UNICEF: Tuwasaidie watoto wa Sudan
UNICEF: Tuwasaidie watoto wa Sudan
Shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, linatoa wito kwa wadau kutoa msaada wa dharura ili kuwasaidia watoto wa Sudan wanaotatizwa na vita ambavyo vilianza mwaka mmoja uliopita na waathiriwa wakubwa ni watoto milioni 24 nchini humo.
Watoto hao wamepitia madhila mengi, kulazimika kukimbia kwao na kutohudhuria shule. Wengine wamekimbilia nchini Kenya kwa ajili ya kusaka hifadhi.
UNICEF nchini Kenya kwa kushirkiana na washirika, wadau na wasanii wameandaa hafla maalum jijini Nairobi, iliyopatiwa jina UNite with the children of Sudan, au Ungana na watoto wa Sudan, lengo likiwa ni kuwaleta pamoja watoto wakimbizi kutoka Sudan na kuukumbusha ulimwengu kuhusu jinamizi la vita.
Katika hafla hiyo UNICEF imewashirikisha wasanii wa kuchora ili kuwasilisha ujumbe. Galal Yousif, kijana kutoka Sudan, ni mmoja wa wachoraji ambaye alilazimika kukimbia vita na kutua Nairobi mwaka mmoja uliopita.
Sanaa yake inajikita katika kutazama ulimwengu kwa jicho la yajayo ukizingatia yaliyopita.UNICEF imewahi kutumia picha yake ya ukutani huko Khartoum, mji mkuu wa Sudan, kabla ya vita kuanza.
Galal alilelewa kijijini karibu na mto Nile. Kwa Sasa yuko Nairobi na anaelezea kuwa safari hiyo ilikuwa ngumu, ”Hatukuwa na uhakika kwa muda mfupi, ila tulifanikiwa kutoka. Kulikuwa na vizuizi vingi vya wapiganaji lakini tuliponea. Niliamua kwenda kijijini kwetu na baada ya hapo ndio niliondoka kwani nisingeweza kupata kazi na kuwasaidia watu wangu nyumbani. Nilionelea pia ni vyema kutumia sanaa kama kipaza sauti changu kuelezea kinachoendelea Sudan. Kwa sasa natumia Sanaa kuwaangazia watoto wa Sudan na kusimulia yaliyowasibu.”
Watoto wanapata makovu ya vita
UNICEF kwa ushirikiano na washirika na wadau iliandaa hafla maalum kuukumbusha ulimwengu kuwa hali ni mbaya Sudan na watoto wanaumia zaidi. Takwimu za UNICEF zinaashiria kuwa watoto milioni 24 wanapambana na utapiamlo, njaa, ghasia na madhila mengine.
Mary Louise Eagleton ni Naibu Mwakilishi wa UNICEF nchini Sudan na anabainisha kuwa watoto wa Sudan wako katika hali mbaya kwani, “Watoto wanapata makovu ya vita … wanakabiliana na madhila. Watoto wasiopungua milioni tano wanapata taabu kote Sudan. Wamepoteza makazi yao, familia zao, marafiki wao na pia imani. Makovu hayo ni mazito ila watoto wana uwezo mkubwa wa kuhimili dhoruba. Tunachokifanya kama UNICEF na wadau wetu Save The Children ni kuwapa watoto hao mazingira salama. Tumewafanyia mamilioni bado wengine wanahitaji.”
Mchoraji mwingine aliyeonesha kipawa chake ni Amani Azhari ambaye ni Msanii wa Sudan aliyeishi nchini Uganda na sasa yuko Nairobi tangu vita vitibuke Khartoum.
Amani ameshawahi kushirikiana na UNICEF katika miradi ya kupambana na ukeketaji wa wanawake yaani FGM. Sanaa yake inajikita kwenye juhudi za kupaza sauti za wasichana na wanawake wanaokabiliana na vikwazo vya kila aina katika jamii.
Nchi yake iliposambaratika alipigwa na butwaa na, “Mara ya kwanza sikuamini kabisa kuwa kuna vita, nilidhani wanasema uongo. Nasikitika sana kwa sasa na familia yangu bado iko huko. Dada zangu na watoto wao na hata wazee wetu wote bado wako huko wanapambana. Hali ni mbaya. Mtandao hauaminiki na mawasiliano sio mazuri." Amesema Amani
Familia zimesambaratika
Vita nchini Sudan vimewaacha mamilioni bila makaazi na kulazimika kukimbilia maeneo salama katika nchi jirani. Sara, mama wa watoto watatu amelazimika kutengana na familia yake tangu vita kuanza.
Mtoto mmoja wa Sarah yuko Kampala anakosoma, mumewe yuko Khartoum kazini na yeye na watoto wake wawili waliosalia wanapata hifadhi kwenye kambi salama inayosimamiwa na shirika la kuhudumia watoto la Save The Children lililo mshirika wa UNICEF.
Maisha Kambini yamemuathiri mwanawe mmoja, “Mwanangu mmoja ana kiwewe na hilo linatutatiza sote. Kwa vile hawapo shule tuna wasiwasi. Pia, tumetawanyika kama familia kwa hiyo sio Jambo la kawaida kwao na hawajalizowea. Tunaishi mahali ambapo hatupajui na ni tofauti na kwetu. Hata hivyo hatuwezi kurejea mpaka nyumbani kutulie.”
UNICEF Kwa ushirikiano na wadau kama Save The Children imekuwa ikiwahudumia watoto wa Sudan. Watoto hao wanakabiliana na ukosefu wa usalama, huduma za msingi na hawaendi shule.
Kijzhala Shako ni meneja Mawasiliano wa Save The Children na anaelezea kuwa ushirikiano wao na UNICEF umewafungulia milango muhimu kwani, ”Ukiangalia hali ya watoto na familia zao…mahitaji yao … vile anavyovihitaji ni vingi kuliko ambavyo Save the Children na UNICEF inaweza kuwatimizia. Kwahiyo tunashirikiana kupata nafasi ya kuingia waliko waathiriwa…. Save the Children iko maeneo 13 ya Sudan na UNICEF kwenye mengine. Kwahiyo tukijumlisha juhudi zetu watu wengi zaidi wanapata usaidizi."
UNICEF kwa ushirikiano na wadau kama shirika la Marekani la misaada ya maendeleo ya kimataifa, USAID wameungana kuukumbusha ulimwengu kuhusu madhila na vita vya Sudan.
Watoto wa Sudan kama wengine wale, wanapania kurejea nyumbani kuishi maisha ya kawaida.