Chonde chonde jizuieni na machafuko zaidi, UN yatoa wito kufuatia mashambulizi ya Israel mjini Beirut
Chonde chonde jizuieni na machafuko zaidi, UN yatoa wito kufuatia mashambulizi ya Israel mjini Beirut
Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi wake juu ya mashambulizi ya Israel katika viunga vya kusini mwa mji mkuu wa Lebanon, Beirut, jana Jumanne, ambayo yalisababisha vifo vingi vya raia.
Katika taarifa kwa waandishi wa habari jana jioni msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amesema "Tunaposubiri ufafanuzi zaidi juu ya hali hiyo, tunahimiza tena pande zote kujizuia na kutoa wito kwa wote wanaohusika kuepusha hali yoyote mbaya zaidi,"
Ujumbe huo pia umezikumbusha pande zote kuzingatia wajibu wao chini ya sheria za kimataifa, kujitolea kwa dharura kutekeleza kikamilifu azimio nambari 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lililopitishwa baada ya vita vya mwaka 2006 kati ya Hizbollah na Israel, na kurejea mara moja katika kusitisha mapigano.
Lazima kujizuia na machafuko zaidi
Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Lebanon, Jeanine Hennis-Plasschaert, pia alitoa wito wa kuwepo kwa utulivu katika taarifa yake akionyesha wasiwasi mkubwa juu ya mashambulizi hayo ambayo amebainisha kuwa yamefanyika katika katika kitongoji cha kusini mwa mji mkuu chenye wakazi wengi.
Plasschaert amesisitiza kwamba "Hakuna suluhu ambayo ni ya kijeshi, na kutoa wito kwa Israeli na Lebanon kutumia njia zote za kidiplomasia kurejea katika usitishaji wa mapigano na kujizatiti tena kwa utekelezaji wa azimio namba 1701 (2006).”
Mashambulizi hayo ya anga yalitokea kufuatia shambulio la roketi kwenye uwanja wa mpira wa kwenye Milima ya Golan inayokaliwa na Israel nchini Syria Jumamosi iliyopita.
Raia kumi na wawili, na haswa watoto na vijana, waliuawa katika shambulio hilo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres na maafisa wengine wakuu wa Umoja wa Mataifa wamelaani vikali shambulio hilo.
Nimesikitishwa na kinachoendelea: Wennesland
Naye Tor Wennesland, Mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya machakato wa amani wa Mashariki ya Kati akiongeza sauti yake kupitia ukurasa wa mtandao wa kijamii wa X amesema “Ninatiwa wasiwasi sana na maendeleo ya hivi karibuni Mashariki ya Kati ambayo yanaweza kuwa na athari kubwa kwa eneo hilo. Naomba tujizuie na tuepuke vitendo vinavyoweza kuyumbisha zaidi eneo hili.”
Wennesland amesema ameshawasiliana na wahusika wote kwa ajili ya kufanya kazi ili kupunguza mivutano.
Amesisitiza kuwa “Lengo la juhudi hizi liko wazi ni kupunguza kasi ya migogoro ya kikanda, ikiwa ni pamoja na kufikia usitishaji mapigano na kuachiliwa kwa mateka wote huko Gaza, na kufanya kazi kwa ajili ya amani ya kudumu.”
la juhudi hizi liko wazi - kupunguza kasi ya kikanda, ikiwa ni pamoja na kufikia usitishaji mapigano na kuachiliwa kwa mateka wote huko Gaza, na kufanya kazi kwa amani ya kudumu.