Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Licha ya juhudi, mapengo yanaendelea kuwa mwiba wa kutokomeza ukimwi kwa watoto ifikapo 2030: UNAIDS

Mandisa Dukashe, mumewe, na binti zao wawili wakionyesha ishara zinazoonyesha hali yao ya VVU wakiwa nje.
AFP PHOTO/MUJAHID SAFODIEN Mandisa Dukashe na familia yake ni wakazi wa Eastern Cape, Afrika Kusini. Mandisa ni muuguzi na anahusika na udhibiti wa VVU na yeye mwenyewe anaishi na VVU. Lakini mumewe na binti zake wamepima VVU na hawana virusi hivyo.

Licha ya juhudi, mapengo yanaendelea kuwa mwiba wa kutokomeza ukimwi kwa watoto ifikapo 2030: UNAIDS

Afya

Ripoti mpya iliyotolewa leo kwa pamoja na shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na ukimwi UNAIDS na muungano  wa kimataifa wa kutokomeza ukimwi unaojumuisha mashirika mbalimbali, inaonyesha kwamba dunia iko katika wakati muhimu wa kubaini endapo viongozi wa dunia watatimiza  ahadi zao  za  kumaliza janga la ukimwi kama tishio la afya ya umma  ifikapo mwaka 2030. 

Ripoti hiyo, iliyotolewa mjini Geneva na Munich inasisitiza uharaka wa kuchukua hatua kwani ukimwi uko  njiapanda na inatanabaiisha, takwimu mpya na tafiti zinazoonyesha kwamba maamuzi na uchaguzi wa sera vinahitajika sasa.

Inasema utoaji wa haraka wa huduma za VVU pekee ndio utakaotimiza ahadi ya kukomesha UKIMWI kwa watoto ifikapo 2030.

Ripoti hiyoKubadili maono kuwa hali halisi” inaonyesha kwamba janga la Ukimwi linaweza kumalizika ifikapo 2030, endapo viongozi wa dunia wataongeza rasilimali na kulinda haki za binadamu hivi sasa.

Kwani inaonyesha kuwa programu maalum zinazolenga maambukizi ya VVU zimesaidia kuepusha maambukizi milioni 4 miongoni mwa watoto wenye umri wa miaka 0-14 tangu mwaka 2000.

Ulimwenguni kote, maambukizi mapya ya VVU miongoni mwa watoto wenye umri wa miaka 0-14 yamepungua kwa asilimia 38 tangu mwaka 2015 na vifo vimepungua kwa asilimia 43.

Mkono wa mtu mzima umekaa begani mwa mvulana mdogo wa Msumbiji, huku mkono mwingine ukimgusa usoni kwa upole.
UN News Anísio, ambaye alizaliwa na VVU, ana matatizo na matibabu kwa sababu anaugua utapiamlo kutokana na ukosefu wahana lishe bora

Tunaweza kutokomeza ukimwi ifikapo 2030

Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS, Winnie Byanyima amesema "Ninapongeza maendeleo ambayo mataifa mengi yanapata katika kusambaza huduma za VVU ili kuwapa afya bora  wanawake vijana na kuwalinda watoto wachanga na watoto wengine dhidi ya VVU. Kwa dawa na sayansi zilizopo leo, tunaweza kuhakikisha kuwa watoto wote wanazaliwa na kuishi bila VVU, na kwamba watoto wote wanaoishi na VVU wanapata huduma na kusalia kwenye matibabu. Huduma za matibabu na kinga lazima ziongezeke mara moja ili kuhakikisha kuwa zinawafikia watoto wote kila mahali. “

Ameongeza kuwa  Hatuwezi kupumzika kwani kifo cha mtoto yeyote kutokana na sababu zinazohusiana na UKIMWI sio tu janga, lakini pia hasira. Ninakotoka, watoto wote ni watoto wetu. Ulimwengu unaweza na lazima utimize ahadi yake ya kukomesha UKIMWI kwa watoto ifikapo 2030.”

Miongoni mwa nchi 12 za muungano wa kimataifa wa kutokomeza ukimwi, kadhaa zimefanikisha upatikanaji wa matibabu ya kudumu ya dawa za kuongeza mud awa kuishi miongoni mwa wanawake wajawazito na wanaonyonyesha wanaoishi na VVU, huku Uganda ikikaribia asilimia 100, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 98, na Afrika Kusini kwa asilimia 97, Msumbiji imefikia asilimia 90, Zambia asilimia 90, Angola na Kenya kwa asilimia 89, Zimbabwe kwa asilimia 88, na Cote d'Ivoire kwa asilimia 84.

