Sudan inakabiliwa na hatari ya njaa huku ukatili dhidi ya watoto ukitamalaki: Gamba
Sudan inakabiliwa na hatari ya njaa huku ukatili dhidi ya watoto ukitamalaki: Gamba
Ripoti ya nane kuhusu watoto na migogoro ya silaha iliyotolewa leo jijini Newyork Marekani na ofisi ya mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa kuhusu watoto na migogoro ya silaha Virginia Gamba, inaonesha kuwa kuongezeka kwa haraka kwa uhasama na kuzorota kwa hali ya kibinadamu kumechochea ongezeko kubwa la ukatili dhidi ya watoto nchini Sudan.
Ripoti hiyo imebainisha kuwa ukatili mkubwa zaidi dhidi ya watoto ulithibitishwa kati ya tarehe 1 Januari 2022 na 31 Desemba 2023, ukidhihirisha ongezeko la kushangaza ikilinganishwa na kipindi kama hicho cha ripoti iliyopita.
Kwa mujibu wa ripoti “Mauaji na kulemazwa ulikuwa ni ukatili uliothibitishwa kwa kiwango cha juu zaidi, ukifuatiwana kusajili watoto vitani na kutumikishwa, ubakaji na aina nyingine za ukatili wa kingono dhidi ya watoto. “
Chachu ya ongezeko hilo
Ripoti inasema ongezeko kubwa la ukatili lilionekana baada ya kuzuka kwa mgogoro kati ya Jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka (SAF) tarehe 15 Aprili 2023.
Aidha, migogoro ya kijamii, hasa kati ya wafugaji na wakulima, imeendelea kusababisha ukatili dhidi ya watoto katika majimbo ya Darfur na Blue Nile.
Ripoti inaelezea kuwa vita nchini Sudan vimeleta madhara makubwa kwa hali ya kibinadamu kwa watoto, ambao sasa wanakabiliwa na njaa huku wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu nchini humo wakikabiliana na vikwazo vikubwa katika utoaji wa msaada.
Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu Virginia Gamba amesema, “hali nchini Sudan ni mbaya sana na maisha ya watoto nchini humo yako hatarini. Naziomba pande zote zinazohusika na migogoro kulinda raia na mali za raia, kwa kufuata sheria za kimataifa za kibinadamu, na kushirikiana na Umoja wa Mataifa kupitisha na kutekeleza hatua madhubuti za kulinda watoto, ikiwa ni pamoja na mipango ya utekelezaji.”
Gamba pia ameeleza wasiwasi wake kuhusu pengo lililoachwa na kumalizika kwa kazi ya mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo UNITAMS, pamoja na kuondoka kwa wafanyakazi maalum wa ulinzi wa watoto kutoka katika ujumbe huo, ambalo litakuwa na athari katika ufuatiliaji na utoaji ripoti kuhusu ukatili dhidi ya watoto.
Amesema “Hii itazuia ushirikiano na pande zinazohusika na migogoro pamoja na juhudi za kupunguza na kushughulikia mahitaji ya ulinzi wa watoto.”
Ushirikiano endelevu katika nyakati za changamoto
Ripoti imebainisha kuwa kabla ya kuongezeka kwa uhasama tarehe 15 Aprili 2023, maendeleo yalifikiwa hasa katika utekelezaji wa mwongozo wa 2021 kupitia uundaji wa mfumo wa kitaifa wa kuachiliwa na kurejeshwa kwa watoto.
Hii ilifanikisha shughuli ya kwanza ya pamoja ya uthibitishaji kati ya Umoja wa Mataifa na waliosaini Mkataba wa Amani wa Juba, ambao ulifanyika mapema mwaka 2023 na kuchangia kuachiliwa kwa watoto 122 kutoka kwa pande zinazohusika na migogoro.
Licha ya changamoto zilizojitokeza kutokana na kuongezeka kwa uhasama, Umoja wa Mataifa uliendelea na ushirikiano na pande zote zinazohusika na mgogoro.
Gamba amehitimisha kwa kusema, “Nina wasiwasi mkubwa kuhusu kiwango cha ukatili kinachowakumba watoto, uharibifu mkubwa wa miundombinu ya kiraia, ikiwa ni pamoja na shule na vituo vya afya, na ukosefu wa juhudi madhubuti za pande zinazohusika na migogoro kuwezesha utoaji wa misaada ya kibinadamu kwa watu wanaoteseka, ikiwa ni pamoja na watoto. Nawaomba pande zote kuhakikisha usitishwaji wa uhasama wa muda mrefu. Hatima ya watoto nchini Sudan inategemea hilo.”