Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Burkina Faso: Mgogoro uliosahaulika Afrika : Kurejesha elimu bora

Watoto wakijifunza jinsi ya kupatia chanjo kuku huko Ouahigouya, Burkina Faso.
© UNICEF/Ndiaga Seck
Watoto wakijifunza jinsi ya kupatia chanjo kuku huko Ouahigouya, Burkina Faso.

Burkina Faso: Mgogoro uliosahaulika Afrika : Kurejesha elimu bora

Utamaduni na Elimu

Nchini Burkina Faso, ufadhili kutoka Mfuko wa Elimu Haiwezi Kusubiri au Education Cannot Wait, wadau wa elimu duniani likiwemo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF na wadau wa kimkakati wanawarejesha shuleni wasichana na wavulana. Wanarejeshwa maeneo salama wanakoweza kujifunza kwa njia mbali mbali ikiwemo kupitia vipindi vya redio. Wakipatiwa  mafunzo kama ya ufundi ili hatimaye wajifunze kile walichokosa.

Katika taifa la hilo la Afrika Magharibi la Burkina Faso, kufungwa kwa shule kunaathiri elimu ya takriban watoto 820,000. Njaa, vita vya silaha, kuhamishwa kwa nguvu na mambo mengine yanawaweka wasichana na wavulana katika hatari kubwa na kupunguza juhudi za kutimiza malengo ya Maendeleo Endelevu.

Wavuti wa UNICEF umechapisha makala inayosema kuwa mgogoro unaoendelea umesababisha kufungwa kwa shule 5,300 na kuwahamisha takriban watu milioni 2. Familia zinahama kutoka makazi yao, wavulana wako katika hatari kubwa ya kusajiliwa katika makundi ya silaha, mamia ya wasichana wanalazimishwa kuolewa katika ndoa za utotoni, na ndoto na uwezo wa kizazi kizima uko kwenye hatihati.

Simulizi ya Juliette na matarajio ya siku zijazo

Kwa wasichana na wavulana waliolazimika kukimbia ukatili, kupatikana kwa fursa za kujifunza zenye ubora unatoa mwanga wa matumaini katika dunia iliyogeuzwa juu chini. Kupitia elimu, watoto kama Juliette na Amadé wanajikakamua kufuata ndoto zao. Hapa, walishiriki hadithi zao za matumaini na ukombozi katika maeneo ya migogoro iliyosahaulika ya Afrika.

Msichana mwenye umri wa miaka kumi na nne akipokea vifaa vya shule kutoka UNICEF huko Kaya, Burkina Faso.
© UNICEF/Amadou Cisse
Msichana mwenye umri wa miaka kumi na nne akipokea vifaa vya shule kutoka UNICEF huko Kaya, Burkina Faso.

Licha ya kulazimishwa kuhama nyumbani, Juliette mwenye umri wa miaka 14 anakataa kuacha ndoto yake ya kuwa mwalimu. Anakumbuka ilivyokuwa akisema, "siku moja, tulikuwa darasani, na walikuja kututoa, na tukakimbia. Tuliweka vitu vyetu kwenye mkokoteni, na tukaja Barsalogho ambapo tulipanda basi kwenda Kaya," anasema Juliette, akiongeza kuwa "njiani, tulipata shida ya njaa na kiu. Tulilala porini. Tulipofika Korko, tulitamani kukaa pale lakini kulikuwa na ukosefu wa usalama, kwa hivyo tuliendelea. Tuliendelea kuteseka hadi tulipofika Kaya.”

Walipofika Kaya, Juliette na mama yake walibahatika na kupata mahali pa kuishi na marafiki yao. Nyumba haikuwa ya kifahari, lakini ilikuwa karibu na shule ya umma. Juliette alikuwa na ndoto ya kuwa mwalimu, na kwa kuwa shule ilikuwa karibu, shauku yake ya kujifunza ilimrudia. Kupitia mpango uliyotolewa na UNICEF kwa ushirikiano na serikali na washirika wa ndani, Juliette aliweza kujisajili katika madarasa ya wanafunzi waliosalia nyuma na sasa amerudi shuleni.

UNICEF na wadau na mwelekeo wa kunusuru watoto kama Juliette

Tangu 2019, Education Cannot Wait (ECW), ambao ni mfuko wa kimataifa wa elimu kwa dharura na migogoro ya muda mrefu unaosimamiwa na UNICEF, umewekeza zaidi ya dola milioni 23 nchini Burkina Faso. Mfuko huu unawafikia takriban watoto 400,000, wakiwemo watoto 167,000 ambao ni wakimbizi wa ndani na zaidi ya watoto 200,000 wa jamii zinazoishi na wakimbizi. Uwekezaji huo unatoa vifaa vya kujifunzia, mafunzo na ufadhili wa walimu, kujenga na kukarabati maeneo ya kujifunzia ya muda, na kutoa usaidizi mwingine wa kina kuwarudisha wasichana na wavulana kwenye usalama na uhakika wa darasani.

"Ninafuraha kupokea vifaa hivi vya shule kwa sababu nilikaribia kwenda kuuza mitaani ili kulipia vifaa na masomo. Nataka kuwa mwalimu na kutoa maarifa kwa watoto. Pia nitakuwa na mshahara kusaidia wazazi wangu," anasema Juliette.

Watoto wanahudhuria kozi ya ufugaji kuku nchini Burkina Faso.
© UNICEF/Ndiaga Seck
Watoto wanahudhuria kozi ya ufugaji kuku nchini Burkina Faso.

