Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yalaani vikali shambulio la kigaidi Somalia lililokatili maisha ya watu 37

Kutoka Maktaba: Picha ya ufukwe wa Lido Somalia ambako familia na marafiki hukutanika kwa burudani mjini Moghadishu
UNSOM Photo Kutoka Maktaba: Picha ya ufukwe wa Lido Somalia ambako familia na marafiki hukutanika kwa burudani mjini Moghadishu

UN yalaani vikali shambulio la kigaidi Somalia lililokatili maisha ya watu 37

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa nchini Somalia umelaani vikali shambulio la kigaidi lililotokea leo kwenye hotel moja katika ufukwe kwa bahari wa Lido mjini Moghadishu nchini Somalia na kukatili maisha ya watu 37 na kujerihi wengine zaidi ya 200.

 

Takriban watu 37 wameuawa na zaidi ya 200 kujeruhiwa, baadhi yao vibaya, katika shambulio la kigaidi Lido Moghadishu Somalia kulingana na ripoti za duru za habari.

"Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema anasikitika kwamba watu wa Somalia wanaendelea kuwa wahanga wa vitendo hivyo vya kigaidi," amesema Farhan Haq, Naibu Msemaji wa Mkuu wa Umoja wa Mataifa kupitia taarifa yake iliyotolewa leo Jumamosi.

Bwana. Haq ameongeza kuwa Katibu Mkuu "Anasisitiza kwamba Umoja wa Mataifa unasimama kidete na Serikali na watu wa Somalia dhidi ya ugaidi na itikadi kali za kikatili,".

Shambulio hilo la Ijumaa usiku lilikuwa moja ya mauaji makubwa zaidi kuwahi kutokea nchini Somalia tangu mashambulio ya Oktoba 2022 huko Mogadishu na kuua zaidi ya watu 120 na kujeruhi zaidi ya 300.

Mabaki ya gari baada ya shambulio la kigaidi Moghadishu- Kutoka Maktaba
UN Photo/Stuart Price Mabaki ya gari baada ya shambulio la kigaidi Moghadishu- Kutoka Maktaba

UN tuko sanjari na watu wa Somalia

Katika taarifa yake iliyotolew mjini Moghadishu Kaimu mwakilishi wa Katibu Mkuu nchini Somalia James Swan amesema Umoja wa Mataifa nchini Somalia unatoa pole kwa familia za wahanga wa shambulio hilo na kuwatakia ahueni ya haraka waliojeruhiwa.

"Ufukwe wa Lido ni mahali maarufu kwa Wasomali kutumia wakati na familia na marafiki na kufurahia uzuri wa ufuo wa Somalia. Kulenga eneo hili ni kitendo cha kuchukiza ambacho kinahitaji hukumu kali zaidi,"

Ameongeza kuwa "Tunapoungana na Wasomali wote wapenda amani katika kuomboleza msiba huu wa kusikitisha, ninathibitisha uungaji mkono wa Umoja wa Mataifa na mshikamano na serikali ya Shirikisho la Somalia katika juhudi zake za kuhakikisha amani, usalama na utulivu nchini humu."

Kwa mujibu wa duru za habari, kundi la kigaidi la Al-Shabaab limedai kuhusika na shambulizi hilo ambalo lilikuwa ni shambulio la bomu la kujitoa mhanga na ufyatulianaji risasi kati ya magaidi hao na vikosi vya usalama vya Somalia na mbali ya kuua watu 37 limejeruhi wengine zaidi ya 200.