Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utoaji wa vitambulisho vya kitaifa kwa wakimbizi nchini Ethiopia waboresha maisha yao

Utoaji wa vitambulisho kwa wakimbizi nchini Ethiopia waboresha maisha yao.
UNHCR
Utoaji wa vitambulisho kwa wakimbizi nchini Ethiopia waboresha maisha yao.

Utoaji wa vitambulisho vya kitaifa kwa wakimbizi nchini Ethiopia waboresha maisha yao

Wahamiaji na Wakimbizi

Nchi ya Ethiopia inatekeleza mpango wa kihistoria wa utoaji wa vitambulisho vya kitaifa unaojumuisha wakimbizi na wasaka hifadhi chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia mradi wake wa vitambulisho kwa maendeleo (D4D) unaolenga kuboresha ujumuishi, utendaji na usimamizi wa vitambulisho vya kitaifa na mifumo ya usajili wa raia mradi unaotekeleza kivitendo Mkataba wa Kimataifa kwa wakimbizi.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya wakimbizi UNHCR tayari baadhi ya wakimbizi walioko katika jiji la Addis Ababa wameshasajiliwa na kupatiwa vitambulisho vyao na wameanza kupata huduma ambazo hapo awali walikuwa wakishindwa kuzifikia kwa kutumia vitambulisho vyao vya ukimbizi pekee. 

Mmoja wa wanufaika hao ni Ibtisam ambaye ni mkimbizi kutoka Yemen ameishi nchini Ethiopia kwa miaka 9 sasa. Hivi karibuni alipokea kitambulisho chake cha kidijitali na kuweza kupata leseni ya biashara. Kisha aliweza kufungua kioski cha kuuza kahawa kwenye soko kubwa zaidi nchini Ethiopia liitwalo, Mercato. 

Ibtisam, mkimbizi kutoka Yemen ambaye ameishi nchini Ethiopia kwa miaka 9 sasa amepokea kitambulisho chake na sasa anaendesha biashara yake.
UNHCR
Ibtisam, mkimbizi kutoka Yemen ambaye ameishi nchini Ethiopia kwa miaka 9 sasa amepokea kitambulisho chake na sasa anaendesha biashara yake.

Ibtisam akiwa ameshikilia kitambulisho mkononi anasema hii ni leseni yangu ya biashara na hii ni kadi yangu ya Fayda. “Huduma nyingi sasa ninaweza kuzipata kwa sababu nina kitambulisho cha Fayda. Kwa taasisi ambazo awali hazikutambua kitambulisho cha ukimbizi, sasa kuna namba maalum unaingiza kwenye mfumo na unapata huduma unazohitaji.”

Fayda ni kitambulisho chenye namba maalum ambacho hutolewa na serikali ya Ethiopia kwa wakazi wanaokidhi vigezo vinavyotambuliwa na Mradi wa Taifa wa vitambulisho. Wananchi wanapatiwa vitambulisho hivyo kwa kutumia teknolojia ya kuchukua alama za mwili ikiwemo vidole.

Elizabeth Tan ni Mkurugenzi wa masuala ya kimataifa ya Ulinzi, kutoka UNHCR na anasema “Hivi karibuni serikali ya Ethiopia ilizindua vitambulisho vyake vya kitaifa vya kidijitali, na imejumuisha wakimbizi kwenye mfumo wake wa kitaifa. Mpaka sasa zaidi ya wakimbizi 3000 wamekwisha patiwa vitambulisho na mpango huu unatarajiwa kusambaa katika nchi nzima ya Ethiopia.”

Soundcloud

Lengo la mradi huu ni kuwafikia hadi wakimbizi 77,000 wanaoishi katika jiji la Addis Ababa kabla hawajapanua zaidi wigo wa utoaji wa vitambulisho hivyo kwa wakimbizi wote walioko nchini Ethiopia 

Ibtisam akiwa mwenye furaha kwa fursa anazozipata sasa kwakuwa na kitambulisho cha Fayda anaeleza licha ya kuwa kupata vitambulisho bado hakuondoi changamoto zote anazobailiana nazo lakini anamshukuru Mungu haombi kwa mtu. “Kuishi katika mazingira ya amani pekee ni jambo kubwa kwangu. Nimeridhika na kuweza kuwapatia mlo watoto wangu. Ninavyoinama na kuwatengenezea kahawa wateja wangu, sioni aibu, ninachojali ni kuwa mimi sio ombaomba, sio mzigo kwa taifa hili na ninaweza kusimama kwa miguu yangu mwenyewe. Ilimradi nina afya njema, ninachotaka ni kufanya kazi na kuishi.