Mafunzo ya ufundi yanafungua milango

Amadé, mwenye umri wa miaka 13, ana ulemavu wa kuona. Mafunzo ya ufundi yamemuweka kwenye njia ya mafanikio. Tangu kuzaliwa, Amadé amekuwa na tatizo la jicho la kushoto. Miaka iliyopita, hali imezidi kuwa mbayá zaidi.

Takriban mwaka mmoja uliopita, Amadé na familia yake walikimbia kutoka Djibo. Mji huo, ulio karibu na mpaka wa Mali, uko katika tishio la mara kwa mara, na vizuizi vilivyowekwa na wapiganaji wanaohusishwa na Al-Qaida na taifa hilo la kiislamu limezuia upatikanaji wa chakula, huduma za afya na huduma zingine muhimu kwa zaidi ya mwaka mmoja. Kwa namna fulani, Amadé na familia yake walifanikiwa kutoka na kupata hifadhi huko Ouahigouya, umbali wa takriban kilometa 100.

Kwa sababu ya ulemavu wake wa kuona, Amadé amekuwa na upatikanaji mdogo sana wa elimu rasmi kwa miaka mingi. "Nilipokuwa mdogo sana, wazazi wangu walinisajili shuleni. Wakati huo, tulikuwa bado Djibo. Kwa bahati mbaya, kutokana na tatizo la jicho langu, nililazimika kuacha masomo katika CP1. Tulijaribu kulitibu, lakini ilikuwa vigumu kwa sababu ya hali mbaya ya usalama," anasema Amadé.

Mnamo mwezi Juni mwaka 2023, Amadé aligundua kituo cha kilimo huko Ouahigouya ambapo mpango unaofadhiliwa na ECW, uliotolewa na UNICEF, ulikuwa unatoa mafunzo ya ufundi. Kwenye shamba, Amadé sasa anajifunza kuhusu utengenezaji wa keki, na ufugaji wa kondoo na kuku.

"Tunafundishwa njia tofauti za kulisha kuku na jinsi ya kuwatunza. Tunajifunza hata jinsi ya kuwachanja ili wasipate magonjwa. Lakini kitu ninachokipenda zaidi ni ufugaji wa kondoo. Ningependa kuwa na uwezo wa kufuga kondoo," anasema.

Msichana anajifunza jinsi ya kuchanja kuku katika kozi ya ufugaji kuku nchini Burkina Faso.
© UNICEF/Ndiaga Seck
Msichana anajifunza jinsi ya kuchanja kuku katika kozi ya ufugaji kuku nchini Burkina Faso.

Mafunzo ni pamoja na ushoni, uzalishaji wa nishati mbadala, na ufugaji

Kama sehemu ya ajenda ya ndani iliyoainishwa katika Makubaliano ya Grand Bargain, uwekezaji huo unatekelezwa mashinani na mashirika ya ndani yasiyo ya kiserikali yakiwemo Children Believe na Centre Diocésain de Communication, kwa msaada kutoka UNICEF na ufadhili kutoka ECW.

Makundi ya wanafunzi 40 hadi 50 kwa kituo yanapewa kifurushi cha masomo matatu. Masomo hayo yanashughulikia kila kitu kutoka ushonaji, ufundi mitambo na nishati mbadala, hadi uwekaji vigae, ufugaji wa kuku, utengenezaji wa jusi, ususi, na, bila shaka, kipenzi cha Amadé, ufugaji wa kondoo.

Ujasiri na dhamira ya Amadé vimevutia walimu na wanafunzi wenzake pia.

"Tangu tuanze mpango huu wa mafunzo, hajawahi kukosa darasa. Jicho lake linapouma sana, anatoka nje hadi litakapopona. Nimevutiwa na ujasiri wake," anasema mwalimu wake Andréa Belem.

Nafanya bidii kuwa miongoni mwa wanafunzi bora. Hivyo, nitaweza kupata ninachohitaji kuanzisha mradi wangu wa ufugaji. Na nitaweza kusaidia wazazi wangu kupata suluhisho la jicho langu lenye ugonjwa. — Amadé, 13

Mwishoni mwa mafunzo ya miezi mitatu, wanafunzi bora watapewa vifaa vya kuanzia. Kwa upande wake, Amadé anatarajia kupewa kondoo ili aweze kuanzisha biashara yake mwenyewe.

"Nafanya bidii kuwa miongoni mwa wanafunzi bora. Hivyo, nitaweza kupata ninachohitaji kuanzisha mradi wangu wa ufugaji. Na nitaweza kusaidia wazazi wangu kupata suluhisho la jicho langu lenye ugonjwa.” anaelezea.

Harakati ya umoja

Zaidi ya wanafunzi 1,000 tayari wamekamilisha mafunzo yao, wakati wengine wanapata msaada wa kurejea shuleni, kupata elimu kwa njia ya mbali kupitia vipindi vya redio, na kufaidika na usaidizi wa kina wa elimu unaotolewa kupitia mpango huo.

Hawako peke yao. Idadi ya wasichana na wavulana nchini Burkina Faso wameelezea hadithi zao kupitia Kadi za posta Kutoka Pembeni kwa Education Cannot Wait. Wanatoa wito kwa viongozi wa dunia kuimarisha na kutoa rasilimali za dharura kwa mashirika kama Education Cannot Wait na UNICEF ili kutimiza ahadi zao za elimu kwa wote, kama ilivyoainishwa katika Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs.