Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tufikirie njia sahihi kukabiliana na changamoto wanazokumbana nazo wakimbizi - Filippo Grandi

Kenya inaendelea kuwa miongoni mwa nchi za juu zinazohifadhi wakimbizi wengi barani Afrika.
© UNHCR/Samuel Otieno
Kenya inaendelea kuwa miongoni mwa nchi za juu zinazohifadhi wakimbizi wengi barani Afrika.

Tufikirie njia sahihi kukabiliana na changamoto wanazokumbana nazo wakimbizi - Filippo Grandi

Wahamiaji na Wakimbizi

Kamishna mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia wakimbizi, UNHCR, Filippo Grandi kupitia hotuba yake kuhusu hatua madhubuti za kushughulikia wakimbizi na kuwapa fursa, aliyoitoa leo Juni 24 katika Chuo Kikuu cha Nairobi, Kenya ameuomba ulimwengu kutafakari njia sahihi za kutumia ili kukabiliana na changamoto ambazo wakimbizi wanakumbana nazo wanapoingia katika nchi jirani kutafuta hifadhi.

Katika hotuba hiyo mbele ya wanafunzi na wanazuoni wengine, Grandi ameieleza dunia kwamba kuna takribani watu milioni 120 katika hesabu za hivi karibuni , wakiwemo wakimbizi na watu wanaotafuta hifadhi ndani ya nchi yao wenyewe, yaani wakimbizi wa ndani jambo ambalo limesababishwa na vita na machafuko yanayoendelea katika sehemu mbalimbali ulimwenguni jambo ambalo linaashiria hatari ulimwenguni kote.

Grandi amekutana na wanazuoni hao ikiwa ni hatua ya kuwashirikisha ili kutafuta njia mbadala ya kukabiriana na suala la watafuta hifadhi  na wakimbizi ulimwenguni.

“Hii ndiyo sababu, kukutana na wanazuoni, niliweka hatua madhubuti ambazo zinaweza kuchukuliwa kushughulikia sababu za msingi, kuleta utulivu wa mtiririko wa idadi ya watu, kulinda watu waliofurushwa kwa nguvu wanapohama na kuwapa fursa. Kwa sababu ni lazima tutambue kuwa fursa zipo.” Amesema Grandi.

Mwanafunzi kutoka Sudan Kusini akiwa darasani katika shule moja nchini Kenya, ambayo inaendelea kuwa miongoni mwa nchi za juu zinazohifadhi wakimbizi wengi barani Afrika.
© UNHCR/Charity Nzomo
Mwanafunzi kutoka Sudan Kusini akiwa darasani katika shule moja nchini Kenya, ambayo inaendelea kuwa miongoni mwa nchi za juu zinazohifadhi wakimbizi wengi barani Afrika.

Kenya imesaidia

Mbali na nchi ya Kenya kuwa na watu wengi wenye asili kutoka nchi jirani ambayo ni matokeo ya wakimbizi na watafuta hifadhi lakini pia uwepo wa watu hao kwa namna nyingine, umesaidia pakubwa katika ukuaji na maendeleo ya nchi ya Kenya

“Wakati mwingine kama watu ambao walilazimika kutoroka vita na mateso, wakati mwingine kama mwenyeji wa wakimbizi na watu waliohamishwa; na wakati mwingine kutoka kwa mitazamo yote miwili, mnapaswa kujivunia kwamba, simulizi iliyopo nchini Kenya inabaki kuwa ya mshikamano.” Amesema Grandi.

Grandi ameeleza kwa watunga sera kwamba ni wakati sasa wa kuandika juu ya uwezekano wa kutatua changamoto hii ambayo inaigusa dunia nzima huku akiwaasa wanazuoni katika chuo kikuu cha Nairobi na ulimwenguni kwa ujumla kutumia maarifa waliyo nayo ili kutafuta suluhisho la tatizo hili.

Siku za hivi karibuni mwezi huu wa juni, Kamishna Grandi alitembelea katika Chuo Kikuu cha Georgetown, Washington, DC na kuzungumza kuhusu wimbi kubwa la watu wanaokimbilia nchi jirani kutafuta hifadhi na hatari ambazo wanakabiliana nazo wakiwa safarini huku akigusia picha za kutisha za wakimbizi na wahamiaji katika kambi za wakimbizi nchini Libya zinavyotafsiri ugumu ambao watu hao wanaupitia ambao hastahili mtu yeyote kupitia ugumu kama huo.