Qatar yaipatia WFP tani 120 za tende kusaidia wakimbizi wa DRC na Burundi nchini Tanzania
Qatar yaipatia WFP tani 120 za tende kusaidia wakimbizi wa DRC na Burundi nchini Tanzania
Wito wa kusaidia kwa hali na mali wakimbizi 200,000 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na wale wa Burundi walioko Tanzania umeendelea kuitikiwa ambapo mwitikio wa hivi karibuni zaidi ni kutoka serikali ya Qatar ambayo imetoa msaada wa tani za ujazo 120 za tende zenye lishe kwa ajili ya kuimarisha afya za wakimbizi hao.
Shehena hiyo imekabidhiwa katika bandari ya Dar es salaam, kwa shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP nchini Tanzania kwa ajili ya wakimbizi hao walioko kwenye kambi za Nduta na Nyarugusu zilizoko Kigoma, kaskazini-magharibi mwa taifa hilo la Afrika Mashariki.
Taarifaya WFP Tanzania iliyotolewa jijini Dar es salaam imesema tende hizo zitasaidia wakimbizi walio hatarini kwa upande wa lishe kama vile akina mama wanaonyonyesha watoto wachanga pamoja na wagonjwa waliolazwa hospitalini.
WFP inasema msaada huu kutoka Qatar umekuja wakati shirika hilo linakabiliwa na pengo kubwa la ufadhili hali iliyosababisha wakimbizi kupatiwa asilimia 60 tu ya kiwango cha lishe kwa siku kinachotakiwa.
Mkurugenzi Mkazi wa WFP nchini Tanzania Sarah Gordon amesema msaada huo umekuja wakati muafaka na utasaidia wale walio na uhitaji zaidi na kwamba tende hizo zitachangia katika kuinua lishe ya maelfu ya wakimbizi.
Kwa sasa WFP kila mwezi hupatia wakimbizi hao kikapu chenye nafaka zilizoongezewa virutubisho, kunde, chumvi na mafuta ya kupikia, kwa lengo la kukidhi mahitaji ya msingi ya chakula na lishe.