Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wananchi Terekeka Sudan Kusini wanufaika na mradi wa FAO kwa sekta ya uvuvi

Nyumba ya familia huko Terekeka, Sudan Kusini, jamii zinazotegemea uvuvi kujipatia riziki na mlo wa siku..
Picha: FAO/Albert González Farran
Nyumba ya familia huko Terekeka, Sudan Kusini, jamii zinazotegemea uvuvi kujipatia riziki na mlo wa siku..

Wananchi Terekeka Sudan Kusini wanufaika na mradi wa FAO kwa sekta ya uvuvi

Ukuaji wa Kiuchumi

Wananchi katika Kaunti ya Terekeka nchini Sudan Kusini wameeleza kufurahishwa na mafanikio wanayoyapata kutokana na mradi wa miaka mitano wa kuboresha mnepo wa Jamii za Wavuvi (FICREP). 

Huyo ni Stelle Clement, mjasiriamali wa mghahawa katika jamii ya Terekeka, Equatoria ya Kati nchini Sudan Kusini. Anasema, “faida ninayopata kutokana na biashara yangu ni tegemeo la familia yangu. Inaniwezesha kuwaandalia watoto wangu mahitaji, kuweka chakula mezani, na kuhakikisha wanapata matibabu yanapohitajika.”

Stelle Clement ni mmoja wa wanufaika wa mradi huu wa uvuvi ambao umeiinua sana jamii ya hapa kupitia ufadhili wa dola za Kimarekani milioni tano kutoka Ufalme wa Uholanzi ikiwa ni moja ya njia za kushughulikia baadhi ya changamoto kuu za janga la tabianchi.

Samaki ndiyo bidhaa pekee ya kilimo ambayo inasafirishwa mara kwa mara kutoka Sudan Kusini kwenda nje ya nchi, na inazalisha takribani dola milioni 30 kwa mwaka.

Miongoni mwa malengo mengine, mradi umeunda vikundi 20 vya wavuvi na, kwa mara ya kwanza, mradi umeanzisha kituo bora cha kuunda mitumbwi kwa ajili ya vijana.

Yametolewa mafunzo kwa watengeneza mitumbwi 40 chipukizi ili kuunda mitumbwi ya kienyeji lakini sasa kwa kutumia gundi imara zaidi ili kuiewezesha mitumbwi hii kudumu kwa muda mrefu na pia kukarabatiwa kirahisi.

Demissie Redeat Habteselassie, Afisa Uvuvi wa FAO nchini Sudan Kusini anaeleza zaidi akisema, “Tumeboresha tanuri za kukaushia samaki, tumeboresha chanja za kukaushia samaki, na hii imesaidia jamii za wavuvi kupata mapato zaidi, kupunguza hasara zao na kuongeza mapato yao kupitia bidhaa za samaki zilizoongezwa thamani. Na hapa, kwa kawaida, jamii za wavuvi zinategemea zaidi samaki na uwezo wao wa kuzalisha na kuongeza faida yao ni muhimu sana. Kwa hiyo, hilo ndilo mradi wetu kimsingi unafanyia kazi.”

Uchumi wa Sudan Kusini unategemea zaidi mafuta, yakichangia takriban asilimia 95 ya mauzo ya nje na ni kichocheo kikuu cha mapato ya serikali.

Hata hivyo, nchi inakabiliwa na ukuaji tete wa uchumi huku mfumuko wa bei ukisukuma takriban watu milioni 1.6, au takriban asilimia 12 ya watu wote, kuwa hatarini na hivyo njia mbadala za kujipatia kipato ni muhimu.