Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nilitumikishwa vitani nikiwa na umri wa miaka 11, Baraza la Usalama tusaidieni

Wavulana wadogo, walioachiliwa kutoka kwa makundi yenye silaha katika Mkoa wa Kivu Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wakiangalia nje ya dirisha mnamo Oktoba 29, 2021.
© UNICEF/Jean-Claude Wenga Wavulana wadogo walioachiliwa kutoka kwa makundi yenye silaha katika Mkoa wa Kivu Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wanatazama nje wakiwa karibu na dirisha.

Nilitumikishwa vitani nikiwa na umri wa miaka 11, Baraza la Usalama tusaidieni

Amani na Usalama

Mtoto aliyetumikishwa na waasi vitani huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC hii leo amehutubia wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani na kuwasihi washirikiane ili kusaidia watoto walioathiriwa na mizozo ya kivita.

Akizungumza huku utambulisho wake ukiwa umefichwa kwa ajili ya usalama wake, mtoto huyo mwenye umri wa miaka 16 sasa anasema alitekwa nyara akiwa na umri wa miaka 11 wakati wakielekea shuleni yeye na wenzake wawili.

Porini tulikuwa wapagazi wa vyakula vya wizi

Akisimulia amesema “huko porini, tulitumiwa kama wabebaji wa chakula ambacho watu wenye silaha walipora kutoka kwenye mashamba ya watu wengine, na mabegi yetu ya shule yalichomwa. Na tena, baada ya miezi mitatu wakaanza kutufundisha kutumia silaha.”  

Anasema maisha hayakuwa ya raha, kwa sababu mihogo iliyokaushwa ndio ilikuwa chakula. Aliogopa wanyama wa porini na pia kutumiwa kwenda kuiba mihogo na viazi kwenye mashamba ya watu wengine nyakati za usiku na pia kupora magari.

Virginia Gamba atoa taarifa kwa Baraza la Usalama UN kuhusu watoto na migogoro ya silaha.
UN Photo/Loey Felipe Virginia Gamba ambaye ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili dhidi ya watoto kwenye mizozo ya kivita akihutubia Baraza la Usalama.

Ukatili wa aina hii na nyinginezo ni miongoni mwa ukatili ulioripotiwa Barazani hii leo na Virginia Gamba ambaye ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili dhidi ya watoto kwenye mizozo ya kivita.

Akiwasilisha ripoti ya kila mwaka ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhus ukatili kwenye mizozo, Bi. Gamba amesema mwaka 2023 umevunja rekodi ya miaka 10 ya idadi ya matukio ya ukatili kwa watoto kwenye mizozo ya kivita.

Amesema katika mwaka huo wa 2023, Umoja wa Mataifa ulithibitisha visa vya kusikitisha 32,990 vya ukatili dhidi ya watoto 22,557, kiwango ambacho ni cha juu zaidi katika miaka takribani 10 iliyopita.

Watoto waliuawa, walikatwa viungo na kutumikishwa vitani

Matukio ya ukatili waliyokumbana nayo watoto hao mwaka 2023 ni pamoja na kuuawa, kukatwa viungo, ikifuatiliwa na kutumikishwa na kutumika vitani, kunyimwa huduma za kiutu na kutekwa nyara.

Ripoti inachambua zaidi matukio hayo ikisema watoto 5,301 waliuawa na wengine 6,348 walikatwa viungo na/au kujeruhiwa, ikiwa ni ongezeko la kutisha la asilimia 35 ikilinganishwa na miaka iliyotangulia.

“Matumizi ya silaha za vilipuzi kwenye maeneo yenye watu wengi, pamoja na mashmbulizi ya jumla dhidi ya rai ana miundombinu ya kiraia yalikuwa na madhara makubwa kwa watoto,” amesema Bi. Gamba.

Ongezeko la matukio ya watoto kutumikishwa vitani lilithibitishwa ambapo watoto 8,655 walitumkishwa na asilimia 15 kati yao walikuwa watoto wa kike ambao wanabeba mzigo mkubwa zaidi wa ukiukwaji wa haki zao pindi wanapotumikishwa.

Ubakaji na aina nyingine za ukatili wa kingono nao uliongezeka kwa asilimia 25 na kuathir iwatoto 1,470, hasa watoto wa kike. Ubakaji wa magenge uliendelea kwa kiasi kikubwa na matukio hayo yakiripotiwa zaidi Jamhuri ya Afrika ya Kati, (CAR), Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, (DRC) na Haiti.

Gaza na Israeli nako watoto walikumbwa na ukatili 2023

Huko Gaza nako, mzozo unaoendelea pamoja na Ukingo wa Magharibi na Yerusalem Mashariki na pia Israel umezidi kushamiri na kuwa na machungu makubwa kwa watoto.

Matukio ya ukatili dhidi ya watoto 4,500 yalithibitishwa na matukio mengine 23,000 ya ukatili dhidi ya watoot wa Palestina na Israeli yanaendelea kuchunguzwa.

Gamba amesisitiza, “Hebu nikumbushe pande kinzani, iwe serikali au vikosi visivyo vya kiserikali, pindi mnapoamua kupigana, basi isiwe kinyume na Chata ya Umoja wa Mataifaa, hawawezi kufanya hivyo kwa gharama ya maisha na ustawi wa watoto. Hebu niwe wazi, hakuna msamaha wowote wa kudhuru watoto wakati wa vita.”

Mwakilishi huyo Maalum amesema ripoti ya Katibu Mkuu inaelezea kinagaubaga kwamba tunahitaji kutatua changamoto mpya za amani na usalama kwa kuweka watoto kama kitovu au msingi wa hatua zetu.

Katibu Mkuu wa zamani UN Ban Ki-Moon akizungumza jukwaani wakati wa mkutano wa Baraza la Usalama UN kuhusu watoto na migogoro ya silaha.
UN Photo/Loey Felipe Ban Ki-Moon, Naibu Mwenyekiti wa Jopo la Wazee na alikuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akihutubia Baraza la Usalama kuhusu watoto katika mzozo wenye silaha.

Jopo la wazee linasemaje?

Ban Ki-Moon ambaye ni Naibu Mwenyekiti wa Jopo la Wazee amesisitiza kwamba hakupaswi kuweko na ukwepaji sheria kwa wale wanaotekeleza uhalifu dhidi ya watoto kokote pale duniani, iwe wao ni serikali au vikundi vilivyojihami kwenye tawala za kibabe au kidemokrasia.

“Utofautishaji huo hauna maana yoyote kwa wazazi wa watoto waliouawa, na vivyo hivyo kwa taasisi zinazohusika na kusimamia haki ya kimataifa.”

Baraza la Usalama saidieni watoto waliotumikishwa vitani

Akitamatisha hotuba yake mtoto kutoka DRC amesihi wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa washirikiane ili kusaidia watoto walioathiriwa na mizozo ya kivita.

“Msaada huu utaasidia kulinda watoto, utawawezesha kupata elimu, na huduma za afya, na pia utalinda watoto dhidi ya mazingira yenye ghasia ambamo kwamo haki za watoto zinakiukwa, hasa maenoe ambayo yanadhibitiwa na vikundi vilivyojihami.”