Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hakuna mtoto anayepaswa kuachwa nyuma katikavita dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu: UNODC/IOM

Msichana akiwa amegeukia kamera ameketi kwenye bembea ya kijani na njano kwenye uwanja wa michezo.
© UNODC/Alejandra Silva Uwanja wa kuchezea watoto Macedia Kaskazini

Hakuna mtoto anayepaswa kuachwa nyuma katikavita dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu: UNODC/IOM

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Siku ya Kimataifa ya Kupinga Usafirishaji Haramu wa Binadamu huadhimishwa tarehe 30 Julai kila mwaka. Kaulimbiu ya mwaka huu ni "Hakuna mtoto anayepaswa kuachwa nyuma katika vita dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu."

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Dawa na Uhalifu (UNODC) imeandaa nyenzo za utafiti kuhusu utumikishwaji wa watoto ili kuongeza uelewa wa tatizo hili la kimataifa na kutoa wito wa kuchukua hatua za kukomesha usafirishaji haramu wa binadamu.

Usafirishaji haramu wa watoto ni nini?

Usafirishaji haramu  wa watoto unahusisha matumizi ya watoto yanayofanywa na wahalifu kwa lengo la utumikishwaji. Huu ni uhalifu mkubwa na ukiukaji wa haki za binadamu, hata kama inaonekana kwamba mtoto amekubali kwa namna fulani "kutumikishwa." Mara nyingi, hii hufanyika kupitia kutumia nguvu, udanganyifu, kulazimishwa, matumizi mabaya ya mamlaka, au mazingira magumu.

Picha ya mwili wa mtu anaye na nywele zimefungwa kwenye bun, ameketi kwenye kiti na kuangalia nje ya dirisha lenye vichwa.
IOM/Muse Mohammed Teknolojia hii itaboresha uzalishaji wa akwimu za kuhifadhi faragha na kuharakisha sera inayozingatia ushahidi katika mapambano dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu

Watoto wanaweza kutumikishwa katika njia mbalimbali. Miongoni mwao ni:

utumikishwaii wa kingono, ambao unaweza kujumuisha dhuluma dhidi  watoto ili kuwatumikisha kingono kwa malengo ya biashara au utengenezaji wa nyenzo za ukatili wa kijinsia kwa watoto. Aidha, kazi za shuruti ambapo watoto hufanya kazi katika mazingira magumu kwenye sekta mbalimbali, ikiwemo kilimo, viwanda, migodi au kama wafanyakazi wa majumbani. Njia nyingine ya utumikishwaji ni kuwalazimisha watoto kuombaomba mitaani au kufanya uhalifu kama vile wizi. Watoto katika migogoro ya silaha hutumikishwa kwa kuchukuliwa kama wapiganaji, kutumiwa kingono au kuwekwa katika utumwa wa majumbani. Ndoa za utotoni ni njia nyingine ya utumikishwaji unaowaathiri zaidi wasichana.Wasichana hawa wanaozeshwa kwa malipo au ili kuboresha hali ya kijamii, mara nyingi kama sehemu ya mil ana desturi za kitamaduni zenye madhara. Kuasili watoto kinyume cha sheria ni utumikishwaji unaojumuisha usafirishaji wa watoto kwa ajili ya kwaasili kwa lengo la kuwatumikisha, mara nyingi kwa kuwalaghai au kuwalazimisha wazazi au walezi wao.

Wakati mwingine waathiriwa wa usafirishaji haramu wa watoto wanaweza kutumikishwa  katika njia kadhaa. Kwa mfano, mtoto anayelazimishwa kuombaomba mitaani anaweza pia kutumikishwa kingono.

Mtu akiwa ameshika bango la maandamano linalosomeka 'Usafirishaji haramu wa binadamu unafanyika hapa' wakati wa maandamano ya umma.
© Unsplash/Hermes Rivera "Walk For Freedom" ni siku ya uhamasishaji duniani na upiganaji wa hatua za ndani katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu.

Usafirishaji haramu wa watoto ni wa kawaida kwa kiasi gani?

Mwaka wa 2020, UNODC ilirekodi takriban visa 20,000 vya usafirishaji haramu wa watoto. Hata hivyo, kutokana na ugumu wa kugundua utumikishwaji na kuripoti rasmi, idadi halisi inaweza kuwa kubwa zaidi.

Katika miaka 15 iliyopita, idadi ya watoto kati ya waathiriwa waliotambuliwa wa usafirishaji haramu wa binadamu imeongezeka mara tatu. Takriban 1 kati ya waathiriwa 3 waliotambuliwa ni mtoto.

Wasichana na wavulana wanaathirika na usafirishaji haramu wa binadamu, lakini inaweza kuathiri watoto kwa njia tofauti kulingana na jinsia na eneo. Wasichana wanasafirishwa zaidi kwa utumikishwaji wa kingono, wakati wavulana wanasafirishwa kwa ajira za shuruti.

Usafirishaji haramu wa watoto unafanyika wapi?

