Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama: Majeruhi waongezeka Ukraine huku mashambulizi ya Urusi yakitamalaki

Matokeo ya shambulio la kombora katikati mwa Kiev.
© UNICEF/Ukraine
Matokeo ya shambulio la kombora katikati mwa Kiev.

Baraza la Usalama: Majeruhi waongezeka Ukraine huku mashambulizi ya Urusi yakitamalaki

Amani na Usalama

Afisa wangazi ya juu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu amerejea kulaani vikali mashambulizi mabaya ya makombora katika miji mingi nchini Ukraine yaliyofanyik jn Jumatatu, wakati daktari mkuu kutoka hospitali kuu ya watoto iliyoathirika akielezea kwa Baraza la Usalama hali ya kuzimu inainayowaghubika wagonjwa na wahudumu wa afya baada ya kutokea.

Hospitali mbili kuu za kibingwa za watoto na wanawake nchini Ukraine ziliharibiwa kwa kiasi kikubwa pamoja na miundombinu muhimu ya nishati, wakatiwashambulio hilo lililoripotiwa kuua makumi ya raia, wakiwemo watoto, na kujeruhi zaidi ya watu 110.

Joyce Msuya, Kaimu Mratibu wa Misaada ya kibindmu na masuala ya dharura wa Umoja wa Mataifa, amewaambia wajumbe wa Baraza la Usalama kwamba Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR) inahakiki takwimu hizo, huku wafanyakazi wa uokoaji, wahudumu wa hospitali na wahudumu wa kujitolea wakiendelea kuzoa vifusi kuwasaka walionaswa chini ya ardhi na chini ya uchafu.

Ameongeza kuwa "Moyo wangu unawaendea wale wote walioathirika," akisisitiza kwamba hospitali zina ulinzi maalum chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu.

Hivyo amesema "Kuelekeza mashambulizi kwa makusudi dhidi ya hospitali inayolindwa ni uhalifu wa kivita, na wahusika lazima wawajibishwe."

Mashambulizi ya kimfumo

Bi. Msuya amebainisha zaidi kuwa matukio ya hivi karibuni yalikuwa sehemu ya "mtindo wa kina wa mashambulizi ya kimfumo yanayodhuru afya na miundombinu mingine ya kiraia kote Ukraine. Na mashambulizi yameongezeka tangu masika ya 2024," alisema.

Kufikia tarehe 30 Juni, kabla ya wimbi la hivi karibuni la mashambulizi ya makombora, OHCHR imethibitisha vifo vya raia 11,284 na wengine 22,594 waliojeruhiwa kutokana na vita ilivyoanza na uvamizi wa Urusi Februari 2022.

Zaidi ya hayo, Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa WHO, limethibitisha mashambulizi 1,878 yanayoathiri vituo vya huduma za afya, wafanyakazi, usafiri, vifaa na wagonjwa.

Kando na uharibifu wa shule, nyumba na miundombinu muhimu ya kiraia, "matokeo ya hali ya kibinadamu nchini Ukraine, bila shaka, ni makubwa," amesisitiza Bi. Msuya.

Ufikiaji wa misaada ya kibinadamu

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kwamba shughuli za misaada zimeathiriwa na mashambulizi hayo, huku zaidi ya watu milioni 14.6, karibu asilimia 40 ya wakazi wa Ukraine wakihitaji aina fulani ya usaidizi wa kibinadamu.

Pia ameonyesha wasiwasi mkubwa juu ya upatikanaji wa fursa za ufikiaji wa kibinadamu kwa watu milioni 1.5 katika mikoa inayokaliwa na Urusi ya Donetsk, Kherson, Luhansk na Zaporizhzhia.

"Kama wengine wote wanaoishi karibu na mstari wa mbele wa vita nchini Ukraine, bila shaka wanahitaji upatikanaji wa haraka wa huduma za afya na dawa, chakula, na maji safi ya kunywa. Kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kibinadamu, ni muhimu kwamba misaada ya kibinadamu isiyo na upendeleo iwezeshwe kwa raia wote wanaohitaji,” amesema Bi. Msuya.

