SCO mna uwezo wa kukomesha vita ili kukabiliana na changamoto nyingine za ulimwengu - Guterres
SCO mna uwezo wa kukomesha vita ili kukabiliana na changamoto nyingine za ulimwengu - Guterres
Amani na Usalama
Ubinadamu unahitaji uchumi mmoja wa kimataifa, soko la kimataifa, mtandao wa kimataifa, na seti moja ya sheria za matumizi ya teknolojia mpya, hasa akili mnemba, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ameyasisitiza hayo akizungumza leo Alhamisi Julai 4 mjini Astana katika mkutano wa ushirikiano wa nchi za ukanda wa Ulaya na Asia uitwao Shanghai Cooperation Organisation au SCO ambao ni ushirika wa kisiasa, kiuchumi, kimataifa na usalama na ulinzi la Ulaya na Asia lililoanzishwa na China na Urusi mnamo mwaka 2001.
Changamoto za kimataifa
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameonesha wasiwasi wake kwamba tofauti za kijiografia na kisiasa zinazuia jumuiya ya kimataifa kushughulikia ipasavyo masuala muhimu yanayoathiri kila mtu. Hasa, akitaja vitisho viwili vilivyopo yaani mabadiliko ya tabianchi na maendeleo ya teknolojia ya kidijitali.
"Tunakutana katika mazingira magumu ya kimataifa. Vita vikiendelea. Mgawanyiko wa kijiografia na kisiasa. Janga la kutokujali. Kujiondoa kutoka kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu. Ubaguzi na janga la wa uaminifu. Watu wanapoteza imani katika ushirikiano wa kimataifa,” amesema, akikumbuka ahadi ambazo hazikutimizwa, viwango viwili na kuongezeka kwa ukosefu wa usawa. Nchi zinaweza tu kutatua matatizo haya ya kimataifa kwa kuunganisha nguvu, Guterres anaamini.
Shanghai Cooperation Organization
Haikutokea tu kwamba mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameibua masuala haya katika Shanghai Cooperation Organisation. Idadi ya jumla ya nchi za SCO ni takriban watu bilioni 3.5. "SCO ni shirika kubwa zaidi la kikanda duniani - lina nguvu na lazima lifanikishe amani," Guterres amebainisha.
Nchi nyingine wakati huo mwaka 2001 zilizohusika katika kuanzisha SCO ni pamoja na Kazakhstan, Tajikistan, Kyrgyzstan na Uzbekistan, halafu baadaye wakaingia India, Pakistan na Iran.
Lengo kuu ni amani
"Ni wakati wa kuweka upya upya ahadi yetu ya pamoja ya ushirikiano wa kimataifa," Katibu Mkuu amesisitiza. Ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa kwa kuzingatia kanuni za Mkataba wa Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa na Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu, ndio kiini cha juhudi hizo.
Amani katika mataifa mengine
Pia Katibu Mkuu amesisitiza kuwa amani inahitajika katika Mashariki ya Kati - kusitishwa kwa mapigano huko Gaza na kuachiliwa mara moja na bila masharti kwa mateka wote wa Israeli waliochukuliwa mnamo Oktoba 7.
Kulingana na yeye, amani "kulingana na Mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria ya kimataifa" lazima ipatikane nchini Ukraine. Ametaka amani ipatikane katika nchi nyingine pia: kuanzia Sudan hadi Sahel, kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) hadi Somalia, kutoka Myanmar hadi Haiti na Afghanistan.
Ziara ya nchi za Asia ya Kati
Kando ya mkutano wa SCO, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amefanya mikutano kadhaa ya nchi mbili le oleo Julai 7, ikiwa ni pamoja na kukutana na Rais wa Belarus Alexander Lukashenko. Wakati wa mkutano huo, Guterres amezungumzia haja ya kukomesha vita nchini Ukraine kwa kuzingatia kanuni za Mkataba wa Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa na kuheshimu uadilifu wa eneo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia ameeleza wasiwasi wake kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Belarus. Amebainisha kuwa msamaha uliotangazwa nchini Belarus siku moja kabla ni hatua ya kuelekea heshima kamili ya haki za binadamu na kuhakikisha uhuru wa kimsingi katika nchi hii.
Leo, mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa anamaliza ziara yake ya siku mbili nchini Kazakhstan na kuelekea Tajikistan. Hapo awali, kama sehemu ya safari hii, Guterres alitembelea Uzbekistan na Kyrgyzstan.