Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAIDS yatoa mafunzo ya kujikinga na UKIMWI kwa vijana nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati

Mwanamke Mwafrika anashikilia vidonge vitatu vyeupe vya kupunguza makali ya virusi vya ukimwi mkononi mwake.
© UNICEF/Olivier Asselin Dawa za HIV za kurefusha maisha zinasaidia kutoa matumaini kwa vijana barani Afrika

UNAIDS yatoa mafunzo ya kujikinga na UKIMWI kwa vijana nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na UKIMWI UNAIDS nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) linahamasisha jamii kupamba na na UKIMWI kwa kutoa elimu ya ngono salama kwa vijana.

Takwimu za UNAIDS zinaonesha watu milioni 30.7 wanaoishi na Virusi vya UKIMWI - VVU sasa wanapata matibabu. Hii ni hatua kubwa katika afya ya umma ambayo pia imepunguza takriban nusu ya vifo vinavyohusiana na UKIMWI tangu mwaka 2010, kutoka zaidi ya milioni moja hadi 630,000 mwaka 2023. 

Hata hivyo vifo hivyo ni vingi ikilinganishwa na lengo la kuwa na vifo 250,000 ifikapo mwaka 2025.

UNAIDS wanasema mwaka 2023 kulikuwa na wastani wa maambukizi mapya ya VVU milioni 1.3 na takriban nusu ya walioambukizwa wanaishi mashariki na kusini mwa Afrika (35%) huku magharibi na Afrika ya kati wakiwa na maambukizi kwa asilimia 15%.

Mkurugenzi wa UNAIDS, nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chris Fontaine anaeleza jinsi takwimu hizi zilimpelekea kutoa elimu kwa vijana kama anavyoeleza, “Vita na umaskini vimesababisha vifo vingi vya mapema nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, na matokeo yake, ni kuwa asilimia 78 ya idadi ya watu, ni chini ya umri wa miaka 35. Vijana hawa wanakabiliana na changamoto kubwa kupata elimu bora; kwa mfano, ni watu 4 kati ya 10 tu wa Kati ya Afrika ambao wanaweza kusoma na kuandika Ukosefu wa usawa wa kijinsia na ukatili wa kijinsia umewaacha wanawake katika hali hatarishi zaidi kwa VVU.”

Miongoni mwa waliopatiwa mafunzo katika Kituo cha Elimu kwa Afya ya Jinsia kwa Vijana, CISJEU ni Gniwali Ndangou. Ndangou  ambaye sasa ni mwalimu rika wa CISJEU na aliye katika mstari wa mbele katika juhudi za kupambana na UKIMWI anaeleza jinsi maisha yake yalivyokuwa kabla ya kupata mafunzo, “Mimi ni yatima, ni mimi pekee kati ya ndugu zangu watatu ambaye ninapata matibabu kila siku na ninakunywa dawa bila kuacha. Ninaishi na VVU tangu nilipozaliwa. Zaidi ya mara moja, nilijaribu kujiua kwa kunywa vidonge.”

Familia ya Kiafrika imeketi pamoja nje ya nyumba huko Benjaminkro, Côte d'Ivoire, huku baba akimfanyia mtoto wake kipimo cha VVU nyumbani.
© UNICEF/Frank Dejong Familia wakifanya vipimo vya HIV nyumbani

Tiba ipo

Ugonjwa wa VVU unaweza kuzuilika na kutibika na hakuna mtu anayepaswa kufa kutokana na ugonjwa huu. Hii ndiyo motisha ya walimu rika huko Bangui katika azma yao ya kuwaelimisha vijana wenzao kuhusu njia za kuzuia kueneza UKIMWI kwa kuzingatia mbinu salama za kujamiiana.

Kupitia vituo cha CISJEU, Gniwali na vijana wengi kama yeye sasa wana uelewa zaidi na wanaishi maisha yenye maisha yenye malengo na yenye afya.

Michael Guéret, ni Afisa wa Mpango wa CISJEU, na anaekeza kuhusu kituo hicho “CISJEU ni kituo kinachowajali vijana kinachotoa huduma nyingi kama vile kuzuia, uhamasishaji, na matibabu kulingana na mahitaji ya jamii na kwa ajili ya jamii. Pia tumeajiri na kuwafundisha waelimishaji rika 160. 80 wakiwa mashuleni na wengine 80 katika vituo vya vijana.”

Mapungufu makubwa yanaendelea kudhoofisha juhudi za kukomesha UKIMWI kwa watoto, huku zaidi ya nusu (57%) ya watoto wenye umri wa miaka 0-14 wakipata matibabu ya VVU.

Mwaka jana 2023 karibu watoto 120,000 wenye umri wa miaka 0-14 waliambukizwa VVU, wakati vifo vinavyotokana na UKIMWI miongoni mwa watoto vilifikia 76,000.