UNHCR yaziongeza Uganda na Libya kwenye orodha ya nchi zipokeazo wakimbizi kutoka Sudan
UNHCR yaziongeza Uganda na Libya kwenye orodha ya nchi zipokeazo wakimbizi kutoka Sudan
Mapigano yakiendelea Sudan, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) limeziongeza Uganda na Libya kwenye orodha ya nchi zinazopokea wakimbizi na hivyo kufanya idadi ya nchi zinazopokea wakimbizi hao kufikia 7.
Ewan Watson, ambaye ni Mkuu wa Mawasiliano ya Kimataifa wa UNHCR amewaeleza waandishi wa habari jijini Geneva, Uswisi hii leo kuwa nchi nyingine 5 ambazo tayari zilikuwa zimeorodheshwa ni Jamhuri ya Afrika ya Kati, (CAR), Ethiopia, Sudan Kusini, Chad na Misri.
Kutokana na kuongezeka kwa nchi mbili hizo, kiwango cha fedha cha kusaidia wakimbizi hao katika nchi hizo hadi mwishoni mwa mwaka huu nacho kimeongezeka kutoka dola bilioni 1.4 hadi dola bilioni 1.5.
Wakimbizi Libya na Uganda
Nchini Libya, UNHCR imesajili zaidi ya wakimbizi 20,000 wa Sudan ambapo wamefika nchini huko tangu Aprili2023, na makadirio ya wengine wengi zaidi kufika mashariki mwa nchi hiyo.
Tangu mapigano yaongezeke katika jimbo la Darfur, huduma za kijamii zinazotolewa eneo hilo zimezidiwa uwezo huku familia za wakimbizi zikijikuta zikilala nje kutokana na kukosekana kwa makazi. Vifaa vya matibabu havikidhi mahitaji, hivyo kuwaweka Watoto katika hatari ya utapiamlo.
Nchini Uganda, nchi yenye idadi kubwa ya wakimbizi barani Afrika, imepokea zaidi ya wakimbizi 39,000 wa Sudan tangu kuanza kwa vita mwaka jana. Kati yao, karibu 27,000 wamefika mwaka huu pekee ambayo ni takribani mara tatu zaidi ya ilivyotarajiwa huku wengi wao wanahifadhiwa katika makazi ya wakimbizi ya Kiryandongo, magharibi mwa nchi ambapo wanapokea misaada ya kibinadamu.
Watu wanahamahama Sudan kila wakati
Watson amesema miezi 14 tangu kuzuka kwa vita nchini Sudan, maelfu ya watu bado wanahama nchini humo kila siku, wakikimbia ukatili na unyanyasaji, vifo, huduma hafifu, upatikanaji mdogo wa misaada ya kibinadamu na njaa inayowakabili, ijapokuwa nchi jirani zimeonesha mshikamano mkubwa katika kuwapokea wale wanaokimbia vita.
Tangu mzozo huo uanze, watu milioni 10 wamekimbia makazi yao nchini Sudan, huku wengi wakilazimika kuyahama makazi yao mara kadhaa kutafuta usalama.
Kwa ujumla UNHCR inasema kati ya hao milioni 10, milino 2 wamekimbilia nchi jirani na milioni 7.7 ni wakimbizi wa ndani wapya na wakimbizi 220,000 ambao wamehamia wenyewe ndani ya nchi.