Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Amri za Israel za watu kuhama kila wakati zimefurutu ada: UNRWA

Wapalestina waliokimbia makazi yao, wakiwemo wanawake, watoto, na wazee, wanahamishwa kutoka Khan Younis huko Gaza kwa mikokoteni inayokokotwa na punda, wakiishi katika hali mbaya.
© UNRWA Khan Younis amri mpya ya watu kuhama inazilazimisha familia wakiwemo watoto na wazee kukimbia tena kwenda kusaka ausalama

Amri za Israel za watu kuhama kila wakati zimefurutu ada: UNRWA

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA limesema sasa amri za Israel za watu kuhama kwenye Ukanda wa Gaza zimefurutu ada kwani ni asilimia 14 pekee ya eneo zima la Gaza ndio haliko chini ya amri za kuhama.

Kamishina Mkuu wa UNRWA Philippe Lazarini kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X amesema “Kila baada ya siku moja Mamlaka za Israeli hutoa maagizo haya na kulazimisha watu kukimbia, na kusababisha zahma na hofu kubwa”.

Ameongeza kuwa mara nyingi, watu huwa na saa chache tu za kubeba chochote wanachoweza na kuanza tena safari, hasa kwa miguu au kwenye mikokoteni ya punda waliojaa kwa wale wanaoweza kumudu.

Amri hizi zinamuathiri kila mtu

Mkuu huyo wa UNRWA amesema mwanaumme mmoja muathirika ametuambia kuwa “Takriban kila mtu katika Ukanda wa Gaza ameathiriwa na maagizo haya. Wengi wamelazimika kukimbia kwa wastani mara moja kwa mwezi tangu vita ilipozuka upya miezi tisa iliyopita.”

Ameendelea kusema mwanaume huyo hivi karibuni alilazimika kukimbia mara mbili ndani ya saa 10.

Lazzarini ameikumbusha dunia kwamba Gaza “Watu wanaendelea kutafuta usalama, kitu cha thamani zaidi, ambao haupo. Mbinu hii ya uokoaji inaleta tu taabu, hofu na mateso zaidi kwa watu ambao hawana uhusiano wowote na vita hivi vinavyoendelea.”

Mehitimisha ujumbe wake kwa kusisitiza kwamba “. Watu wa Gaza sio mpira wa pini wa kupigwa danadana au vipande vya chess, ni watu.”