Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Al Hassan apatikana na hatia ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya kibinadamu Mali 

Mwanamume aliyevaa kilemba cheupe na miwani ameketi chumba cha mahakama, akiangalia skrini ya kompyuta.
©ICC-CPI Al Hassan Ag Abdoul Aziz Ag Mohamed Ag Mahmoud wakati wa hukumu mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC tarehe 26 Juni 2024

Al Hassan apatikana na hatia ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya kibinadamu Mali 

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Hii leo, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC imemkuta na hatia Al Hassan Ag Abdoul Aziz Ag Mohamed Ag Mahmoud kwa makosa dhidi yaje ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu aliyotenda nchini Mali.

Mahakama hiyo imesema Al Hassan alitenda makosa hayo kati ya tarehe 2 Aprili 2012 na 29 Januari mwaka 2013 huko Timbuktu, kaskazini mwa Mali, eneo ambalo lililikuwa linadhibitiwa wakati huo na na vikundi vilivyojihami vya Ansar Dine na Al-Qaida in Islamic Maghreb au (AQIM).

Majaji katika kesi hiyo walikuwa Antoine Kesia-Mbe Mindua ambaye alikuwa Jaji Mfawidhi, na wengine Jaji Tomoko Akane na Jaji Kimberly Prost.

Akisoma uamuzi wao, Jaji Kesia-Mbe alisema, “ijapokuwa Al Hassan alikuwa anafanyia kazi kundi lililokuwa linadai kutumia sheria ya kiislamu ya Sharia, kesi hii haikuwa inahusu Sharia, au dini ya kiislamu kwa ujumla.”

Alisema kesi ilihusu vitendo na tabia ya mtu mmoja Al Hassan, katika muktadha mahsusi. Mahakama ilichunguza ushahidi wa kuthibitisha uhusika wa Al Hassan pasipo shaka katika vitendo husika.

Mahakama ilisema kuwa baada ya kuajiriwa na viongozi waandamizi wa AQIM, Al Hassan alikuwa mwanachama mwandamizi wa Polisi wa kikundi hicho akichukua jukumu la uongozi likiwemo kupanga mtandao wa kazi ya polisi.

Polisi wa kikundi hicho walikuwa na dhima kubwa kwenye mfumo wa Ansar Dine/AQIM uliokuwa umewekwa kwa ajili ya kutekeleza uhalifu.

Makosa dhidi ya Al Hassan

Makosa aliyobainika kuwa nayo ni uhalifu dhidi ya binadamu kwa kutenda mateso, uhalifu wa kivita wa kufanya mateso na kufanya watu dhalili, uhalifu wa kivita wa kukata watu viungo, kuhukumu watu bila kesi, uhalifu wa kivita wa kufanyia watu mateso na vitendo visivyo ya kibinadamu.

Ingawa Mahakama ilibaini matukio ya ukatili wa kingono Timbuktu wakati wa kipindi husika, Al Hassan  hakupatikana na hatia dhidi ya makosa ya uhalifu wa kivita wa ubakaji na utumwa wa kingono, uhalifu wa kivita wa kubaka binadamu na ndoa za lazima.

Al Hassan pia hakupatikana na hatia dhidi ya makosa ya kushambulia maeneo na vifaa vilivyolindwa.

Tangazo kuhusu mchakato wa utoaji hukumu dhidi ya Al Hassan itatolewa punde na hukumu inaweza kupingwa na Mwendesha Mashtaka wa ICC au upande wa utetezi wa Al Hassan ndani ya siku 30.

Kauli ya Guterres

Mara baada ya ICC kutoa tangazo hilo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alieleza kutambua uamuzi huo na kusema ni hatua muhimu katika kuwajibisha na zaidi ya yote hatua muhimu katika juhudi za kupatia haki yao waathiriwa na manusura wa uhalifu huo uliotendeka huko Timbuktua nchini Mali.

“Hii itasaidia kudhihirisha kuwa ukwepaji wa sheria hautavumiliwa,” amesema Katibu Mkuu akitamatisha taarifa yake iliyotolewa na msemaji jijini New York kwamba “fikra zangu zinasalia na waathiriwa wa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu huko Timbuktu Mali ambamo kwayo Al Hassan amepatikana na hatia.”