Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Volker Turk aonya kuhusu kuzuiliwa kiholela kwa wahamiaji na wakimbizi - Libya

Wahamiaji waliookolewa katika pwani ya Libya na NGO, SOS Méditerranée. (Maktaba)
© SOS Méditerranée/Anthony Jean
Wahamiaji waliookolewa katika pwani ya Libya na NGO, SOS Méditerranée. (Maktaba)

Volker Turk aonya kuhusu kuzuiliwa kiholela kwa wahamiaji na wakimbizi - Libya

Wahamiaji na Wakimbizi

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu Volker Türk ameitaka jumuiya ya kimataifa kusitisha makubaliano yake na Afrika Kaskazini juu ya wanaotafuta hifadhi na wahamiaji kutokana na hali inayoendelea ya kukata tamaa ya wahamiaji hao na wakimbizi kutokana na mateso nchini Libya.

Katika wito kwa mamlaka ya Libya wa kuchunguza uhalifu dhidi ya maelfu ya watu walio hatarini katika hatua hiyo, Turk asisitiza kugunduliwa kwa kaburi la halaiki mwezi machi kusini magharibi mwa Libya likiwa na miili ya watu 65 wanaodhaniwa kuwa ni waamiaji.

“Kama hii sio ya kutisha vya kutosha, tunafuatilia ripoti za kaburi jingine la umati lililogunduliwa hivi karibuni, katika eneo la jangwa kwenye mpaka wa Libya na Tunisia, wapendwa wale waliokufa wana kila haki ya kujua ukweli” alisema Volker Turk

Kamishna Mkuu pia alihimiza mapitio ya mpango wa muda mrefu kati ya Umoja wa Ulaya na mamlaka ya Libya yenye jukumu la kuwazuia wahamiaji wanaojaribu kuvuka Bahari ya Mediterania Kwenda Ulaya kutokana na hali ya hatari ambayo wahamiaji hao wanakumbana nayo wanapopitia katika njia hiyo, huku wataalamu huru wa haki za binadamu na mashirika ya kutoa misaada yanayohusika na utafutaji na uokoaji mara kwa mara yamekosoa utaratibu huo.

Katika muda wa miezi 12 tangu Aprili 2023, zaidi ya watu 2,400 walikufa au kutoweka wakati wakijaribu kuvuka bahari ya kati ya Mediterania, ambapo zaidi ya 1,300 waliondoka Libya.

Ni jambo lisiloeleweka kwamba watu wanaotafuta usalama na utu, wanateseka na kufa katika mazingira yasiyoelezeka, nakumbusha mataifa yote juu ya wajibu wa Pamoja chini ya sheria ya kimataifa kuokoa Maisha na kuzuia vifo baharini”

Kufuatia makadirio mapya kutoka Umoja wa Mataifa, wahamiaji hufa mara mbili zaidi  wanapojaribu kuvuka kupitia njia za ardhini kuliko wale wanaotumia njia za Bahari ya Mediterania huku matokeo ya wazi yanaonyesha kuongezeka kwa idadi ya watu wanaojaribu kuvuka Sahara, wakisukumwa na migogoro mipya huko Sahel na Sudan, mshtuko wa hali ya hewa na dharura za muda mrefu Mashariki na pembe ya Afrika huku kukiwa na hali tete ya kisiasa na mzozo ambao umeigawa nchi hiyo tangu kupinduliwa kwa Rais wa muda mrefu Muammar Gaddafi mwaka 2011.

Volker Turk amesema kurekebisha hali hiyo inayoendelea inawezekana huku akitoa wito wa mchakato wa mpito wa haki na upatanishi wa msingi unaozingatia haki na usuluhishi endelevu wa kisiasa.