Umoja wa Mataifa hautaitelekeza Gaza
Umoja wa Mataifa hautaitelekeza Gaza
Timu za misaada za Umoja wa Mataifa na mashirika mengine yanayoshirikiana na Umoja wa Mataifa yanaendelea na nia ya dhati ya kufikisha misaada ya kuokoa maisha kwa watu wa Gaza wenye uhitaji, licha ya hatari zinazidi kuongezeka kwa wanaofanya kazi huko.
Mashambulizi makali yanaendelea
Katika taarifa ya hivi karibuni, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, liliripoti mashambulizi ya anga katikati mwa Gaza katika siku za hivi karibuni, hasa katika kambi za wakimbizi za Bureij, Maghazi na Nuseirat na mashariki mwa Deir Al Balah.
Wakati huo huo, mashambulizi ya ardhini ya jeshi la Israel "yanaendelea kupanuka", UNRWA inabainisha, hasa katika maeneo ya kusini ya Mji wa Gaza na mashariki mwa Rafah, na kusababisha mateso zaidi na "kuyumbisha" zaidi mtiririko wa misaada ya kibinadamu.
Vikwazo vya usafirishaji
Kwa upande wa Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya Kibinadamu, OCHA, linaripoti kwamba kati ya tarehe 18 na 23 Juni, mipango mitatu iliyoratibiwa ya kuchukua misaada kutoka upande wa Palestina wa Kerem Shalom ilifutwa kutokana na wasiwasi wa usalama, ikiwa ni pamoja na uhasama mkali na kuanguka kwa utulivu na usalama wa umma katika njia iliyopangwa na jeshi la Israel kwa ajili ya usafirishaji wa mizigo kati ya kivuko na Gaza ya kati.
Njaa
Uchambuzi wa data za satelaiti za hivi majuzi za Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO unaonesha ongezeko linaloendelea la ardhi ya kilimo iliyoharibiwa, huku zaidi ya nusu ya ardhi ikiharibiwa katika Ukanda wa Gaza au zaidi ya asilimia 57 kufikia Mei 2024. Kati ya ardhi hizi zilizoharibiwa, takriban asilimia 61 ni bustani, asilimia 19 ni mboga na mboga. Asilimia 20 ni nafaka. Picha hizo za satelaiti zinaonesha kuwa njia za magari makubwa, ufyatuaji makombora na shinikizo zingine zinazohusiana na migogoro pia zimeharibu miundombinu ya kilimo katika Ukanda wa Gaza.
Hakuna kurudi nyuma
Leo Jumanne Juni 26, Mkuu wa OCHA ambaye hivi karibuni ataondoka katika wadhifa huo, Martin Griffiths akijibu ripoti za vyombo vya habari kwamba Umoja wa Mataifa ulikuwa umeonya kwamba huenda juhudi za msaada zitasimama hadi pale hali ya usalama na uratibu na jeshi la Israel vitakapoimarika, amekanusha akisema hakuna kitu kama hicho.
"Tunaendelea, kama tulivyofanya kwa miezi hii mingi kujadiliana na viongozi wa Israeli na wengine kwa usaidizi mwingi, kutoka Marekani, kama unavyojua, kupata masharti sahihi ya kuiruhusu misaada kufikishwa kwa usalama.” Griffiths ameiambia Idhaa ya Umoja wa Mataifa katika mahojiano maalum yaliyofayika Geneva, Uswisi ikiwa ni siku chache kabla ya kuondoka katika wadhifa wake.
"Hatukimbii Gaza hata kidogo, lakini kile ambacho ni kweli sasa na nadhani huo ndio msingi wa hadithi hii bila shaka kwamba tunajali sana hali ya usalama huko Gaza, na inazidi kuwa mbaya zaidi kufanya kazi." Amesema Griffiths.
"Misaada inaweza kuleta mabadiliko, ndiyo maana tunahitaji kufungua njia hizi zote," Bwana Griffiths amesisitiza.
"Ndio maana tunahitaji usalama, ndiyo sababu tunahitaji gati kuanza upya na kupata usaidizi huo nje ya ufuo ikiwa hilo linaweza kufanywa pia. Tutaendelea nayo. Lakini tunawaangusha kila siku kila wakati hatuna uwezo wa kupata msaada kwa ajili ya watu wenye uhitaji.”