Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalamu huru wa UN: Gaza imekumbwa na baa la njaa

Wakilazimika kuhama makazi yao kwa amri za Israel, Wapalestina huchukua mali nyingi wawezavyo, kabla ya kuelekea kutafuta mahali papya pa kujihifadhi.
UNRWA
Wakilazimika kuhama makazi yao kwa amri za Israel, Wapalestina huchukua mali nyingi wawezavyo, kabla ya kuelekea kutafuta mahali papya pa kujihifadhi.

Wataalamu huru wa UN: Gaza imekumbwa na baa la njaa

Amani na Usalama

Kundi la wataalamu huru wa Umoja wa Mataifa hii leo wamesema ni dhahiri shahiri kuwa baa la njaa imeenea katika ukanda mzima wa Gaza kufuatia vifo vya hivi karibuni vya watoto wa kipalestina kutokana na njaa na utapiamlo.

Katika taarifa yao iliyotolewa leo na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu jijini Geneva Uswisi kwa kauli moja wataalamu hao wamenukuliwa wakieleza kuwa “Tunatangaza kwamba kampeni ya makusudi ya Israel iliyolenga kuleta njaa kwa watu wa Palestina ni aina ya mauaji ya halaiki na imesababisha njaa katika eneo lote la Gaza. Tunatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuweka kipaumbele katika utoaji wa misaada ya kibinadamu kwa kutumia ardhi, kukomesha Israel kulizingira eneo la Gaza, na kusitisha mapigano.”

Wametaja baadhi ya watoto ambao wamekufa ambao ni Fayez Ataya aliyekuwa na umri wa miezi sita alikufa tarehe 30 Mei 2024 na Abdulqader Al-Serhi aliyekuwa na umri wa miaka 13 alikufa tarehe 1 Juni 2024 katika hospitali ya Al- Aqsa huko Deir Al-Balah. Mtoto Ahmed Abu Reida alikufa tarehe 3 Juni 2024 katika hema alipokuwa akipatiwa hifadhi yeye na familia yake huko Al- Mawasi, Khan Younis.

“Watoto wote hawa watatu walifariki kutokana na utapiamlo na ukosefu wa huduma za afya zinazofaa,” wamesema wataalam hao.

Wataalamu hao wameeleza kuwa kifo cha mtoto kutokana na utapiamlo na upungufu wa maji mwilini kinaashiria kuwa miundombinu ya afya na kijamii imeshambuliwa na kudhoofika sana. “Mtoto wa kwanza anapokufa kutokana na utapiamlo na upungufu wa maji mwilini, inakuwa jambo lisilopingika kwamba njaa imetawala,” wataalam walisema.

“Wakati mtoto wa miezi 2 na Yazan Al Kafarneh wa miaka 10 alipokufa kwasababu ya njaa tarehe 24 Februari na 4 Machi mtawalia, hii ilithibitisha kuwa njaa ilikuwa imepiga kambi huko kaskazini mwa Gaza. Ulimwengu wote ulipaswa kuingilia kati mapema kukomesha kampeni ya njaa ya mauaji ya kimbari inayotekelezwa na Israeli na kuzuia vifo hivi," wataalam walisema.

Wakilazimishwa kuhama makazi yao kwa amri za Israel, Wapalestina huchukua mali nyingi wawezavyo, kabla ya kuelekea kutafuta mahali papya pa kujihifadhi.
UNRWA
Wakilazimishwa kuhama makazi yao kwa amri za Israel, Wapalestina huchukua mali nyingi wawezavyo, kabla ya kuelekea kutafuta mahali papya pa kujihifadhi.

Wataalamu hao wamesema mpaka sasa wapalestina 34 wamekufa kutokana na utapiamlo tangu tarehe 7 Oktoba, wengi wao wakiwa ni watoto na kwamba kitendo cha kutochukua hatua ni kuonesha ushirikino na wanaosababisha madhila hayo kwa wananchi wa Gaza.

Wataalamu waliotoa taarifa hii ya pamoja ni: Michael Fakhri, Special Rapporteur on the right to food; Balakrishnan Rajagopal, Special Rapporteur on the right to adequate housing, Tlaleng Mofokeng, Special Rapporteur on the right of everyone to the enjoyment of the highest attainable standard of physical and mental health, Francesca Albanese, Special Rapporteur on the situation of human rights in the Palestinian Territory occupied since 1967; Pedro Arrojo-Agudo, Special Rapporteur on the human rights to safe drinking water and sanitation,  Paula Gaviria Betancur, Special Rapporteur on the human rights of internally displaced persons; George KatrougalosIndependent Expert on the promotion of a democratic and equitable international order;   Barbara G. Reynolds (Chair), Bina D’Costa, Dominique Day na Catherine NamakulaWorking Group of Experts on People of African Descent.