Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO Tanzania yasaidia kupunguza vifo vya wajawazito wakati wa kujifungua

WHO Tanzania kupitia huduma za dharura za afya yasaidia kupunguza vifo vya wajawazito wakati wa kujifungua.
WHO
WHO Tanzania kupitia huduma za dharura za afya yasaidia kupunguza vifo vya wajawazito wakati wa kujifungua.

WHO Tanzania yasaidia kupunguza vifo vya wajawazito wakati wa kujifungua

Afya

Hakuna mwanamke anayepaswa kufa wakati wa kujifungua, ndio maana Shirika la Umoja wa Mataifa la afya Ulimwenguni WHO nchini Tanzania baada ya kushuhudia ongezeko la vifo vya wajawazito kutokana na wajawazito kupata ugumu kuvifikia vituo vya afya ilitafuta fedha ya kusaidia kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo miundombinu na kuongeza maarifa kwa wataalamu wa afya.

Dorcas Simon, mkazi wa mkoani Kigoma ulio kwenye mwambao wa kaskazini mashariki mwa Ziwa Tanganyika na karibu na mpaka wa nchi ya Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo anaeleza changamoto alizokumbana nazo wakati wa kijifungua huku akiwa mbali na kituo cha afya. 

Anasema, “Mimi nina watoto watatu, wa kwanza nilijifungulia nyumbani na wapili pia nikajifungulia nyumbani. Huyu mtoto wa tatu nilipojifungulia nyumbani pia alikuwa na changamoto mbalimbali, uzito wake ulikuwa mdogo, ilituchukua saa tatu kufika katika kituo cha afya mimi na familia yangu tukawa na wasiwasi ningempoteza mtoto wangu wa kiume.”

Soundcloud

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Jesca Leba anaeleza takwimu za vifo vya wajawazito wakati wa kujifungua.“Ukianza mwaka 2020 tulikuwa na vifo 119 vya wajawazito, mwaka 2021 vifo hivyo vilipungua na kufikia 75. Mwaka 2022 viliongezeka na kufikia 102”

Serikali ya Tanzania wakishirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO nchini humo na wadau wengine wakavalia njuga suala hilo na kutaka kumaliza kabisa vifo vya wajawazito wakati wa kujifungua. WHO ilipata fedha kutoka ubalozi wa Norway na kununua magari ya kubeba wagonjwa ili iwe rahisi kusafirisha wajawazito.

Magari hayo ya kubeba wagonjwa yamefanikisha kuwasafirisha wajawazito zaidi ya 2000 kutoka wilaya mbalimbali za mkoa huo wa Kigoma.

WHO Tanzania yasaidia kupunguza vifo vya wajawazito wakati wa kujifungua

Dorcas Simon ni mnufaika wa usafiri huo “Lisingekuwa gari la kubeba wagonjwa sijui kitu gani kingetokea kwangu mimi na kwa mtoto. Kwa sasa hivi mtoto yupo salama na mimi nipo salama.”

WHO Tanzania pia walinunua vifaa tiba na kutoa mafunzo kwa watoa huduma ya afya zaidi ya 300 kama anavyoeleza afisa afya ya umma wa WHO Tanzania Dkt. Jairos Hiliza “Hapo awali mkoa ulikuwa na uwezo mdogo katika mfumo wake wa rufaa na uwezo wa uchunguzi. WHO ilifanikiwa kupata pesa kutoka kwa Ubalozi wa Norway. Tulifanikiwa kununua vifaa vya uchunguzi kama vile Ultrasound na tukaendesha mafunzo ya ukuzaji ujuzi ili kutoa huduma ya dharura ya uzazi mkoani Kigoma.”

Dkt.Baraka Kemero anaeleza manufaa waliyoanza kuyaona. “Tangu ultrasound imeletwa hapa hata rufaa zimepungua kwa ajili ya kwenda kutafuta ultrasound na kuongeza wigo wa sisi kutoa huduma.”

Ama hakika kazi kubwa imefanyika kutoka vifo 112 mwaka 2020 na kupungua mpaka kufikia vifo 26 mwaka huu 2024 kati ya wanawake 100,000 wanaojifungua.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Jesca Leba anaeleza matumaini yake“Kwa sasa tunaona vifo vinaenda kupungua kwa mama na mtoto na mikakati na jitihada mbalimbali ambazo zimefanyika tunaamini hizi namba zitashuka. Tunawashukuru sana wadau wetu wa WHO ambao wamefanya kazi kubwa sana tumeona hata ile kujifungulia nyumbani inapungua kabisa na inaenda kuisha na kufikia sifuri.”