Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

El Niño kutishia uhakika wa chakula Kusini mwa Afrika: WFP

Shamba la mahindi lililoharibiwa na ukame nchini Zambia, mojawapo ya nchi ambazo zimetangaza hali ya dharura huku likikabiliana na athari za El Niño.
© WFP/Nkole Mwape
Shamba la mahindi lililoharibiwa na ukame nchini Zambia, mojawapo ya nchi ambazo zimetangaza hali ya dharura huku likikabiliana na athari za El Niño.

El Niño kutishia uhakika wa chakula Kusini mwa Afrika: WFP

Tabianchi na mazingira

Mamilioni ya watu katika maeneo ya kusini mwa Afrika hawana uhakika wa chakula kufuatia ukame mkali  uliosababishwa na tukio kubwa la El Niño, kwa mujibu wa  ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP iliyotolewa leo mjini Geneva Uswisi.

Kwa mujibu washirika hilo akiba ya nafaka kwenye maghala miongoni mwa  familia kadhaa imeisha na bei ya mahindi, ambayo ndio mazao muhimu zaidi katika eneo hilo imepanda bei na hayapatikani kwa watu wengi. Hali hii inatarajiwa kuzorota, kutokana na upungufu wa uzalishaji na ugavi unaopungua.

Mabadiliko katika mifumo ya mvua na vipindi virefu vya ukame wakati wa msimu muhimu wa kupanda zimeiacha sehemu kubwa ya eneo hilo na mvua kidogo na joto la juu kuliko kawaida. 

Hii imesababisha kupotea kwa nusu ya uzalishaji wa mazao uliotarajiwa nchini Malawi na Zambia huku asilimia 80 ya mavuno yaliyotarajiwa nchini Zimbabwe yakiharibiwa.

Kufikia sasa Malawi, Namibia, Zambia, na Zimbabwe zimetangaza majanga ya kitaifa ya ukame na inatarajiwa nchi nyingine zitafuata, wakati uzito kamili wa mgogoro unavyojitokeza. 

Kufuatia wito wa serikali mabimbali kwa   WFP kutoa msaada moja kwa moja wa huduma za usafirishaji, vifaa vya usafirishaji na ununuzi wa chakula, WFP imesema inaongeza jitihada za kutoa msaada wa dharura wa chakula na lishe kwa watu milioni tano kati ya sasa na Machi 2025.

Hatua zinayoongozwa na serikali yatakidhi sehemu ya mahitaji, lakini ushirikiano kati ya washirika wa kibinadamu na wa maendeleo unahitajika ili kuokoa maisha.

Kwa upande wake WFP imesema inaunga mkono juhudi zilizofanywa na serikali mbalimbali katika kuendesha hatua za pamoja za kisekta, kwa kupanua mipango ya ulinzi wa kitaifa ilioko kwa msaada wa washirika.

WFP na washirika wake pia wamezindua hatua za mapema, kwa kutoa dola milioni 14 kwa ajili ya watu nusu milioni wa Lesotho, Madagascar, Zimbabwe na Zambia. Fedha hizi zimewezesha hatua za mapema za kuboresha vyanzo vya maji na kusambaza ujumbe wa tahadhari.

Mipango hii ya mapema, imesaidia watu walio hatarini kustahimili mshtuko huu, mbinu ambayo haikusaidia tu kuokoa na kuhifadhi maisha ya watu, lakini pia ina ufanisi wa gharama. Lakini, imefikia sehemu ndogo tu ya wale wanaohitaji msaada.