Mwanamke mjamzito anashikilia chupa ya dawa, mkono wake mwingine ukikaa kwenye tumbo lake, dhidi ya ukuta wenye rangi nyekundu.
© UNICEF/UN0640796/Dejongh Mwanamke mjamzito mwenye umri wa miaka ishirini aliyezaliwa na virusi vya Ukimwi, hutumia dawa kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Jitihada za kukomesha ukimwi zinajikokota

Kwa mujibu wa ripoti nchi za Muungano wa Kimataifa zinatumia ubunifu ili kuondokana na vikwazo na kuharakisha maendeleo kuelekea kukomesha UKIMWI kwa watoto.

Hata hivyo, pamoja na maendeleo si dunia wala nchi za muungano huo ambazo kwa sasa ziko kwenye njia ya kufikia ahadi zinazohusiana na VVU kwa watoto na vijana na kasi ya maendeleo katika kuzuia maambukizi mapya ya VVU na vifo vinavyotokana na UKIMWI miongoni mwa watoto imepungua katika miaka ya hivi karibuni.

Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani  WHO, amesema "Kuharakisha utoaji na matumizi ya huduma za VVU kwa watoto na vijana ni wajibu wa kimaadili, na chaguo la kisiasa. Nchi 12 zinaonyesha kuwa zimefanya chaguo hilo, lakini changamoto kubwa zimesalia. Wakati tumepiga hatua katika kuongeza upatikanaji wa huduma kwa wanawake wajawazito kupima na kupata matibabu ili kuzuia maambukizi ya VVU, bado tuko mbali kattika kuziba pengo la matibabu ya watoto. Tunahitaji kuimarisha zaidi ushirikiano na kufikia Muungano wa Kimataifa, na ni lazima tufanye kazi hii kwa umakini, madhumuni na mshikamano na akina mama, watoto na vijana wote walioathirika.”

Takriban watoto 120,000 wenye umri wa miaka 0-14 waliambukizwa VVU mwaka 2023, huku takriban 77,000 kati ya maambukizo haya mapya yakitokea katika nchi za Muunganowa kimataifa.

Vifo vinavyotokana na UKIMWI miongoni mwa watoto wenye umri wa miaka 0-14 vilifikia 76,000 duniani kote huku nchi za Muungano wa kimataifa zikiwa na 49,000 kati ya vifo hivi visivyo vya lazima. Viwango vya maambukizi vimesalia kuwa juu sana katika baadhi ya maeneo, hasa Afrika Magharibi na Kati, huku viwango vinavyozidi asiilimia 20 katika nchi zikiwemo Nigeria na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Mkono wenye glavu unamshika mgonjwa kidole huku mkono mwingine wenye glavu ukitumia kipande cha kipimo cha haraka cha uchunguzi ili kuchambua sampuli ya damu.
UNICEF/Frank Dejongh Kijana barubaru akifanyiwa vipimo vya Virusi vya UKIMWI huko nchini Ivory Coast

Lazima tufanye kazi nzuri kuwalinda watoto

"Katika mapambano dhidi ya VVU, ni lazima tufanye kazi bora zaidi kwa watoto," almesema Peter Sands, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Kimataifa wa Kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria, Global Fund ambao unatoa ufadhili wa programu za VVU katika zaidi ya nchi 100.

Ameongeza kuwa "Katika kuunga mkono programu za kitaifa, tumekuwa tukinunua dawa za karibuni kabisa za dolutegravir za matibabu ya watoto kwa bei za majadiliano. Uwekezaji wetu katika mifumo ya maabara unasaidia kuhakikisha watoto wachanga walio katika hatari ya kuambukizwa wanapimwa kwa haraka na kwamba wale ambao wameambukizwa wanaanzishwa haraka katika matibabu ya kurefusha maisha yanayolingana na umri. Mbinu tofauti za upimaji na matibabu zinasaidia kuziba pengo la uchunguzi na kuhakikisha utoaji wa huduma unaomlenga mtoto zaidi.”

Ripoti inasema itatia hofu kwamna pengo la matibabu kati ya watu wazima na watoto linaendelea kuongezeka.