Usafirishaji haramu wa watoto hufanyika duniani kote, lakini kwa utofauti wa kieneo. Kaskazini mwa Afrika na Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, kwa mfano, watoto wanachangia sehemu kubwa ya waathiriwa wa usafirishaji haramu, na ajira ya kulazimishwa ndio imekithiri Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Hata hivyo, katika Amerika ya Kati na Karibea, waathiriwa wengi waliotambuliwa ni wasichana, hasa vijana balehe, ambao wamesafirishwa kwa utumikishwaji wa kingono. Kusini mwa Asia, karibu nusu ya waathiriwa ni watoto waliotumikishwa kama wafanyakazi au kulazimishwa kuolewa.

Wanawake wawili vijana wanaingiza vipodozi katika chumba chenye mwanga mdogo na kioo. Mwanamke mmoja ni katika mbele amevaa blouse nyekundu, wakati mwingine mwanamke mmoja aliyevaa blouse ya rangi ya pinki anavyoonekana katika kioo.
© UNICEF/UNI91025/Noorani Msichana akijipodoa katika dangura mji wa Tangail nchini Bangladesh. Mwanamume alwaahidi kuwatafutia kazi lakini badala yake akawauza Kandapara.(2009)

Je, ni kwa jinsi gani watoto huwa katika hatari ya kutumikishwa?

Usafirishaji haramu  wa watoto unastawi katika hali ya matatizi kwenye familia, umaskini, ukosefu wa usawa, ulinzi usiotosha na ukosefu wa malezi ya wazazi. Wahalifu mara nyingi hulenga watoto kutoka familia maskini sana au wale walioachwa na wazazi na walezi wao. Migogoro, matatizo ya kiuchumi na majanga ya mazingira yanawafanya watoto, hasa wale wasio na walezi na waliotengana na familia zao, kuwa katika hatari zaidi.

Wakati wasafirishaji wengi wa binadamu ni wahalifu sugu, wanaweza pia kuwa wajasiriamali wa ndani, wapenzi wa karibu, na wanafamilia. Wasafirishaji haramu  wa binadamu hutumia majukwaa ya mtandaoni, mitandao ya kijamii, na wavuti za siri kuwasiliana, kutumikisha na kudumisha mamlaka mabaya dhidi ya watoto. Kwa msaada wa teknolojia ya kisasa, wanakwepa kugunduliwa na kuendelea kusambaza maudhui ya kikatili.

Matumizi ya watoto ya mtandao na mitandao ya kijamii bila uangalizi, mara nyingi bila hatua sahihi za usalama, yanaweza kuwaweka watoto  katika hatari zaidi ya kutumikishwa.

Usafirishaji haramu wa watoto unaathiri vipi waathiriwa na jamii?

Uhalifu huu una madhara makubwa kwa ukuaji wa kimwili, kiakili na kijamii wa watoto. Waathiriwa mara nyingi wanapata matatizo ya kiafya ya muda mrefu, matatizo ya kiwewe, wasiwasi, msongo mawazo, na matatizo ya kujumuika kijamii. Watoto wana uwezekano wa kukumbwa na ukatili mkubwa na wasafirishaji haramu wa binadamu mara mbili zaidi ikilinganishwa na waathiriwa watu wazima. Idadi hii ni kubwa zaidi miongoni mwa wasichana.

Mwanamke aliyevaa shati lenye muundo anainua mkono wake kuelekea bango kubwa lililofunikwa kwa alama za mikono zenye rangi nyingi lenye maandishi '#EndHumanTrafficking'.
© UNHCR/Osama Idriss Mkimbizi ambaye familia yake iliathirika na usafirishaji haramu wa binadamu akiunga mkono kampeni ya UNHCR ya kupinga usafirishaji haramu wa binadamu Sudan

UNODC inafanya nini kushughulikia tatizo hili?

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Dawa na Uhalifu UNODC inafanya kazi ya kuongeza uelewa kuhusu tatizo hili la kimataifa na kuchochea hatua za kukomesha usafirishaji haramu wa watoto, aidha inafanya utafiti juu ya mada hiyo.

UNODC pia inatoa msaada wa kiufundi kwa mataifa katika kuzuia uhalifu, utendaji wa haki na ulinzi wa waathiriwa, pamoja na utekelezaji mzuri wa itifaki ya kimataifa ya kuzuia, kukandamiza na kuadhibu usafirishaji haramu wa binadamu, hasa wanawake na watoto. Ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa inatengeneza mwongozo wa hatua za haki na ulinzi kuwasaidia watoto walioathirika na utumikishwaji . Pia inachambua vipaumbele ili kubaini matatizo katika uchunguzi, mashtaka na hukumu na kutoa mapendekezo sahihi kwa nchi.

UNODC inaratibu kazi ya Kikosi cha Uratibu wa Mashirika ya kupinga usafirishaji haramu wa binadamu. Mwaka 2023, jukwaa hili la Umoja wa Mataifa, lililoongozwa na shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji (IOM) na Ofisi ya Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu Ukatili dhidi ya Watoto, na lilitoa wito wa hatua za haraka kuzuia na kumaliza usafirishaji haramu wa watoto ifikapo mwaka 2025.