Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usalama mtandaoni kwa mtazamo wa Kiafrika – Nnenna Ifeanyi-Ajufo

Nnenna Ifeanyi-Ajufo, Profesa wa sheria na teknolojia katika Shule ya Sheria ya Leeds, Chuo Kikuu cha Leeds Beckett, Uingereza
UN Photo/Evan Schneider
Nnenna Ifeanyi-Ajufo, Profesa wa sheria na teknolojia katika Shule ya Sheria ya Leeds, Chuo Kikuu cha Leeds Beckett, Uingereza

Usalama mtandaoni kwa mtazamo wa Kiafrika – Nnenna Ifeanyi-Ajufo

Utamaduni na Elimu

Nchi nyingi za Kiafrika zinakabiliwa na changamoto za kipekee kutokana na nafasi zao kidijitali, na ukosefu wao wa uwezo na miundombinu ya kutosha, amebainisha Nnenna Ifeanyi-Ajufo wakati wa hotuba yake katika mjadala wa ngazi ya juu uliofanywa na Baraza la Usalamala Umoja wa Mataifa leo Alhamisi Juni 20, ukilenga: "Kudumisha amani na usalama wa kimataifa: Kushughulikia vitisho vinavyoendelea mtandaoni."

Nnenna Ifeanyi-Ajufo ambaye ni profesa wa sheria na teknolojia katika Shule ya Sheria ya Leeds, Chuo Kikuu cha Leeds Beckett, Uingereza, anahudumu kama makamu mwenyekiti wa Kikundi cha Wataalamu wa Usalama wa Mtandao wa Muungano wa Afrika (AUCSEG) na amehusika kikamilifu katika kushauri Kamisheni ya Muungano wa Afrika (AUC) na nchi wanachama wa Afrika kuhusu mifumo iliyopo ya kisheria ya kimataifa, kikanda na kitaifa kuhusiana na utawala wa mtandao, pamoja na kukuza usalama wa mtandao barani Afrika.

Ifeanyi-Ajufo ameeleza kuwa Muungano wa Afrika (AU) umelipa kipaumbele suala la usalama wa mtandao, kulijumuisha katika Ajenda ya 2063 na kupitisha mifumo kama vile Makubaliano ya Muungano wa Afrika kuhusu Usalama wa Mtandao na Ulinzi wa Data.

Amefafanua kwamba mtazamo huu wa kikanda, ikiwa ni pamoja na msimamo wa pamoja wa Kiafrika kuhusu sheria ya kimataifa katika mtandao na juhudi za kujenga uwezo, unaonesha msimamo thabiti katikati ya ongezeko la vitisho vya mtandao.

Aidha amebainisha kuwa matukio ya hivi karibuni, kama vile mashambulizi ya mtandao kwenye makao makuu ya Kamisheni ya Muungano wa Afrika na miundombinu muhimu nchini Kenya, yanasisitiza haja ya haraka ya kuimarisha hatua za usalama wa mtandao.

“Kwa mfano, Kenya ilikabiliwa na zaidi ya mashambulizi ya mtandaoni milioni 860 mwaka wa 2023 pekee, na kuathiri miundombinu ya habari nchini humo.” Ameeleza mtaalamu huyo wa sheria na masuala ya mtandao.

Changamoto hizi zinaangazia mistari usi wazi kati ya watendaji wa serikali na wasio wa serikali wanaohusika katika vita vya mtandao, amesema akiongeza kwamba kushughulikia masuala haya kunahitaji mikakati mahususi inayotambua tofauti za kikanda huku ikiimarisha mifumo ya kimataifa ya usalama wa mtandao ili kulinda dhidi ya matishio yanayoibuka katika anga la mtandao.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (katikati) akihutubia katika mjadala wa wazi wa ngazi ya juu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu usalama wa mtandao.
UN Photo/Manuel Elías
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (katikati) akihutubia katika mjadala wa wazi wa ngazi ya juu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu usalama wa mtandao.

Katibu Mkuu UN

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, yeye amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa ili kukabiliana na matishio yanayoongezeka katika ‘anga la mtandao’, uhalifu wa mtandaoni, na utumiaji silaha wa zana za kidijitali, akiangazia maendeleo ya haraka ya teknolojia ya kidijitali na athari zake za kuleta mabadiliko katika uchumi na jamii kote ulimwenguni.

Katibu Mkuu amesema, hii ni mara ya pili kwa Baraza la Usalama kufanya kikao rasmi kuhusu suala hili akitaka kuunganishwa kwa masuala yanayohusiana na mtandao katika maazimio ya sasa ya Baraza la Usalama.

Pia ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za kuzuia, kuweka mifumo inayoendana na haki za binadamu, na mkataba ujao wa uhalifu wa mtandaoni ili kupunguza hatari na kuimarisha mnepo wa mtandao wa kimataifa, akisisitiza jukumu muhimu la juhudi za kimataifa katika kulinda amani na usalama wa kimataifa.