Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya Gaza ni janga kubwa la kibinadamu: Kaag

Sigrid Kaag Mratibu Mwandamizi wa Kibinadamu na Ujenzi wa Gaza
UN Photo/Manuel Elías
Sigrid Kaag Mratibu Mwandamizi wa Kibinadamu na Ujenzi wa Gaza

Hali ya Gaza ni janga kubwa la kibinadamu: Kaag

Amani na Usalama

Mratibu Mwandamizi wa Kibinadamu na Ujenzi wa Gaza Sigrid Kaag leo amesema hali katika Ulanda wa Gaza inasalia kuwa “Janga kubwa la kibinadamu na kiwango cha uharibifu kinakaribia kutoelezeka.”

Kaag, ameyasema hayo akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya video kutoka Amman, na kuongeza kuwa "Kwa muda wa miezi kumi sasa, raia wa Palestina wamekumbwa na hali mbaya ya maafa ya kibinadamu, kuanzia kwenye kiwango cha uharibifu hadi athari na kiwewe kwa maisha ya mtu binafsi, bila shaka, ikiwa ni pamoja na idadi kubwa ya watu ambao ni raia waliopoteza maisha.”

Ameendelea kusema kuwa wakati joto la kiangazi linaongezeka timu ya Umoja wa Mataifa na washirika "wanafanya kazi kwa kweli kushughulikia uhaba mkubwa wa usimamizi wa taka na vifaa vya usafi wa mazingira, haswa ikiwa tutaendelea kushuhudia hatari ya milipuko linapokuja suala la magonjwa ya kuambukiza."

Kaag amesema kazi ya Umoja wa Mataifa inalenga "kuhakikisha kuwa tuko tayari, ikiwa wakati usitishaji uhasama unahitajika sana utakapotangazwa na kurasimishwa."

Uharibifu mkubwa wa makazi ya watu Gaza
UN News/Ziad Taleb
Uharibifu mkubwa wa makazi ya watu Gaza

UN na wadau wanahaha kukusanya msaada

Afisa huyo amesema hivi sasa "Umoja wa Mataifa na washirika wake wanafanya kazi kuongeza usambazaji wa msaada kupitia akiba ya awali kutoka Jordan na Misri. Tunawaomba wafadhili waendelee kufadhili, na bila shaka katika ngazi ya kisiasa, ninashirikiana na kila mtu kuhakikisha kwamba tunaweza kufanya hivyo na kufikisha msaada.”

Kaag amesema, "Ninaulizwa swali, bila shaka, tunahitaji nini? Je, ni mateso na kiwewe gani huletwa kwa raia wasio na hatia? Na ni ujumbe gani unaotoa kuhusu uwezo wa kuikwamua na kuijenga upya Gaza?"

Amesema, "kwa uelewa wetu, kuna jukumu la wazi kwa Mamlaka ya Palestina linapokuja suala la vipaumbele na linapokuja suala la uwezeshaji, linapokuja suala la umiliki na kuungwa mkono na watu kwa kile kinachohitajika kufanywa, ambapo inahitajika kufanywa. Kuirejesha na kuijenga upya sio mchakato rahisi. Ukiangalia masuala rahisi sana, muhimu, umiliki wa ardhi, watoto wanataka shule ya aina gani ikiwa hawako katika shule ya kawaida? Ikiwa wataenda shule ya sekta ya umma, ni mahitaji gani? ubunifu wa ajira. Ni orodha ndefu.”

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alimteua Kaag Desemba 2023 kama Mratibu Mwandamizi wa Kibinadamu na Ujenzi wa Gaza kwa mujibu wa Azimio 2720 la Baraza la Usalama (2023).

Katika jukumu hili, anawezesha, kuratibu, kufuatilia, na kuthibitisha shehena za misaada ya kibinadamu kwenda Gaza.