Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Machungu,  ukatili vyakumba wakimbizi na wahamiaji barani Afrika wakielekea Mediteranea kisha Ulaya

Wahamiaji ambao wamerejeshwa pwani ya Libya baada ya kufunga safari kupitia bahari kuelekea Ulaya wakipokelewa na wafanyakazi wa IOM.
IOM Libya Wahamiaji ambao wamerejeshwa pwani ya Libya baada ya kufunga safari kupitia bahari kuelekea Ulaya wakipokelewa na wafanyakazi wa IOM.

Machungu,  ukatili vyakumba wakimbizi na wahamiaji barani Afrika wakielekea Mediteranea kisha Ulaya

Wahamiaji na Wakimbizi

Mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) la kuhudumia wahamiaji, IOM na Kituo cha Wahamiaji Mseto (MMC) yametoa ripoti inayoelezea kuendelea kwa vitendo vya unyanyasaji, ukiukwaji wa haki za binadamu na unyonyaji ambao unafanywa sio tu baharini Mediteranea lakini pia kwenye njia za nchi kavu katika bara la Afrika kuelekea ufukwe kwa bara hilo kwenye bahari ya Mediterania.

Taarifailiyotolewa leo na mashirika hayo huko Geneva, Uswisi inasema ripoti hiyo iliyopewa jina la “Katika safari hii, hakuna anayejali ikiwa unaishi au kufa” imeangazia juu ya hatari ambazo hazijaandikwa na kutangazwa kwa wakimbizi na wahamiaji.

Inaeleza kwamba watu wengi wanakadiriwa kufa zaidi kuelekea Ulaya kupitia jangwa la Sahara kuliko Bahari ya Mediterania huku vifo vya wakimbizi na wahamiaji jangwani vikidhaniwa kuwa ni maradufu zaidi ya vile vinavyotokea kwa wanaovuka kupitia Bahari ya Mediterania huku ikionya juu ya ongezeko kubwa la watu wanaojaribu kuvuka ardhi hii hatari.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wakimbizi na wahamiaji wanazidi kuvuka maeneo ambako makundi ya waasi, wanamgambo na wahalifu wengine wanafanya kazi, na ambapo biashara haramu ya binadamu, utekaji nyara kwa ajili ya kikombozi, kazi za kulazimishwa na ukatili wa kingono umeenea.

Licha ya ahadi zinazofanywa na Jumuiya ya kimataifa kuokoa maisha na kushughulikia udhaifu unaondelea, kwa mujibu wa sheria za kimataifa, mashirika hayo matatu yanaonya kwamba hatua za sasa za kimataifa hazitoshi kutokana na mapungufu makubwa kwenye ulinzi katika njia ya kati ya Mediterania.

Yanachotaka sasa mashirika hayo ni ulinzi mahsusi kulingana na njia wanazotumia wakimbizi na wahamiaji ili kuokoa maisha, kupunguza machungu na kung’oa mzizi wa kile kinachosababisha watu kukimbia nchi zao kwa kusaka mbinu bora za ujenzi wa amani.