Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mabadiliko ya tabianchi na matumizi ya bidhaa za misitu vyaiweka misitu hatarini zaidi – FAO

Bundi Mkuu Mwenye Pembe Anatua kwenye tawi la mti katikati ya majani mabichi.
©UNEP/Jessica Kerr Mabadiliko ya tabianchi yanazidi kuhatarisha mustakabali wa misitu duniani

Mabadiliko ya tabianchi na matumizi ya bidhaa za misitu vyaiweka misitu hatarini zaidi – FAO

Tabianchi na mazingira

Mabadiliko ya tabianchi yanazidi kuongeza uwezekano wa misitu duniani kukabiliwa na matatizo kama vile mioto wa nyika na wadudu, imesema ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) ambalo linasisitiza unuhimu wa ubunifu katika kufikia mustakabali endelevu kwa sekta ya misitu.

Ikipatiwa jina Hali ya Misitu Duniani 2024: Ubunifu wa Sekta ya Misitu kuelekea mustakabali endelevu zaidi (SOFO), ripoti hiyo imetolewa leo Jumatatu katika kikao cha 27 cha Kamati ya Misitu (COFO), ambacho kinafanyika katika makao makuu ya FAO jijini Roma, Italia.

Ripoti inasema mabadiliko ya tabianchi yanasababisha misitu kuwa hatarini zaidi kuvamiwa na mimea vamizi, huku wadudu na viini vya magonjwa vikihatarisha ukuaji na uhai wa miti.

Misonobari inashambuliwa na wadudu

Minyoo aina ya pine nematodes ambayo hudhuru miti aina ya misonobari tayari wamesababisha uharibifu mkubwa kwa misitu ya asili ya misonobari katika baadhi ya nchi za Asia, na maeneo ya Amerika Kaskazini yanatarajiwa kupata uharibifu mkubwa kutokana na wadudu na magonjwa kufikia mwaka 2027.

Kadhalika, ukataji miti kwa ajili ya kuni duniani, umesalia katika viwango vya juu baada ya kushuka kwa muda mfupi wakati wa janga la coronavirus">COVID-19.

Makadirio yanaonesha kuwa mahitaji ya miti duniani yanaweza kuongezeka kwa asilimia 49 kati ya 2020 na 2050.

Kwa mujibu wa ripoti hii, ubunifu katika sekta ya kilimo utachangia kwa kiasi kikubwa katika kutatua changamoto kama hizi  ili kuwezesha kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu .

Mkurugenzi Mkuu wa FAO QU Dongyu, akinukuliwa kwenye taarifa ya shirika hilo iliyotolewa leo Roma, Italia amesema, "FAO inatambua kwamba sayansi na ubunifu ni muhimu katika kufikia suluhu zenye msingi wa misitu. Toleo hili la SOFO litawezesha FAO kuongeza ubunifu unaotegemea utafiti katika misitu. Ninaamini pia itasaidia Wanachama wa FAO na wadau wengine katika kuwezesha ubunifu unaowajibika, jumuishi, na muhimu katika sekta ya misitu ili kuimarisha uendelevu na uthabiti wa mifumo ya kilimo kwa ajili ya dunia bora na mustakabali bora kwa wote.”

Suluhu Bunifu

Ripoti hii inabainisha aina tano za ubunifu zinazoongeza uwezo wa misitu kushughulikia changamoto za kimataifa: kiteknolojia, kijamii, sera, taasisi, na kifedha.

Mifano ni pamoja na uwezo wa akili mnemba  kuwezesha uchambuzi wa kiotomatiki wa wingi wa takwimu zinazokusanywa moja kwa moja kwa kutazama rada, na zile za lidar zilizokusanywa kila siku na droni, setilaiti, na vituo vya anga.

Vilevile  kupitishwa kwa ubunifu katika matumizi ya mbao zitokanazo na taka na zile zisizohitaji mafuta kisukuku.

Aina nyingine za ubunifu uliobainishwa ni kuwa na  sera zinazolenga kuwashirikisha wanawake, vijana, na watu wa jamii za asili katika kuendeleza suluhisho zinazoongozwa na jamii pamoja na ubunifu katika sekta ya fedha za umma na binafsi ili kuongeza thamani ya misitu.

Ripoti hii inapendekeza mbinu jumuishi na zinazozingatia jinsia ili kuhakikisha ugawaji sawa wa manufaa miongoni mwa wanaume, wanawake na vijana katika makundi yote ya kijamii na kiuchumi na kikabila. Kukuza uvumbuzi lazima kuzingatia na kuunganisha washikadau wote hali ya mahali, mitazamo, maarifa, mahitaji na haki.

Ripoti hii pia  imeorodhesha hatua tano ambazo zitasaidia kuongeza ubunifu katika sekta ya misitu: kuongeza uelewa, kukuza ujuzi wa ubunifu, uwezo na maarifa, kuhimiza ubia wa kuleta mabadiliko, kuhakikisha upatikanaji wa fedha zaidi na kwa wote kwa ajili ya ubunifu, na kutoa sera na mazingira ya udhibiti yanayotia motisha.