Israel yashambulia msafara wa Umoja wa Mataifa huko Gaza
Israel yashambulia msafara wa Umoja wa Mataifa huko Gaza
Majeshi ya Israel yamefanya mashambulizi makali dhidi ya msafawa wa Umoja wa Mataifa uliokuwa katika kituo cha ukaguzi wakati wakielekea mjini Gaza hapo jana. Limesema leo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina UNRWA katika wavuti wake.
Akiripoti kuhusu tukio hilo katika mtandao wake wa X Kamishna Mkuu wa UNRWA Philippe Lazzarini ametaka wale wote waliohusika katika tukio hilo wawajibishwe. “Mashambulizi makali kutoka kwa Wanajeshi wa Israel kwenye msafara wa Umoja wa Mataifa uliokuwa ukielekea katika wa Gaza. Ingawa hakuna majeruhi, timu zetu zililazimika kujificha”.
Mkuu huyo wa UNRWA ameeeleza kuwa moja ya magari ambayo hayaingii risasi la Umoja wa Mataifa lilishambulikwa kwa kupigwa "angalau risasi tano" wakati likingoja mbele kidogo ya kituo cha ukaguzi cha Wanajeshi wa Israel kusini mwa Wadi Gaza, eneo ambalo linagawanya kaskazini na kusini mwa eneo hilo.
“Gari limeharibika vibaya, liliacha msafara. Timu hizo zilikusanyika tena na hatimaye walifika mjini Gaza,” alisema Bw. Lazzarini, akiongeza kuwa msafara huo “umeratibiwa na kuidhinishwa” na Mamlaka za Israel “kama ilivyokuwa kwa misafara mingine yote ya Umoja wa Mataifa”.
Maagizo mapya ya wanagaza kutakiwa kuhama yawaathiri walioko Khan Younis
Maagizo hayo mapya yanajiri huku mashambulizi zaidi ya anga na silaha kali za Israel yakiendelea kulenga vijiji vya mashariki mwa Khan Younis. Maagizo mapya ya wananchi kutakiwa kuhama yametolewa na wanajeshi wa Israel kwa watu wanaopata hifadhi katika maeneo ambayo hapo awali yalitaja kama eneo "salama" la kibinadamu magharibi mwa Khan Younis, ambapo watu wapatao 400,000 wanaaminika kuwa wamejihifadhi huko, kwa mujibu wa mamlaka za eneo hilo.
Vyombo vya habari vinavyolinukuu jeshi la Israel vimedokeza kuwa itakuwa hatari kukaa katika maeneo haya kwani lilinuia kujibu mashambulizi yaliyoanzishwa dhidi yake kutoka huko.
Kwa mujibu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada, OCHA, takriban watu tisa kati ya 10 huko Gaza wameyakimbia makazi yao angalau mara moja tangu Oktoba mwaka jana.
Watu wengi wanaishi katika hali mbaya, shirika la Umoja wa Mataifa lilionya, huku magonjwa ya kuambukiza yakiongezeka.
Wakitoa mfano wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani, WHO, ambalo liliripoti kwamba kutoka 7 Oktoba hadi 7 Julai, karibu watu milioni moja walirekodiwa kupata maambukizi ya magonjwa ya kupumua. “Takriban wagonjwa 575,000 wa kuharisha na zaidi ya wagonjwa 00,000 waliogua homa ya manjano”, Hata hivyo WHO imesema huenda idadi halisi ya maambukizo inaweza kuwa kubwa zaidi.
Mauaji ya watoto huko Ukingo wa Magharibi
Wakati huo huo hii leo imetolewa ripoti inayoeleeza katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na walowezi wa Israel, Shirika la Umoja wa Mataifa la la Kuhudumia Watoto UNICEF limesema kumeongezeka mauaji ya vijana zaidi ya mara tatu tangu Oktoba 7 2023, ikilinganishwa na miezi tisa ya mwanzo ya 2023.
Kwa wastani kijana mmoja wa Kipalestina anafariki kila baada ya siku mbili.
Shirika hilo limesema kuwa watoto 143 wa Kipalestina wameuawa katika Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na Jerusalem Mashariki, tangu mashambulizi ya kigaidi yanayoongozwa na Hamas nchini Israel yalipoanzisha vita huko Gaza, ikilinganishwa na watoto 41 wa Kipalestina waliouawa kuanzia Januari hadi Septemba 2023.
Watoto wawili wa Israel pia waliuawa katika Ukingo wa Magharibi katika ghasia zinazohusiana na migogoro katika kipindi hicho, UNICEF ilisema, na kuongeza kuwa zaidi ya watoto 440 wa Kipalestina pia wamejeruhiwa kwa risasi.
“Kwa miaka kadhaa sasa, watoto wanaoishi katika Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na Jerusalem Mashariki, wamekabiliwa na ghasia za kutisha," Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Bi. Catherine Russell alisema na kuongeza kuwa “Hali imezorota kwa kiasi kikubwa, sambamba na kuongezeka kwa uhasama ndani ya Gaza. Tunaona madai ya mara kwa mara ya watoto wa Kipalestina kuzuiliwa wakirudi nyumbani kutoka shuleni, au kupigwa risasi wakitembea barabarani. Vurugu zinapaswa kukomeshwa sasa.”
Kuishi kwa hofu kila siku
Vitendo vya watoto kujeruhiwa vimeripotiwa katika majimbo 10 kati ya 11 katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu; zaidi ya nusu ya mauaji hayo yalikuwa katika maeneo ya Jenin, Tulkarm na Nablus. “Maeneo haya yameshuhudia ongezeko la operesheni kubwa za kijeshi katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, na kuashiria mabadiliko katika kiwango na upeo,” UNICEF ilieleza.
“Mvutano unaoongezeka katika Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na Jerusalem Mashariki, pia unaathiri ustawi wa kimwili na kiakili wa maelfu ya watoto na familia, ambazo sasa zinaishi kwa hofu kila siku ya maisha yao. Watoto wanaripoti kuogopa kutembea katika vitongoji vyao, au kusafiri kwenda shuleni.”
Kabla ya tarehe 7 Oktoba 2023, watoto katika Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na Jerusalem Mashariki, tayari walikuwa wanakabiliwa na viwango vya juu vya ukatili katika kipindi cha miaka 20, huku watoto 41 wa Kipalestina na watoto sita wa Israeli waliuawa katika miezi tisa ya kwanza ya mwaka jana. Pia wameathiriwa pakubwa na vizuizi vya harakati na ufikiaji ambavyo vilitatiza maisha yao ya kila siku.
UNICEF imetoa wito mpya kwa wahusika kukomesha mara moja na kuzuia ukiukwaji mkubwa zaidi dhidi ya watoto, ikiwa ni pamoja na mauaji na ulemavu wa watoto.
Makundi yote yanayohusika katika mzozo lazima wazingatie wajibu wao chini ya sheria za kimataifa za kulinda watoto. Haki ya watoto ya kuishi lazima itunzwe na watoto hawapaswi kamwe kuwa walengwa wa unyanyasaji, bila kujali ni nani au wapi.
“Gharama ya kweli ya mzozo unaoendelea kati ya Palestina na Israeli itapimwa katika maisha ya watoto-waliopoteza maisha na wale ambao maisha yao wamebadilika milele,” alisema Bi Russell. “Watoto wanachohitaji sana ni kukomeshwa kwa ghasia na suluhu ya kudumu ya kisiasa kwa mgogoro huo, ili waweze kufikia uwezo wao kamili katika amani na usalama.”