Polisi wa Sudan Kusini wanolewa na UNMISS
Polisi wa Sudan Kusini wanolewa na UNMISS
Maafisa wa polisi wanaohudumu chini ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS wametoa mafunzo kwa askari polisi wa nchi hiyo ili waweze kuimarisha ulinzi na usalama wakati huo huo wakiheshimu haki za binadamu.
Nchi ya Sudan Kusini inakabiliwa na kuongezeka kwa mfumuko wa bei huku ajira nazo zikiwa ngumu kupatikana hali hizi mbaya zimechocheea uhalifu. Jeshi la polisi limejikuta kwenye shinikizo kubwa la kushughulikia changamoto hizo wakati wakiwa na rasilimali chache wakati huo huo wakienda miezi kadhaa bila ya kulipwa mishahara.
Pamoja na changamoto hizo bado wanawajibu wa kulinda raia na mali zao ndio maana polisi wa UNMISS wakaandaaa mafunzo ya vitendo katika makao makuu ya nchi hiyo jijini Juba yakihusu matumizi sahihi ya nguvu wanapokamata wahalifu, namna ya kuwasaka watuhumiwa kwa usalama, ulinzi usio na silaha, huduma ya kwanza, ulinzi wa viongozi na watu mashuhuri, usalama wa misafara ya magari, doria ndani ya jamii na kufanya uchunguzi.
Sophia Ennim ni Afisa Polisi wa Umoja wa Mataifa chini ya UNMISS na anasema mafunzo hayo yatasaidia sio tu kupambana na wahalifu bali pia wakati wa uchaguzi wa kwanza ya nchi hiyo unaotarajiwa kufanyika mwezi Desemba mwaka huu, “Tunataka kubadilishana nao uzoefu na tena, tunajua wanajitayarisha kuelekea uchaguzi na tunafikiri wakati huu ndio bora kwao kujikumbusha upya mbinu zao za kipolisi.”
Samuel Nai, ni mmoja wa maafisa wa Polisi wa Sudan Kusini aliyehitimu mafunzo hayo. Anasema “Kazi hii ya upolisi inachosha sana, inachangamoto sana, lakini uzoefu tulioupata hapa utatusaidia kufanya vyema zaidi katika siku zijazo. Haya ndiyo mabadiliko tunayotaka kutoka kwa polisi.”
Mbali na kushukuru kwa mafunzo hayo Afisa wa polisi wa Suda Kusini Lilian Poni ambaye anatumikia polisi kwa miaka 19 ametoa wito kwa wanawake zaidi kupata fursa sawa ili kukuza zaidi taaluma zao.
“Nikiwa nimekaa hapa, naona wanaume ni wengi wanawake ni wachache. Kwa hivyo angalau wanapaswa kuweka usawa wa kijinsia, ikiwa wanaume ni 10, wanawake wanapaswa kuwa 10 pia.”
Mafunzo haya kwa jeshi la polisi yanafuatia kikao cha usimamizi wa utulivu wa umma ambacho kiliomba askari wapatiwe mafunzo ili kusaidia kuhakikisha kuwa uchaguzi mkuu wa nchi hiyo unafanyika kwa njia huru, ya haki, ya kuaminika na ya amani.
UNMISS wameeleza kuwa pamoja na changamoto za ulinzi na usalama na taifa hilo kujiandaaa na uchaguzi lakini mafunzo yanayoendeshwa nao yana lengo kuu la kujenga uwezo wa maafisa wa polisi wa Sudan Kusini kukidhi mahitaji ya jamii zao.