Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wasichana balehe wanakabiliwa na viwango vya kutisha vya ukatili mikononi mwa wenzi wao :WHO

WHO inasema wasichana balehe wanakabiliwa na  ukatili mkubwa mikoni mwa wenzi wao
© UNICEF/Olivier Asselin WHO inasema wasichana balehe wanakabiliwa na ukatili mkubwa mikoni mwa wenzi wao

Wasichana balehe wanakabiliwa na viwango vya kutisha vya ukatili mikononi mwa wenzi wao :WHO

Wanawake

Ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni WHO msichana barubaru 1 kati ya 6 waliokuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi mwaka jana, alikumbwa na ukatili wa kimwili au kingono kutoka kwa mpenzi wake.

Kwa mujibu wa ripoti karibu wasicna barubaru milioni 19 watakuwa wamepitia ukatili wa kingono wanapokuwa na umri wa miaka 20

Ripoti imechapishwa kwenye jarida la kitabibu la LANCET na inamnukuu Dkt. Pascale Allotey, kutoka WHO akisema ukatili huu unaweza kuwa na madhara ya kudumu kwa msichana husika na hivyo suluhisho lipatikane.

"Unyanyasaji kutoka kwa mpenzi wa karibu unaanza mapema kwa mamilioni ya wasichana barubaru duniani kote, Ikizingatiwa kwamba ukatili katika miaka hii muhimu ya malezi unaweza kusababisha madhara makubwa na ya kudumu, hivyo unahitaji kuchukuliwa kwa uzito zaidi kama suala la afya ya umma kwa kuzingatia kuzuia na msaada maalum unaolengwa kwa kundi hilo."

Ukatili huo unaweza kuwa na athari mbaya kwa afya ya vijana, mafanikio ya kielimu, mahusiano ya baadaye, na matarajio ya maisha yote.

Kwa mtazamo wa afya, WHO inasema huongeza uwezekano wa majeraha, huzuni, matatizo ya wasiwasi, mimba zisizopangwa, magonjwa ya zinaa, na hali nyingine nyingi za kimwili na kisaikolojia.

wasichana wakimbizi wa ndani katika kituo kinachosaidiwa na UNICEF cha Al Salam Sudan
© UNICEF/Ahmed Elfatih Mohamdeen wasichana wakimbizi wa ndani katika kituo kinachosaidiwa na UNICEF cha Al Salam Sudan

Ukatili huu ni dalili ya ukosefu wa usawa

Utafiti huu unatumia takwimu zilizopo ili kutoa uchambuzi wa kina wa kuenea kwa unyanyasaji wa kingono wanaofanyiwa wasichana wenye umri wa miaka 15-19 ambao wamekuwa katika mahusiano.

Pia ripoti inabainisha mambo mapana zaidi ya kijamii, kiuchumi na kiutamaduni ambayo huongeza hatari zao.

Kulingana na makadirio ya WHO, kanda zilizoathiriwa zaidi ni Oceania  asilimia 47 na Afrika ya kati Kusini mwa Jangwa la Sahara asilimia 40, wakati viwango vya chini zaidi ni Ulaya ya kati asilimia 10 na Asia ya Kati asilimia 11, kutoka kwa takriban asilimia 6 ya wasichana balehe waliofanyiwa ukatili kama huo katika nchi zilizoathiriwa kidogo, hadi asilimia 49 kwa zile zilizo na viwango vya juu zaidi. 

Uchambuzi huo mpya umegundua kuwa ukatili wa mpenzi wa karibu dhidi ya wasichana balehe ni jambo la kawaida katika nchi na kanda za kipato cha chini, katika maeneo ambayo kuna wasichana wachache katika shule za sekondari, na ambapo wasichana wana haki dhaifu ya umiliki wa mali na urithi ikilinganishwa na wanaume.

Ndoa za utotoni zimetajwa kuwa huongeza hatari kwa kiasi kikubwa, kwa kuwa tofauti za umri wa wenzi wa ndoa husababisha kutofautiana kwa mamlaka, utegemezi wa kiuchumi, na kutengwa kwa jamii, haya  yote huongeza uwezekano wa kuvumilia unyanyasaji.

Wasichana wa shule za msingi hutembea hadi kituo cha jamii kinachoungwa mkono na UNICEF katika Wilaya ya Shahristan (Maktaba)
© UNICEF/Mark Naftalin Wasichana wa shule za msingi hutembea hadi kituo cha jamii kinachoungwa mkono na UNICEF katika Wilaya ya Shahristan (Maktaba)

Wasichana balehe wanahitaji huduma na msaada

Utafiti pia unaangazia hitaji la dharura la kuimarisha huduma za usaidizi na hatua za kuzuia mapema zilizolengwa kwa vijana, sambamba na hatua za kuendeleza mashirika ya haki za wanawake na wasichana kuanzia kwenye programu za shule zinazoelimisha wavulana na wasichana juu ya uhusiano mzuri na kuzuia unyanyasaji, hadi kisheria, ulinzi, na uwezeshaji wa kiuchumi.

Kwa kuwa vijana wengi hawana rasilimali zao wenyewe za kifedha, wanaweza kukabiliana na changamoto fulani katika kuacha mahusiano mabaya.

"Utafiti unaonesha kuwa ili kukomesha unyanyasaji wa kijinsia, nchi zinapaswa kuwa na sera na programu zinazochagiza usawa kwa wanawake na wasichana," amesema mwandishi wa utafiti huo Dkt. Lynnmarie Sardinha, Afisa wa kiufundi wa takwimu na vipimo dhidi ya unyanyasaji wa wanawake katika shirika la WHO.

Kwa mujibu wa ripoti kwa sasa, hakuna nchi iliyo katika njia nzuri ya kukomesha unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana kufikia tarehe ya ukomo wa malengo ya Maendeleo Endelevu la 2030.

Kukomesha ndoa za utotoni ambazo huathiri msichana 1 kati ya 5 duniani kote na kupanua wigo wa ongezeko la wasichana kwenye elimu ya sekondari itakuwa sababu muhimu za kupunguza unyanyasaji wa mpenzi dhidi ya wasichana balehe.

WHO inaunga mkono nchi kupima na kushughulikia unyanyasaji dhidi ya wanawake, ikiwa ni pamoja na juhudi za kuimarisha kinga na hatua ndani ya sekta ya afya. Miongozo mipya ya WHO kuhusu kuzuia ndoa za utotoni imepangwa kutolewa ifikapo mwisho wa mwaka 2024.