Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miji kadhaa ya Ukraine yakumbwa na wimbi jipya la mashambulizi ya makombora ya Urusi

Shughuli za uokoaji katika eneo la shambulizi la asubuhi katika mji mkuu wa Ukraine, Kyiv.
UNOCHA/Viktoriia Andriievska
Shughuli za uokoaji katika eneo la shambulizi la asubuhi katika mji mkuu wa Ukraine, Kyiv.

Miji kadhaa ya Ukraine yakumbwa na wimbi jipya la mashambulizi ya makombora ya Urusi

Amani na Usalama

Nchini Ukraine Jumatatu ya leo Julai 8 imeanza na wimbi jingine la mashambulizi makubwa ya kijeshi yaliyotekelezwa na Urusi na kuua makumi ya watu, hospitali ya watoto ikiwa ni miongoni mwa maeneo yaliyoshambuliwa.

Mashambulizi haya ya leo yaliyotokea wakati watu waliopokuwa ndio kwanza wanaianza siku, yameilenga miji kadhaa ya Ukraine ikiwemo mji mkuu, Kyiv na mji mingine kama Kryvyi Rih na Pokrovsk.

Akilaani mashambulizi hayo, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Ukraine ambaye pia ni mratibu mkuu wa misaada ya kibinadamu nchini humo, Denise Brown, amesema, "ni jambo lisilokubalika kuona kwamba watoto wanauawa na kujeruhiwa katika vita hii. Chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu, hospitali zina ulinzi maalum. Raia lazima walindwe."

Mbali na Hospitali ya Watoto ya Ohmatdyt huko Kyiv, miundombinu mingine ya umma pia imeharibiwa, pamoja na majengo ya biashara na makazi katika miji ikiwa ni pamoja na Dnipro, Kramatorsk, Kryviy Rih, Kyi na Pokrovsk.

Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa, takriban watu 20 wameuawa katika mashambulizi haya ya leo Julai 8.

Rais Volodymyr Zelenskiy wa Ukraine amesema zaidi ya makombora 40 yamerushwa.

Uharibifu uliosababishwa na shambulio la kombora la asubuhi katika mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, wakati hospitali ya watoto ilipopigwa.
UNOCHA/Viktoriia Andriievska
Uharibifu uliosababishwa na shambulio la kombora la asubuhi katika mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, wakati hospitali ya watoto ilipopigwa.

Ofisi ya haki za binadamu OHCHR

Matukio haya ya hivi karibuni ya umwagaji damu yanafuatia tahadhari kutoka kwa wachunguzi wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa kwamba mwezi Mei ulishuhudia idadi kubwa zaidi ya vifo vya raia vilivyosababishwa na mashambulizi ya Urusi katika takriban mwaka mmoja.

Kulingana na ripoti ya ofisi hiyo kati ya tarehe 1 Machi na 31 Mei, angalau raia 436 waliuawa na wengine 1,760 walijeruhiwa.

Waliojeruhiwa ni pamoja na wafanyakazi sita wa vyombo vya habari, wafanyakazi 26 wa huduma za afya, wafanyakazi 5 wa kutoa misaada na wafanyakazi 28 wa huduma za dharura.

Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa imeongeza kuwa wengi wao yaani asilimia 91 ya waliopoteza maisha walikuwa katika eneo linalodhibitiwa na Ukraine na asilimia tisa katika eneo linalokaliwa na Urusi.

Katika kipindi hicho hicho cha taarifa, mamlaka ya Urusi iliripoti kwamba raia 91 waliuawa na 455 kujeruhiwa nchini Urusi kutokana na mashambulizi yaliyoanzishwa na vikosi vya kijeshi vya Ukraine, hasa katika mikoa ya Belgorod, Briansk na Kursk.

UNICEF imeshtushwa na kusikitishwa

Kupitia taarifatake iliyotolewa leo akilaani vikali mashambulizi hayo mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumiawatoto UNICEF Catherine nRussel amesea “Nimeshtushwa na habari kutoka Ukraine leo kwamba watu wasiopungua 150 wameripotiwa kuuawa au kujeruhiwa, na hospitali ya watoto kuharibiwa vibaya huko Kyiv, wakati wa wimbi la makombora mabaya nchini kote.”

Msururu wa makombora ulianguka katika miji mbalimbali ikiwa ni pamoja na Kyiv, Dnipro, Kryvyi Rih, Sloviansk na Kramatorsk.

Ameongeza kuwa “Bado hatujajua idadi ya watoto waliouawa au kujeruhiwa katika mashambulizi haya. Moyo wangu unawahurumia wale ambao wamepoteza wapendwa wao. Shambulio kwenye Hospitali ya Okhmatdyt, kituo kikubwa zaidi cha matibabu cha watoto nchini humo, bado ni kumbusho jingine la kikatili kwamba hakuna mahali palipo salama kwa watoto nchini Ukraine. Hospitali zinapaswa kuwa mahali salama, na zinapewa kiwango maalum cha ulinzi chini ya sheria za kimataifa. Raia, pamoja na watoto na vifaa na huduma wanazozitegemea, lazima vilindwe kila wakati.”

Bi. Russel amehitiishaujumbe wake akisema “Karibu miaka mitatu tangu kuongezeka kwa vita nchini Ukrainia, inaonekana hakuna mwisho wa hofu ambayo watoto na familia zao wanalazimika kuivumilia.

Matokeo ya shambulio la kombora kwenye mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, wakati hospitali ya watoto na mijengo mengine yaliharibiwa vibaya.
UNOCHA/Viktoriia Andriievska
Matokeo ya shambulio la kombora kwenye mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, wakati hospitali ya watoto na mijengo mengine yaliharibiwa vibaya.

#Siowalengwa

Na wakati kukiwa na video iliyochapishwa mtandaoni ikionyesha wahudumu wa kujitolea wakijaribu kuchakura katika kifusi na kusaka manusura katika hospitali mjini afisa mkuu wa UNICEF nchini Ukraine, Munir Mammadzade amesema katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X kwamba shirika hilo lilikuwa likitoa huduma za dharura za maji na usafi kwenye kituo hicho, saa chache baada ya tukio hilo. 

"Tumepokea ripoti za kutisha za hospitali ya watoto huko Kyiv iliyoharibiwa sana katika shambulio asubuhi ya leo, na ripoti za majeruhi. Watoto si watu wa kulengwa #NotTarget na lazima walindwe kila wakati."