"Asilimia 57 pekee ya watoto wanaoishi na VVU ndio wanapata matibabu ya kuokoa maisha, ikilinganishwa na asilimia 77 ya watu wazima," amesema Mkurugenzi Msaidizi wa Msaidizi wa shirika  la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF kuhusu masuala ya  HIV/AIDS, Anurita Bains.

Ameendelea kusema kwamba “Bila ya kupima na kutibu mapema na kwa ufanisi, VVU bado ni tishio la kudumu kwa afya na ustawi wa watoto na vijana na kuwaweka katika hatari ya kifo. Ili kuziba pengo la matibabu, lazima tuunge mkono serikali kuongeza mbinu bunifu za upimaji na kuhakikisha watoto na vijana wanaoishi na VVU wanapata matibabu na usaidizi wanaohitaji."

Mwaka 2023, kulikuwa na maambukizi mapya 210,000 duniani kote miongoni mwa wanawake vijana na wasichana wenye umri wa miaka 15-24.

130 000 katika nchi za Global Alliance, mara nne zaidi ya lengo la 2025 lililowekwa la 50 000. Kuzuia maambukizi mapya kati ya kundi hili la umri ni muhimu kulinda afya na ustawi wa wanawake vijana na kupunguza hatari ya maambukizi mapya miongoni mwa watoto.

Baba mwenye VVU Nathan Lutaaya akimshikilia mtoto wake huku akisubiri pamoja na wazazi wengine kwa ajili ya kipindi cha elimu ya afya katika Kituo cha Afya cha Namwendwa IV huko Kamuli, Uganda, kikiongozwa na mama mshauri Sarah Nabirye.
© UNICEF/Jimmy Adriko Wazazi wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi, vvu wakiwa katika kliniki yao ya kuwapatia usaidizi wilayani Kamuli nchini Uganda.

Pengo la usawa wa kijinsi na haki za binadamu ni mwiba

Kwa mujibu wa ripoti hiyo kukosekana kwa usawa wa kijinsia na ukiukaji wa haki za binadamu kunaongeza uwezekano wa wanawake kuambukizwa VVU na kupunguza uwezo wao wa kupata huduma muhimu.

Ulimwenguni kote inasema ripoti karibu mwanamke mmoja kati ya watatu wamekumbana na aina fulani ya unyanyasaji wakati wa maisha yao, huku wasichana balehe na wanawake vijana wakiathiriwa kupita kiasi na unyanyasaji kutoka kwa wapenzi wa karibu.

Katika nchi nne za Muungano wa kimataifa ambazo takwimu zake zipo, nchi hizo haziko kwenye msitari unaostahili kwa sasa wa kufikia lengo la kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2025 chini ya asilimia 10 ya wanawake, watu muhimu na wanaoishi na VVU ndio pekee wanaokabiliwa na pengo la usawa wa kijinsia na unyanyasaji wa kijinsia.

Kundi la wanawake wakishiriki katika mkutano wa ICW wa UNAIDS nchini Nigeria, wakiwa wameketi na kusimama kuzunguka meza ya mkutano mbele ya mabango ya uhamasishaji.
UNAIDS Nigeria Wanachama wa chama cha kimataifa cha wanawake wanaoishi na UKIMWI, ICW nchini Nigeria wakiwa kwenye mkutano wao ambako hupeana matumaini na kujiamini. Kulia ni Assumpta Reginald, Mratibu wa ICW Kanda ya Afrika Magharibi.

Muungano wa kimataifa kukomesha ukimwi kwa watoto

Muungano wa Kimataifa wa Kukomesha UKIMWI kwa Watoto ifikapo mwaka 2030 ulizinduliwa mwaka 2022 na WHO, UNICEF na UNAIDS ili kuimarisha ajenda ya VVU kwa watoto.

Hivi sasa muungano huo umekua, na pamoja na mashirika ya Umoja wa Mataifa, unajumuisha vuguvugu la asasi za kiraia, ikiwa ni pamoja na Mtandao wa Kimataifa wa Watu wanaoishi na VVU, serikali za kitaifa katika nchi zilizoathirika zaidi, na washirika wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na PEPFAR na Mfuko wa Kimataifa Global Fund.

Nchi kumi na mbili ni wanachama: Angola, Cameroon, Côte d'Ivoire, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Kenya, Msumbiji, Nigeria, Afrika Kusini, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Uganda, Zambia, na Zimbabwe.