Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC: Kuna ongezeko la kutisha la usafirishaji haramu wa watu

Manusura wa unyanyasaji wa kingono nchini DR Congo wanapona kwa usaidizi wa wafanyakazi wa mstari wa mbele wa UNFPA.
© UNFPA/Junior Mayindu
Manusura wa unyanyasaji wa kingono nchini DR Congo wanapona kwa usaidizi wa wafanyakazi wa mstari wa mbele wa UNFPA.

DRC: Kuna ongezeko la kutisha la usafirishaji haramu wa watu

Wahamiaji na Wakimbizi

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa jana Julai 4 mjini Geneva, Uswisi waeleza kusikitishwa na ripoti za kuenea kwa usafirishaji haramu wa watu, hasa kwa ajili ya utumwa wa kingono na unyonyaji, na kuongezeka kwa ndoa za watoto na za kulazimishwa zinazotokana na migogoro na kuhama makwao mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

"Tunashtushwa na idadi iliyoripotiwa, takribani waathirika 531 wa unyanyasaji wa kingono unaohusiana na migogoro kuanzia Agosti 2023 hadi Juni 2024, katika majimbo ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini, Ituri, Tanganyika na Manyema," wataalam wamesema na kuongeza kwamba, "madai yaliyoletwa kwetu yanaelezea wanawake na wasichana waliofurushwa walitekwa nyara kwa madhumuni ya unyanyasaji wa kingono, unyonyaji au utumwa wa kingono, wakati wakitafuta chakula au kuni au kushiriki katika shughuli za kilimo.
 
"Ripoti za kuhusika kwa vikosi vya ulinzi na usalama katika utumwa wa kingono, unyonyaji wa kijinsia, ukatili wa kijinsia na ndoa za utotoni ni jambo la kutia wasiwasi." Wanasisitiza wakidai kwamba, “ongezeko lililoripotiwa la ndoa za utotoni, za mapema na za kulazimishwa na kuhalalisha ukiukaji huu wa haki za binadamu kunatia wasiwasi sana, wataalam walisema.
 
Ukosefu wa utambulisho vya watu waliosafirishwa kiharamu na watu walio katika hatari ya usafirishaji haramu wa binadamu na ukosefu wa upatikanaji wa huduma za ulinzi ni jambo la msingi wakati wa migogoro inayoendelea na janga la kibinadamu.
 
Wataalamu hao wanaongeza kwamba wanafahamu, "pia kwamba hii ni ncha tu ya barafu. Changamoto, kama vile hofu ya kulipizwa kisasi na makundi yenye silaha, unyanyapaa wa kijamii, ukosefu wa ufuatiliaji wa ufanisi wa waathiriwa waliotekwa nyara ambao wanaweza kusafirishwa, kutambuliwa, na kupelekwa haraka kwa huduma za ulinzi, pamoja na kutokujali, huzuia waathiriwa kutoa taarifa kwa mamlaka na mashirika ya Umoja wa Mataifa.”
 
Mapigano kati ya vikosi vya jeshi na vikundi visivyo vya serikali katika majimbo kama vile Kivu Kaskazini na Kusini yanasababisha idadi kubwa ya watu kuyahama makazi yao, na hivyo kuzidisha hatari za ulinzi. Mashirika ya kibinadamu na mashirika ya kiraia yanatatizika kufanya kazi ndani na kufikia maeneo haya, jambo ambalo linazuia kwa kiasi kikubwa watu waliokimbia makazi yao kupata chakula na elimu, na ulinzi. Wasichana hasa wadogo, wanakabiliwa na hatari kubwa ya kusafirishwa kwa ajili ya unyonyaji wa kijinsia na ndoa za utotoni.
 

Kufungwa kwa MONUSCO

 
Wataalamu hao pia wameelezea wasiwasi wao kuhusu kufungwa kwa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC wakisema, "tuna wasiwasi kwamba kwa kujiondoa kwa MONUSCO, vipengele muhimu vya mifumo ya hadhari ya mapema ya ukiukaji wa haki za binadamu haitafanya kazi tena, na hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa ufuatiliaji wa haki za binadamu, kuripoti na uchunguzi."
 
Serikali ya DRC inapaswa kuhakikisha upatikanaji usiozuiliwa wa wahusika wa haki za binadamu katika eneo lote, ili kuhakikisha uwekaji kumbukumbu na uzuiaji wa ukiukaji wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na kuhusu unyanyasaji wa kingono unaohusiana na migogoro na usafirishaji haramu wa watu.
 
"Tunaziomba pande zote katika mzozo wa DRC, kwa ushirikiano na jumuiya ya kimataifa, kushughulikia kikamilifu ukiukwaji huo na kuimarisha upatikanaji wa haki na masuluhisho, kwa nia ya kukabiliana na hali ya kutowajibisha wahusika kama njia ya kujenga amani ya kudumu na kwa kufuata sheria za kimataifa kuhakikisha uwajibikaji kwa wafanyaji wa uhalifu huu wa kutisha.” Wataalam hao wamesema na kwamba wamekuwa katika mawasiliano na mamlaka za DRC.