Mgao wa chakula wa WFP waleta nuru kwa wakazi wa Mangina DRC
Mgao wa chakula wa WFP waleta nuru kwa wakazi wa Mangina DRC
Mangina, ni wilaya ya vijijini inayopatikana takriban kilomita 30 magharibi mwa mji wa Beni, jimboni Kivu Kaskazini, mashariki mwa DRC. Mangina ni eneo ambalo limekaribisha watu wengi waliokimbia makazi yao kutokana na mashambulizi mengi ya makundi yenye silaha, ikiwemo waasi wa ADF ambao walichoma nyumba zao na kupora mali zao
Wanaume, wanawake na watoto wengi waliokimbia makazi yao wanakabiliwa na lishe duni. Hospitali kuu ya MANGINA inasema kuwa takribani wanawake 200 na watoto zaidi ya 300 wamegundulika kuwa na utapiamlo mkali.
Claude Kalinga, Msemaji wa Ofisi ya shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani-WFP nchini DRC, anatangaza kwamba Umoja wa Mataifa, kupitia shirika hilo umeanzisha miradi kadhaa ya lishe kwa ajili ya watu hao walio katika mazingira magumu, ili kupambana na janga hili.
Claude Kalinga, Msemaji wa WFP nchini DRC anasema " Kwa bahati mbaya, tumesitisha shughuli zetu za kugawa chakula huko Mabalako kufuatia ukosefu wa fedha. Tumesitisha kazi hii tangu Machi mwaka huu. Lakini pia kwa bahati nzuri kila kitu kiko shwari, tulizindua shughuli za lishe katika mwezi huo huo wa Machi, ambapo tunalenga watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, wajawazito na wanaonyonyesha ili kupambana na utapiamlo mkali".
Nilisafiri hadi Mangina kukutana na wanufaika wa mradi huu wa WFP. Masika Maombi Françoise mkazi wa Mangina ni mama wa watoto wanane , ambapo wawili kati yao wanakabiliwa na lishe duni. Akisema PAM anamaanisha WFP. " Nimejikuta hapa kwa sababu nilikuja na watoto wangu hospitalini kwa matibabu. Lakini watoto hugunduliwa na lishe duni. Kwa hiyo niliombwa nisubiri hadi watibiwe na kupewa chakula ili kutibu lishe duni. Ni PAM (WFP) inayotupa chakula hiki na ninashukuru kwa sababu inasaidia watoto wetu".
Kaswera Mathumo Jolie, daktari wa watoto katika hospitali ya Mangina akanieleza umuhimu wa chakula hiki kwa watoto. " Tunalenga watoto wenye umri wa kuanzia miezi 6 hadi miaka mitano. Kipimo cha kwanza ni mzunguko eneo la juu la mkono.. Ikiwa kipimo kitakuwa kwenye alama ya manjanoau nyekundu , basi atakuwa amebainika na utapiamlo hivyo apatiwa lishe. Pia tunapima uzito na urefu wa mtoto hivyo tunaangalia hali yake ya lishe ili aanze kwa uangalizi na kupewa chakula. Chakula hiki tunachotoa ni mchanganyiko wa karanga ambacho kinatolewa na kanisa la 8 CEPAC, ambalo lilifadhiliwa na WFP".
Nikamuuliza Jolie wanafanya nini kwa wajawazito? " Mbali ya watoto, pia tunalenga wanawake wajawazito na wanaonyonyesha walio na watoto wenye umri wa chini ya miezi 6. Kwa wajawazito tunachukua wale ambao wana kipimo ya mzunguko wa juu wa mkono wa chini ya mia mbili na thelathini . Pia tunachukua wajawazito wenye umri wa chini ya miaka 18 na pia kiwango cha damu chini ya gramu 10 za damu. Wanawake hawa tunawapatia uji, uji huu ni mchanganyiko wa unga wa mahindi, soya, mafuta na maziwa kidogo. Tunachanganya na kutoa mgawo kwa wiki mbili ama ya mwezi mzima".
Nikarejea kwake Claude Kalinga, anazungumzia matatizo tofauti ambayo WFP inakabiliana nayo Mashariki mwa DRC. "Eneo hili jimboni Kivu Kaskazini, ni mazingira maalum kwa sababu tumekuwa tukikabiliwa na taarifa potofu na za uongo kwa miaka mingi, lakini pia kila aina ya uvumi kuhusu kazi ya WFP. Hii ndiyo sababu tunakuja mara kwa mara katika eneo hili ili kujaribu kufanya kazi na washirika wetu kutoka jumuiya mbalimbali ili kuwaletea taarifa sahihi na za kweli".
Nikukumbushe kwamba mnamo Oktoba mwaka 2023, kwa sababu ya habari potofu na za uongo baada ya mauaji ya watu 26 huko Oicha jimboni Kivu Kaskazini, wakazi wenye hasira walichoma moto malori matatu ya WFP yaliyokuwa yakisafirisha shehena ya chakula.
Tani kadhaa za maharagwe, unga na mafuta yaliyokusudiwa kwa ajili ya wakimbizi ziliteketea.