DRC: Ukuaji wa haraka wa M23 huko Kivu Kaskazini unatia wasiwasi, aonya Bintou Keita
DRC: Ukuaji wa haraka wa M23 huko Kivu Kaskazini unatia wasiwasi, aonya Bintou Keita
Hali ya usalama mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imeendelea kuzorota katika miezi ya hivi karibuni, na kufikia viwango vya kutisha vya ghasia na kuhama kwa raia, mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, Bintou Keita amewaeleza wajumbe wa Baraza la Usalama leo Jumatatu Julai 8 jijini New York, Marekani.
Amesema "anatiwa wasiwasi sana" na "upanukaji wa haraka" wa kundi la wapiganaji la Mouvement du 23 mars (M23) katika jimbo la Kivu Kaskazini na viunga vyake katika jimbo la Kivu Kusini, licha ya operesheni nyingi zinazofanywa na jeshi la DRC (FARDC), linaloungwa mkono mara kwa mara na MONUSCO na Ujumbe wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) nchini DRC (SAMIDRC).
"Katika muda wa wiki mbili zilizopita, M23 imeteka maeneo kadhaa ya kimkakati katika Kivu Kaskazini, ikiwa ni pamoja na mji wa Kanyabayonga, ambao uko katika maeneo ya Lubero na Rutshuru. Wakati wa mashambulizi yao ya hivi karibuni ya kijeshi, M23 na wafuasi wake walichoma kambi kadhaa za FARDC na kusababisha watu wapya kuhama makazi yao, na hivyo kuzidisha hali mbaya ya kibinadamu na haki za binadamu tayari.” Bi Keita amesisitiza.
Msaada wa Rwanda kwa M23
"Kama ilivyoandikwa na Jopo la Wataalamu, ambalo linaripoti kwa Kamati ya Vikwazo iliyoanzishwa na Baraza hili, Serikali ya Rwanda imeongeza uungaji mkono wake kwa M23, na kuiwezesha kupata mafanikio makubwa katika eneo la mashariki mwa DRC. Kuongezeka kwa kasi kwa mgogoro wa M23 kunabeba hatari ya kweli ya kusababisha mzozo mpana zaidi wa kikanda.” Ameongeza.
Mbali na kuongezeka kwa mgogoro wa M23, mfululizo wa mashambulizi ya ADF, Zaire na makundi yenye silaha ya CODECO katika jimbo la Ituri yamesababisha vifo vya takriban watu 300 katika miezi ya hivi karibuni, mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa ameeleza. Kusini zaidi, ADF pia imeingia mara kwa mara katika eneo la Lubero huko Kivu Kaskazini, na kuua idadi isiyokuwa ya kawaida ya raia.
Huko Kivu Kusini, mgogoro wa M23 pia umefikia eneo la Kalehe, huku mashambulizi yasiyo ya moja kwa moja yakipiga Minova na miji mingine ya karibu, na kuua na kujeruhi raia kadhaa na kuzalisha wakimbizi wapya.
Katika "muktadha huu tata", MONUSCO iliendelea kuunga mkono operesheni za kijeshi za FARDC.
"Operesheni za pamoja zimeweza kuchangia ulinzi wa raia, hasa kuhusiana na operesheni dhidi ya vikundi vya CODECO na Mai Mai huko Ituri. MONUSCO pia imetoa mafunzo kwa watu wapya 500 wa FARDC kama sehemu ya operesheni mpya ya pamoja ya FARDC-MONUSCO, iliyopewa jina la Northern Scalpel. Operesheni Springbok, katika kutetea Goma na Saké, imeendelea kukabiliana na operesheni za M23, na inaendelea,” akasema Bi Keita.
Kwa upande wake, SAMIDRC, inayojumuisha wanajeshi kutoka Afrika Kusini, Tanzania na Malawi, imeendelea na kazi yake na inatarajiwa kufikia uwezo kamili wa kufanya kazi ifikapo katikati ya mwezi huu wa Julai, amefafanua.
Janga kubwa la kibinadamu
Mkuu wa MONUSCO amekumbuka kwamba DRC inakabiliwa na "mojawapo ya majanga makubwa zaidi, magumu zaidi na yaliyopuuzwa ya kibinadamu ya wakati wetu."
Kuongezeka kwa ghasia mashariki kunaendelea kusababisha idadi kubwa ya watu kuyahama makazi yao, na kuzidisha hali mbaya ya kibinadamu ambayo tayari ilikuwepo. Kwa jumla, DRC sasa ina watu milioni 7.3 waliokimbia makazi yao, wakiwemo milioni 6.9 katika majimbo ya mashariki pekee.
Mwisho wa shughuli za MONUSCO katika Kivu Kusini
Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa amerudia kusema kuwa tarehe 25 Juni, yeye na Waziri Mkuu Judith Suminwa Tuluka waliongoza hafla ya kufunga operesheni za MONUSCO huko Kivu Kusini, na kuhitimisha zaidi ya miaka 20 ya operesheni katika jimbo hilo.
Kwa ombi la serikali ya Congo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliamua mnamo Desemba 2023 kuondoa kikosi cha MONUSCO kutoka Kivu Kusini katika mwaka huu wa 2024 kama sehemu ya kuondoka polepole kwa Ujumbe huo kutoka nchi hiyo. Kuanzia sasa, MONUSCO inaweka kikomo utekelezaji wa mamlaka yake kwa majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri.
"Sambamba na hilo, mchakato wa mpito unaendelea. Mchoro, yaani mpango wa mpito wa mkoa wa Kivu Kusini, ukiambatana na Mpango wa Msaada kutoka kwa timu ya Umoja wa Mataifa, umekamilika," ameongeza, akihamasisha Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa kuunga mkono mabadiliko haya, ikiwa ni pamoja na kifedha, ili mipango yote iende vizuri.
According to the UN envoy, in the context of the disengagement of MONUSCO and the transition, the Kulingana na mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa, katika muktadha wa kutoshirikishwa kwa MONUSCO na kipindi cha mpito, kuongeza kasi ya Mpango wa Kupokonya Silaha, Uondoaji, Uokoaji na Utulivu wa Jamii (P-DDRCS) "utahitaji dhamira kali kwa upande wa mamlaka ili kushawishi makundi yenye silaha ya hitaji la kupokonywa silaha, kuanzia majimbo ya Tanganyika, Kivu Kusini, Maniema na Ituri, na kusubiri mwisho wa mzozo wa Kivu Kaskazini, pamoja na kujitolea kwa muda mrefu kutoka kwa washirika wa kimataifa wa DRC."
Serikali mpya
Zaidi ya hali ilivyo mashariki mwa DRC, Bintou Keita ameeleza kuhusu kuundwa kwa serikali mpya ya Congo, iliyozinduliwa mwezi Juni, na uteuzi wa Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke katika historia ya nchi hiyo, Judith Suminwa Tuluka.
Bi. Keita amekaribisha hali hiyo Akieleza kuwa, “Serikali mpya inajumuisha, pamoja na Waziri Mkuu, wanawake 17 kati ya mawaziri 54, ambayo inawakilisha ongezeko la wazi kutoka asilimia 27 hadi 33 ya uwakilishi wa wanawake.”