Joyce Msuya, Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu na Mratibu wa Misaada ya Dharura, akitoa taarifa ya mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu kudumisha amani na usalama wa kimataifa.
UN Photo/Eskinder Debebe
Joyce Msuya, Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu na Mratibu wa Misaada ya Dharura, akitoa taarifa ya mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu kudumisha amani na usalama wa kimataifa.

Rasilimali zinazohitajika

Bi. Msuya amesisitiza haja ya rasilimali zaidi ili kuendeleza shughuli za kibinadamu.

Amesema "Ili kuendeleza shughuli katika mazingira yanayozidi kuwa magumu na hatari, tunahitaji haraka wafadhili ili kuharakisha ufadhili wa hatua za  kibinadamu”.

Ameongeza kuwa "Hasa wakati msimu mwingine wa baridi unakaribia kukiwa hakuna dalili ya kupunguza uhasama au athari zao kwa raia na miundombinu ya kiraia."

Daktari ameelezea hali ya jehanamu inayoshuhudiwa

Volodymyr Zhovnir, daktari wa upasuaji wa moyo na utoaji wa dawa ya usingizi katika hospitali ya watoto, ameelezea tukio hilo kwa wajumbe wa Baraza la Usalama wakati kituo chao huko Kyiv kilipopigwa na kombora Jumatatu.

Kupitia njia ya video amesema "Saa 04:42 asubuhi tulihisi mlipuko wa nguvu, ardhi ikatikisika na kuta zikatetemeka, watoto na watu wazima walipiga mayowe na kulia kutokana na hofu na kujeruhiwa kutokana na maumivu...ilikuwa ni hali ya kuzimu kweli”.

Kulingana na duru za habari, watu wawili walikufa wakati sehemu ya Hospitali ya watoto ya Ohmatdyt ilipogongwa na kombora.

Amebainisha athari kubwa ya muda mrefu kwa watoto wa Ukraine wanaohitaji huduma ya matibabu ambao wamekumbwa katika mapigano, pamoja na athari za muda mrefu za kisaikolojia.

Bwana Zhovnir amesisitiza kwamba “kushambulia hospitali za watoto ambako wanatibiwa kansa na magonjwa mengine mabaya sio uhalifu wa kivita tu, ni mbali zaidi ya kikomo cha ubinadamu".

Urusi: Magharibi wanajaribu kulinda serikali ya Kyiv

Balozi wa Urusi na Mwakilishi wa Kudumu kwenye Umoja wa Mataifa Vassily Nebenzia, ambaye ni Rais wa Baraza la Usalama kwa mwezi Julai, amezungumza katika wadhifa wake wa kitaifa.

Amesema ni wazi kutokana na taarifa za wenzake wa Magharibi kwamba "mada ya madai ya mashambulizi ya Urusi kwenye hospitali ya watoto ambayo ilipeleka kwenye mkutano wa dharura si mada ya kufurahisha sana."

Ameendelea kusema kuwa "Labda waliona uchambuzi mwingi wa kile kilichotokea kwenye picha na video, ambayo inafuata wazi kwamba hili lilikuwa kombora la jeshi la ulinzi wa anga la Ukraine”.

Akiongeza kuwa "Hapa unapata mazingaombwe ya mchezowa maneno yaliyoonyeshwa na wanachama wa Magharibi wa Baraza la Usalama, wakijaribu kwa kila njia kulinda serikali ya Kyiv".

Balozi Nebenzia amesema kuwa udanganyifu wa mbinu hii uko wazi kwa macho kama ilivyogunduliwa mara moja na Wayukreni wenyewe kupitia video ya shambulio hilo iliyoonekana kwenye mtandao.

Alisema mamlaka ya Ukraine ilijaribu kupotosha mtazamo kutoka kwenye tukio hilo ili "kuwavuruga raia kutoka kwenye uasi wa kila siku wa ufisadi wa Serikali".