Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua zahitajika CAR kushughulikia ukiukwaji wa haki za binadamu mahabusu: UN

Ziara katika gereza la Ngaragba  mjini Bangui  CAR wakati  wa COVID-19
MINUSCA
Ziara katika gereza la Ngaragba mjini Bangui CAR wakati wa COVID-19

Hatua zahitajika CAR kushughulikia ukiukwaji wa haki za binadamu mahabusu: UN

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Hatua za haraka na madhubuti zinahitajika ili kuhakikisha kuheshimiwa kwa haki za binadamu katika vituo vya rumbande nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, ambako mateso na unyanyasaji, kukamatwa na kuwekwa kizuizini kinyume cha sheria na kiholela, utapiamlo na huduma duni za afya vimeenea, kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo na Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kuleta Utulivu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati MINUSCA).

Kwa mujibu wa ripoti hiyo maelfu ya watu kwa sasa wanazuiliwa katika mahabusu zizlizo na msongamano wa watu nchini kote, huku kukiwa na upungufu mkubwa wa chakula, maji, usafi wa mazingira na huduma za kimsingi za afya.

Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk amesema "Matokeo ya ripoti hii yanatia wasiwasi na yanahitaji hatua za haraka na madhubuti kutoka kwa mamlaka ya kitaifa. Mageuzi yanayoendelea katika mfumo wa jela yanatoa fursa muhimu kwa CAR kushughulikia ukiukwaji huu wa haki za binadamu.”

Ripoti hiyo ambayo ilikabidhiwa pia kwa serikali kwa ajili ya maoni yake, inahusu kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba 2023, na imeorodhesha kasoro mbalimbali ambazo ni pamoja na kushindwa kuzingatia ukomo wa muda wa kisheria wa kukaa chini ya ulinzi wa polisi, kukimbilia mahabusu kabla ya kesi na mazingira duni kizuizini, pamoja na changamoto zinazokabili mfumo wa mahakama.

Pia inaangazia maeneo muhimu yanayopaswa kufanyiwa kazi na mamlaka ya nchi hiyo.

Eneo la kunawa mikono katika gereza la Ngaragba CAR
MINUSCA
Eneo la kunawa mikono katika gereza la Ngaragba CAR

Kamatakama ya kinyume cha sheria

Ripoti pia inaeleza kwa kina mfano wa kukamatwa na kuzuiliwa kinyume cha sheria na kiholela unaofanywa na jeshi na vikosi vya usalama nchini CAR, huku zaidi ya watu 1,500 wakifanyiwa vitendo hivyo mwaka wa 2023.

Zaidi ya hayo, hadi mwisho wa 2023, wafungwa 1,749 walikuwa wakisubiri kesi zao gerezani, baadhi yao wamekuwa wkisubiri kwa karibu miaka sita.

Pia inaangazia wasiwasi kwamba maagizo ya watu kuwekwa kizuizini yalikuwa yanatolewa bila uchunguzi wa kutosha ikiwa kuzuiliwa kwa mtu anayehusika kulikuwa muhimu kulingana na kosa analodaiwa kufanya.

Utapiamlo, ukosefu wa huduma bora za afya na hali duni za usafi zimesababisha milipuko ya magonjwa katika magereza, inasema ripoti hiyo, ikitoa wito wa rasilimali za kutosha kutoa mahitaji muhimu ya wafungwa.

Ripoti hiyo zaidi inatoa wito kwa mamlaka kutii kikamilifu vikwazo vya muda vya kisheria vinavyoweka watu kizuizini, na inatathimini kwamba kuwekwa kizuizini kabla ya kesi kinapaswa kubaki kuwa hatua ya kipekee, inayohalalishwa na ulazima na kulingana na hali.

Watu wakijiandaa kutembelea ndugu zao katika gereza la Ngaragba mjini Bangui
MINUSCA

Serikali ifanye uchunguzi huru

Türk ametoa wito kwa mamlaka kufanya uchunguzi wa haraka na huru katika visa vyote vya utesaji na unyanyasaji, na kuwawajibisha wale waliohusika. Amewataka washirika wote kuunga mkono serikali ili kuboresha mazingira katika maeneo ya mahabusu.

Kamishna Mkuu  huyo wa haki za binadamu na Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu na Mkuu wa MINUSCA, Valentine Rugwabiza, wanatambua juhudi za Serikali za kutatua changamoto za haki za binadamu zinazohusishwa na watu kuwekwa kizuizini ikiwa ni pamoja na kufanya vikao vya mahakama ya uhalifu mara kwa mara, kukarabati na kufungua tena magereza matatu mwaka wa 2023, na kuajiri maafisa magereza zaidi.

Maafisa hao wa Umoja wa Mataifa wameahidi kuendelea uungaji mkono wa Umoja wa Mataifa kwa Serikali ili kuimarisha heshima ya haki za binadamu na utawala wa sheria nchini CAR, ikiwa ni pamoja na katika maeneo yamahabusu.