa hii pia imebainisha kuwa Sudan inategemea zaidi kilimo lakini kwa sasa maisha ya vijijini, mifumo ya chakula na kilimo viko kwenye  mstari wa mbele wa mgogoro, vikikumbwa na uharibifu mkubwa na usumbufu wenye athari na matokeo mabaya kwa uhakika wa chakula na lishe.

Shirila la FAO pia  limeonya kuwa kuna uwezekano kwamba hali ya njaa itazidi kuzorota kufuatia   mvua za juu ya wastani na joto la juu zaidi ya wastani zinazotarajiwa katika majimbo ya kusini na katikati ya Sudan kutokana na hali ya La Niña inayotarajiwa kuanzia Agosti hadi Septemba.

Kwa mujibu wa taarifa hii, FAO na washirika wake wanaongoza juhudi mbalimbali kuzuia kuongezeka kwa hali ya njaa kote nchini Sudan. Hata hivyo, hili pekee haliwezi kuziba mapengo yaliyosababishwa na kupungua kwa uzalishaji wa ndani wa chakula.

Ili kushughulikia hili, FAO inasambaza mbegu kwa kaya za wakulima milioni 1.2 kwa msimu mkuu wa upanzi, ambao ulianza Juni. Aidha, FAO inatoa huduma muhimu za mifugo na inapanga kutoa vifaa vya dharura vya mifugo na uvuvi, ambavyo ni muhimu kwa kuhifadhi chanzo kikuu cha lishe na mapato kwa mamilioni ya watu.

Msaada wa chakula ukitolewa kwa jamii za Darfur Magharibi.
© WFP
Msaada wa chakula ukitolewa kwa jamii za Darfur Magharibi.

Hatuwezi kusubiri Matangazo ya njaa

QU Dongyu ametoa wito wa hatua za haraka na za kiwango kikubwa kusaidia jamii zinazokabiliwa na ukosefu wa chakula nchini Sudan. Amesisitiza kuwa mahitaji ya haraka lazima yatimizwe na maisha yao kuimarishwa ili kujenga mnepo wa kuhimili migogoro, mabadiliko ya tabianchi na mishtuko ya kiuchumi na kujiandaa kwa chochote kitakachokuja.

FAO imeonya kuwa jumuiya ya kimataifa haiwezi kusubiri matangazo ya njaa, badala yake lazima ichukue hatua kwa kiwango cha juu  na kwa haraka ikitumia maonyo kama kichocheo cha hatua hizo.