UN inaendelea na juhudi za kidiplomasia za kupunguza mvutano Mashariki ya Kati
UN inaendelea na juhudi za kidiplomasia za kupunguza mvutano Mashariki ya Kati
Umoja wa Mataifa leo umetangaza nia yake ya kuendelea na juhudi zake za kidiplomasia kwa ajili ya kupunguza mvutano Mashariki ya Kati, baada ya majadiliano na Lebanon, Misri na Qatar.
Eneo hilo likikabiliwa na hatari kubwa inayoongezeka ya mvutano ambao unaleta tishio kwa uthabiti wa Mashariki ya Kati, Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa wa Mchakato wa Amani ya Mashariki ya Kati amekumbusha udharura wa kuchukua hatua na maamuzi na kwa Pamoja ili kukabiliana na vitisho vya haraka na kuweka misingi ya amani ya kudumu.
Mratibu huo Tor Wennesland amesema amejihusisha na majadiliano muhimu katika siku za hivi karibuni na pande zinazohusika na nchi wanachama katika kanda, ikiwa ni pamoja na Lebanon, Misri na Qatar, kwa ajili ya kupunguzwa kwa mvutano wa kanda.
Hatua za haraka ili kuzuia kuzorota zaidi kwa hali
Mikutano hiyo inakuja baada ya kifo cha afisa mkuu wa Hezbollah Fuad Shukr katika shambulio kwenye mji mkuu wa Lebanon Beirut, na mauaji ya kiongozi wa kisiasa wa Hamas Ismail Haniyeh huko Tehran, nchini Iran.
"Tulikagua juhudi zinazoendelea za upatanishi, kupunguza hali hiyo ya mvutano na kutafuta njia za kuzuia mzozo huo kuenea katika maeneo mengine," amesema Tor Wennesland katika taarifa yake.
Amesisitiza haja ya hatua za haraka na zilizoratibiwa ili kuzuia kuzuia kuzorota zaidi kwa hali hiyo.
"Ni muhimu tuchukue hatua kwa uamuzi na kwa pamoja kushughulikia vitisho mara moja na kuweka msingi wa amani ya kudumu."
Mwanadiplomasia huyo wa Umoja wa Mataifa na timu yake wanakusudia kuendeleza juhudi zao na "ushirikiano wa dhati na pande zote zinazohusika ili kuunga mkono amani na utulivu katika eneo hilo.”
Mkuu wa Operesheni za Amani za UN azuru Lebanon
Kwa upande wake, Mkuu wa Operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa Jean-Pierre Lacroix, ambaye anazuru Lebanon, ameitumia leo Ijumaa kukutana na walinda amani wa Umoja wa Mataifa , kabla ya kwenda kwenye vituo vyao mbalimbali kando ya msitari wa bluu au Blue Line.
Jana Alhamisi alikuwa huko Naqoura, kwenye makao makuu ya Kikosi cha Muda cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon UNIFIL.
Huko alikutana na Mkuu wa operesheni ya Umoja wa Mataifa na Kamanda wa Kikosi, Meja Jenerali Aroldo Lázaro.
Pia alizungumza na walinzi wa amani ambao wanafanya kazi katika hali ngumu sana, inayojulikana ikighubikwa na majibizano ya mara kwa mara ya risasi kwenye msitari wa bluu na kuenea zaidi kati ya pande husika.
Mapema leo, amekuwa na mkutano na kamanda wa jeshi la Lebanon kusini mwa Lebanon.
Bwana. Lacroix amesisitiza haja ya vikosi vya wanajeshi vya Lebanon kupanua wigo wa mamlaka yao kote kusini mwa Lebanon, kwa mujibu wa Azimio nambari 1701 la Baraza la Usalama.
Ubomoaji wa makazi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi
Kuhusu hali ndani ya Palestina eneo linalokaliwa kwa mabavu, kumeripotiwa ubomoaji wa nyumba na mali za Wapalestina katika kijiji cha Beit 'Anan, kilichoko kaskazini-magharibi mwa Jerusalem, na katika kijiji cha Al Baqa'a, mashariki mwa Hebron, katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu OCHA pia inaripoti kwamba wakati wa wiki ya Julai 23 hadi 29, mamlaka ya Israel ilibomoa au kulazimisha ubomoaji wa mali 30 zinazomilikiwa na Wapalestina, na kusababisha watu 57 kukimbia makazi yao, pamoja na watoto 25 , ambao walilazimika kuacha nyumba zao.
Tangu Oktoba 7 mwaka jana, mamlaka za Israel zimesimamia au kutekeleza ubomoaji wa zaidi ya majengo 1,300 yanayomilikiwa na Wapalestina katika eneo lote la Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, na kuwafanya takriban watu 3,000 kuyakimbia makazi yao.
Hatari ya hepatitis A
Kwa upande wake, mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA, Philippe Lazzarini, ameonya kwamba wakazi wa Gaza wanakabiliwa na hatari nyingine ambayo ni hepatitis A, ambayo inaenea, ikiwa ni pamoja na kwa watoto.
Tangu kuanza kwa vita, shirika hilo la Umoja wa Mataifa limeripoti karibu kesi 40,000 katika makazi na kliniki zake, ikilinganishwa na visa 85 tu katika kipindi sawa cha kabla ya vita.
"Hili ni ongezeko la kutisha. Mfumo wa usimamizi wa taka huko Gaza umeporomoka. Marundo ya taka hukusanyika wakatihuu wa joto kali la kiangazi. Maji taka yanamiminika mitaani huku watu wakipanga foleni kwa saa nyingi ili tu kwenda chooni. Yote haya kwa pamoja ni kichocheo hatari cha kuenea kwa magonjwa," Lazzarini amesema katika chapisho lake kwenye jukwaa la kijamii la X.
Kwa mujibu wake, upatikanaji wa maji safi na bidhaa za usafi ni kipaumbele kingine huko Gaza akisistizakuwa "Usitishaji mapigano unahitajika sasa ili kurejesha mifumo ya usimamizi wa taka na maji taka, kuleta bidhaa za usafi zinazohitajika na kudhibiti kuenea kwa magonjwa,"