Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fursa za msaada wa unyonyeshaji kuokoa maisha  ya watoto 820,000 kila mwaka: UNICEF/ WHO

Mama akimnyonyesha mwanaye mchanga katika hospitali ya Kusini mwa Madagascar
UN News/Daniel Dickinson
Mama akimnyonyesha mwanaye mchanga katika hospitali ya Kusini mwa Madagascar

Fursa za msaada wa unyonyeshaji kuokoa maisha  ya watoto 820,000 kila mwaka: UNICEF/ WHO

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF, na na shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni WHO, wametoa wito wa  kuboreshwa kwa huduma  za kuwaunga mkono kina mama wanaonyonyesha  kama hatua muhimu ya kuboresha usawa wa afya na kulinda haki za mama na mtoto kuishi na kustawi.

Mashirika haya mawili yamesisitiza hatua hii katika taarifa ya pamoja iliyotolewa New York, Marekani, ambayo inaadhimisha kuanza kwa Wiki ya Unyonyeshaji Duniani, chini ya kauli mbiu "Kuziba Pengo: Msaada wa Ukuchagizaji Maziwa ya Mama kwa Wote."

Taarifa hii ya pamoja imebaini kwamba, katika miaka 12 iliyopita, idadi ya watoto wachanga chini ya umri wa miezi sita duniani wanaonyonyeshwa maziwa ya mama pekee imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 10%. Hii ina maana kwamba asilimia 48 ya watoto wachanga duniani sasa wanapata mwanzo mzuri wa maisha na kuchangia katika kuyaokoa maisha ya maelfu ya watoto.

Banamwana Yvette Mfanyakazi wa Ofisi za Jiji na Kigali.
UNICEF
Banamwana Yvette Mfanyakazi wa Ofisi za Jiji na Kigali.

Mbioni kutimiza lengo

Kwa mujibu wa WHO, ingawa ongezeko hili limekaribia lengo la kuongeza unyonyeshaji kwa angalau asilimia 50 ifikapo mwaka 2025, bado kuna changamoto zinazoendelea ambazo zinapaswa kushughulikiwa.

Hivyo basi, imesema kutoa msaada unaohitajika kwa kina mama ili wanyonyeshe watoto wao kunafaidisha kila mtu.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni za WHO, kuboresha viwango vya unyonyesahji kunaweza kuokoa maisha ya watoto zaidi ya 820,000 kila mwaka.

Mashirika hayo yamesisitiza umuhimu  wa kuwanyonyesha watoto katika kipindi cha ukuaji na maendeleo ya mapema, yakisema kuwa maziwa ya mama hulinda watoto dhidi ya magonjwa na vifo hasa wakati wa dharura, kwani kunyonyesha mtoto  huhakikisha chanzo salama cha lishe na kinachopatikana kwa watoto wachanga na watoto wadogo.

Wakimbizi kinamama wakinyonyesha watoto wao nchini Uganda
Ⓒ WFP/Arete/Siegfried Modola
Wakimbizi kinamama wakinyonyesha watoto wao nchini Uganda

Maziwa ya mama ni kinga kwa watoto

Ripoti hii pia imebaini kuwa kunyonyesha watoto hakupunguzi tu mzigo wa magonjwa ya utotoni, bali pia hatari za aina fulani za saratani na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa mama.

Ripoti hii pia imetoa wito wa kukusanywa kwa takwimu za kuaminika ili kusaidia kushughulikia tofauti za huduma za afya na kuhakikisha kwamba mama na familia wanapata msaada katika  unyonyeshaji kwa wakati unaofaa na wenye ufanisi.

Hii ni kwa sababu, kwa sasa nusu ya nchi tu ndizo zinazokusanya takwimu kuhusu viwango vya unyonyeshaji wa watoto.

Ili kufanikisha maendeleo, ripoti inapendekeza kwamba takwimu zinafaa kuwasilishwa katika  hatua za sera zinazolenga kuboresha unyonyeshaji wa watoto, kama vile sera za ajira zinazojali familia, udhibiti wa matangazo ya  mbadala wa maziwa ya mama, na uwekezaji katika unyonyeshaji.

Mashirika ya WHO na UNICEF yamebaini kuwa kuboresha mifumo ya ufuatiliaji kutasaidia kuimarisha ufanisi wa sera na programu za unyonyeshaji, kutoa maamuzi bora, na kuhakikisha mifumo ya msaada inaweza kufadhiliwa vya kutosha.

Msaada kwa kina mama unawapa motisha

Ripoti hii inathibitisha kwamba kulinda na kusaidia unyonyeshaji miongoni mwa kina mama kutawafanya wanawake kuwa na uwezekano mara mbili wa kunyonyesha watoto wao.

Hata hivyo, ripoti hii imeonya kwamba familia, jamii, watoa huduma za afya, watunga sera, na wahusika wengine wote wana jukumu kubwa katika kuongeza kiwango cha unyonyeshaji watoto duniani.

Miongoni mwa majukumu ya pamoja ni, Kuongeza uwekezaji katika programu na sera zinazolinda na kusaidia unyonyeshaji kupitia bajeti maalum za kitaifa na Kutekeleza sera zinazofaa mahali pa kazi, kama likizo ya uzaziyenye malipo, mapumziko ya kunyonyesha, na upatikanaji wa huduma za watoto za gharama nafuu na zenye ubora.

Aidha, Kutoa msaada na ulinzi kwa mama walio katika hatari wakati wa dharura au jamii zilizowakilishwa kidogo,ikiwa ni pamoja na ushauri wa unyonyeshaji, kuboresha ufuatiliaji wa programu na sera za unyonyeshaji na Kuunda na kutekeleza sheria zinazokataza matangazo ya mbadala wa maziwa ya mama, ikiwa ni pamoja na mbinu za matangazo ya kidijitali.